loader
Familia zinafunda ‘panya road’?

Familia zinafunda ‘panya road’?

NIPO nyumbani kwa Baba na Mama Chichi. Lakini Chichi mwenyewe hayupo nyumbani.

Amekwenda kucheza na wenzake. Tangu asubuhi yuko ‘michezoni’ hadi aliporejea nyumbani kwa ajili ya kupata mlo wa mchana.

Si mama wala baba au mwanafamilia anayefahamu anakochezea mtoto huyo wa kiume mwenye umri chini ya miaka 10. Anacheza nini? Wapi? Na nani?...si suala wanaloshughulika nalo.

Chichi amerudi akiwa amevaa saa mpya, viatu ambavyo si vyake, ameshika biskuti na pipi. Wazazi wanaridhika na majibu ya mtoto kuwa amepewa vitu hivyo au amebadilishana na rafiki zake.

Kesho yake, mtoto jirani ambaye ni rafiki wa Chichi anampitia waende kucheza kama ilivyo kawaida. Rafiki huyo anaishi na mama yake pekee, ambaye wakati mwingi yuko mtaani akichuuza samaki aweze kutunza familia!

Leo ni Siku ya Kimataifa ya Familia ambayo huadhimishwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kwa mujibu wa Tamko Namba 47/237 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililotolewa Septemba 20, 1993.

Akizungumzia maadhimisho hayo ambayo hufanyika kila Mei 15, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima anasema jukumu la msingi la familia ni kulea watoto kwa sababu familia ndiyo chimbuko la uzao wa watu wote duniani.

Anasema malezi ya mtoto katika familia yanahusu kumpa mahitaji ya msingi kulingana na ukuaji wake, kumwendeleza kielimu, kiimani, kitabia na kumfanya awe na mwelekeo na mtazamo wa mtu mwenye fikra chanya na anapokuwa mtu mzima aweze kushiriki vema katika harakati za maendeleo ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na utawala bora. Malezi yana mchango mkubwa katika kuleta utengamano wa kitaifa na hivyo kudumisha umoja, amani na mshikamano miongoni mwa wanajamii kwa kuwa mtoto aliyelelewa vema na familia atakuwa mzalendo, mchapakazi, mwenye bidii na kujituma katika kipindi cha utu uzima.

Ni tofauti na mtoto asiyepata malezi bora. Gwajima anabainisha kuwa familia inao mchango mkubwa katika kuwaandaa watoto watakaokuja kuwa nguvu kazi yenye tija kwa maendeleo ya taifa letu. Wito huu wa Waziri Gwajima ni ujumbe muafaka ambao familia mbalimbali ikiwamo ya mtoto Chichi na rafiki yake, zinapaswa kuuzingatia.

Anakumbusha kuwa maadhimisho haya yanawagusa baba, mama na watoto katika muktadha wa kifamilia ili waweze kukaa kama familia na kujadili changamoto mbalimbali na kuweka mipango ya kutatua. Ni wakati sasa kwa familia zote kujadili kwa undani uhusiano uliopo kati ya wazazi/ walezi na watoto wao ili kujua hatua za kuwaepusha kuingia katika vitendo viovu na vya kihalifu vinavyoweza kugharimu si tu maisha ya watoto, bali na ya jamii kwa ujumla.

Mathalani, malezi anayopewa mtoto Chichi hayana tija katika ulimwengu wa sasa uliojaa ukatili na matendo maovu yanayochochewa na makundi rika.

Wanafamilia wanapaswa kujadiliana na kuweka misingi ya malezi kwa watoto itakayoepusha kuwapa uhuru uliopitiliza unaoweza kuwaingiza kwenye vishawishi vya uhalifu. Kwa mfano, ukiangalia familia ya Chichi, baba na mama yake wapo ni tofauti na rafiki yake anayelelewa na mzazi mmoja (mamama).

Lakini wamekosa busara na maarifa ya kumlea mtoto katika njia impasayo. Hawataki kumuudhi mtoto wao.

Amekuwa huru kupitiliza, jambo ambalo ni hatari sana. Kitendo cha mtoto kwenda kusikojulikana, akarudi na vitu au fedha ambavyo mzazi hujampa na wakati huo huo ukakaa kimya bila kuhoji alikovipata, ni ‘bomu’ linaloweza kuathiri familia, mtoto mwenyewe na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wa rafiki yake Chichi, changamoto aliyonayo ni mama yake kulemewa na mzigo wa malezi na matunzo ya familia. Matokeo yake, anakosa uangalizi wa karibu kwani mama yake hana hata kipato cha kumlipa mwangalizi wa watoto nyumbani! Hili nalo linatoa ujumbe kwa familia kujadili suala zima la migogoro ya ndoa na hata baadhi ya wazazi (wanaume) kutelekeza watoto na kulazimu mama kubeba mzigo wote wa malezi na kujitafutia kipato.

Hivi karibuni, nilisoma habari juu ya watoto 70 wanaoshikiliwa mkoani Mbeya kutokana na operesheni dhidi ya wanaoishi katika mazingira yasiyo rasmi, yanayotajwa kuwa chanzo cha kuzalisha wahalifu wanaohatarisha amani ndani ya jamii.

Katika hao waliokamatwa, wapo waliotelekezwa na wazazi au walezi wao, wengine walikimbia familia zao kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ugumu wa maisha na baadhi kufanyiwa ukatili.

Ni ukweli usiopingika kwamba, watoto aina ya Chichi, wanaweza kujiingiza kwenye vikundi vya kihalifu ikiwamo panya road na kuleta majuto kwa familia. Kama alivyoshauri Dk Gwajima, katika maadhimisho ya siku ya familia leo, ni vyema wanafamilia na jamii wakajadili na kutafakari nafasi yao katika malezi na hatma ya watoto.

Tafakuri iwe ni, je, familia zinalea watoto ambao wakiwa watu wazima watashiriki vema harakati za maendeleo ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na utawala bora au zinazalisha ‘panya road’?

  • 0736525127
https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/d7a5f63d3aa023a1dbab39ab62b9bb45.JPG

NIPO nyumbani kwa Baba na Mama Chichi. ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi