loader
Makongamano ya uwekezaji yafanyike EAC

Makongamano ya uwekezaji yafanyike EAC

JUMATATU Mei 09, mwaka huu, lilifunguliwa Kongamano la pili la siku tatu la kimataifa la uwekezaji na biashara lililohusisha nchi tano zilizo jirani na Ziwa Tanganyika mjini Kigoma, Tanzania. Kongamano hilo lilifunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye likiwahusisha wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara likiwa limeambatana na maonesho ya biashara kutoka nchi husika.

Takriban waoneshaji 300 walikuwepo kwenye maonesho hayo ya bidhaa mbalimbali kutoka maeneo mbalimbali ya nchi za Tanzania, Rwanda, Zambia, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Katika kongamano hilo, Katibu Mkuu wa chama cha CNDD-FDD cha nchini Burundi, Reverien Ndikuriyo, alisema kongamano litasaidia kujua nini cha kufanya kuongeza na kukuza biashara katika nchi washirika.

Kimsingi, makongamano kama hayo yanapaswa kuwapo kwa kiwango cha kutosha hata katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) huku pia, yakizialika nchi nyingine kama wageni watazamaji na wanunuzi wa bidhaa za nchi wanachama. Kwetu sisi, tunaona hili ni jambo jema linalopaswa kufanywa hata mara mbili au tatu kwa mwaka kwa mtindo wa mzunguko katika nchi za EAC.

Tunasema, hilo litasaidia wajasiriamali, wafanyabishara na wawekezaji mbalimbali kubadilishana mawazo na kutafuta au kupata fursa mbalimbali za kibiashara na kiuchumi yakiwamo masoko ya bidhaa na huduma wanazozalisha.

Tunasema, ili kufanikisha hilo, uhusiano imara zaidi miongoni mwa nchi wanachama wa EAC hauna budi kujengwa kwa viongozi wa nchi na wadau mbalimbali kutembeleana na kufanya mijadala inayolenga pamoja na mambo mengine, kubaini na kuondoa vikwazo vilivyopo kadiri imavyowezekana kwa manufaa ya nchi zote husika.

Tunasema kwa kuzingatia makongamano haya tunaweza kuimarisha diplomasia ya kiuchumi na kila mkazi wa Afrika Mashariki akafaidi matunda yake.

Ndiyo maana tunasema, makongamano ya uwekezaji kama lililofanyika Kigoma likihusisha nchi tano zilizojirani na Ziwa Tanganyika yawe endelevu na yafanyike kwa nchi za EAC.

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi