loader
Geita wajipanga chanjo ya polio kila nyumba

Geita wajipanga chanjo ya polio kila nyumba

MRATIBU wa Huduma za Chanjo mkoani Geita, Wille Luhangija amesema jumla ya watoa huduma 1,225, wameandaliwa kupita mtaani nyumba kwa nyumba, ili kutoa chanjo ya polio kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Wille ameeleza katika hafla ya uzinduzi wa chanjo ya polio mkoani Geita, iliyozinduliwa kwenye mtaa wa Lwenge uliopo mjini Geita na kusisitiza waratibu hao watatekeleza hilo kwa miongozo ya serikali.

Amesema timu hiyo itajumuisha viongozi kutoka Wizara ya Afya, viongozi kutoka Tamisemi, waratibu wasimamizi wa halmashauri na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na viongozi wa mitaa, ambao watapita na kusimamia.

Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk. Japhet Simeo amebainisha kuwa mkoa wa Geita unatarajia kutoa chanjo kwa watoto 553,228, ambao watafikiwa katika takribani kaya 324,000 zilizopo mkoani hapa.

“Madhara ya ugonjwa wa polio ni kupooza, lakini asilimia 10 ya watoto wanaopata ugonjwa wa polio wanapoteza uhai, kwa sababu inashambulia mishipa ya fahamu na inapogusa mishipa ya fahamu inayohusiana na upumuaji mtoto anapoteza uhai,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Wilson Shimo, amesema Wilaya ya Geita inatarajiwa kuchanja takribani watoto 256,000 katika halmashauri mbili, kati ya hao zaidi ya watoto 57,376 wanatokea halmashauri ya mji na watoto 197,997 kutoka halmashauri ya wilaya.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule amesema mkoa umejipanga kuwachukulia hatua wazazi wote ambao hawatajitokeza kuwapelekea watoto wenye sifa za kupata chanjo ya polio, kwani chanjo hiyo ni bure na haki ya mtoto.

foto
Mwandishi: Yohana Shida, Geita

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi