loader
Simba, Azam kumalizana leo

Simba, Azam kumalizana leo

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba leo watakuwa ugenini Uwanja wa Chamazi Complex kumenyana na wenyeji wao Azam katika mechi ya ligi.

Kwa miaka ya karibuni Azam FC imeonekana mnyonge mbele ya Simba baada ya kushindwa kutamba kila zinapokutana.

Takwimu zinaonesha katika msimu wa 2019 hadi sasa, timu hizo zimekutana mara saba michezo ya Ligi Kuu na kati ya hizo, Simba imeshinda mara nne na kupata sare tatu.

Timu hizo zinafahamiana kwasababu zilikutana fainali ya Kombe la Mapinduzi Januari mwaka huu na Simba ikashinda bao 1-0 na kuondoka na taji kisha mchezo wa mzunguko wa kwanza wekundu walishinda mabao 2-1.

Timu hizo zinakutana zikiwa katika viwango tofauti, Simba bado iko katika mbio za ubingwa ikishika nafasi ya pili kwa pointi 49, hivyo bado ina uhitaji wa ushindi ili kuendelea kujiweka mazingira mazuri ya kutetea taji.

Lakini Azam FC wanaoshika nafasi ya tano kwa pointi 32 tayari hawako katika mbio za ubingwa ila watahitaji kumaliza nne bora ili wapate nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao.

Mchezo huo kila mmoja ana nafasi ya kushinda kutegemea na mbinu watakazoingia nazo.

Kocha wa Simba, Pablo Franco alisema watajaribu kucheza kwa uwezo wao ili kuondoka na pointi tatu.

“Azam FC ni timu nzuri, tulikutana nao Kombe la Mapinduzi na mzunguko wa kwanza, sote tuna timu nzuri na tunahitaji ushindi, naamini utakuwa mchezo mzuri na wenye nguvu, tumejiandaa vizuri na wachezaji wako tayari kwa mchezo,” alisema.

Kwa upande wake Kocha msaidizi wa Azam FC, Omar Nasser alisema wanawaheshimu Simba ni mabingwa watetezi, ni timu nzuri yenye wachezaji wazuri na kwamba wamejipanga kuingia kwa tahadhari na wako tayari kupambana nao.

“Simba imekuja nyumbani mara tatu na ikatoka sare, najua walikuwa na mfululizo wa kufunga lakini tumejipanga katika mchezo huu, tutajua nani ataibuka na ushindi baada ya dakika 90,” alisema.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi