loader
Ahueni bei mpya za maji vijijini yaja

Ahueni bei mpya za maji vijijini yaja

WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso ametoa maelekezo kwa mamlaka zote za vijijini nchi nzima kupitia upya bei za maji na kuahidi kuwa baada ya Bunge la 12, Mkutano wa Saba unaoendelea atatoa bei mpya za maji vijijini.

Alisema hatua hiyo inatokana na kubaini kuwa kwa sasa bei za vijijini za maji ziko juu kuliko zile za mijini kwa kiwango kilekile cha maji kinachotumika, jambo alilosema si sawa.

Akihitimisha hoja yake ya Bajeti ya mwaka 2022/23 iliyopitishwa rasmi na bunge juzi, Aweso alisema amejifunza kuwa bei za mijini ikiwemo Dar es Salaam wanalipa kwa uniti moja Sh 1,600 wakati vijijini ndoo moja ya lita 20 inalipiwa Sh 50. “Uniti moja ni sawa na ndoo 1,000.

Maana yake ndoo za lita 20 zinazolipiwa kila moja Sh 50 kijijini wanalipa Sh 2,500. Hili haliwezekani,” alisema Aweso. Alisema kutokana na ukweli huo, ametoa maelekezo kwa mamlaka zote za maji vijijini kupitia bei hizo za vijijini na bei mpya sasa itatolewa baada ya Bunge hilo kuhitimisha kazi zake.

Aweso kwa ujumla alisema tatizo la malalamiko ya bei za maji ambalo limelalamikiwa na wabunge wengi waliokuwa wakijadili hoja hiyo ya bajeti ya maji, zimeanza kufanyiwa kazi ikiwemo kuanza mchakato wa kufunga mita za maji za kulipa kabla ya kutumia maji kama ilivyo kwa umeme.

Alisema wizara hiyo ina wajibu wa kulishughulikia hilo ili kuondoa tatizo hilo kwani haiwezekani mwananchi ametumia maji ya Sh 15,000 lakini analetewa bili ya Sh 120,000. Aweso alisema pamoja na kuhamasisha wasomaji mita wa wizara hiyo kuwa waadilifu, pia wameanza kuhakikisha pia wanatumia teknolojia hiyo ya kisasa ili kupata bili ya uhakika. “Kizuri huigwa. Tunaona wenzetu wa Tanesco wana mita za Luku.

Nimeshatoa maelekezo na sasa wadau wamekuja, tunajifunza kuhusu hizi mita kabla ya kumfungia mwananchi. Lakini katika hili mwarobaini wake ni pre-paid mita (kulipa kabla ya kutumia),” alisisitiza. Kuhusu hoja za wabunge za miradi kutokamilika, alisema Rais Samia Suluhu Hassan hajakaa muda mrefu bali mwaka mmoja tu, ndio maana hajaweza kufikia maeneo yote lakini kazi kubwa tayari ameshaifanya.

“Leo hii haijawahi kutokea bajeti ya maji itekelezwe kwa asilimia 80, lakini imetekelezwa kwa asilimia 90 na kwa mara ya kwanza inaposomwa bajeti hii ya maji iliyochangiwa na wabunge 65, wizara isifiwe, tunashukuru sana kwa kututia moyo,” alisisitiza.

Kuhusu upotevu wa maji, alikiri kuwa ni aibu suala hilo kuendelea kutokea lakini alionya kuwa kiwango cha maji cha asilimia 36 kinachopotea si kweli kinapotea bali kinaibiwa kutokana na baadhi ya watu wasiowaaminifu kujiunganishia maji kinyemela.

Alisema moja ya changamoto kubwa iliyokuwa ikiathiri Wizara ya Maji ni miradi chechefu, miradi isiyokamilika na iliyokamilika lakini haitoi maji, ndio maana ikaanzishwa Mamlaka ya Maji Mijini na Vijijini (RUWASA).

Aweso alisema katika kipindi kifupi cha mwaka mmoja, kati ya miradi 177 miradi 127 imeshakwamuliwa na Watanzania wanapata majisafi na salama.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/f2d902494c09838e46849f6ffd2ba150.jpeg

Rais Samia Suluhu Hassan, ametajwa kuwa miongoni ...

foto
Mwandishi: Na Halima Mlacha, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi