loader
Ummy akemea upotoshaji chanjo ya polio

Ummy akemea upotoshaji chanjo ya polio

WIZARA ya Afya imekemea upotoshaji kuhusu chanjo ya matone ya kupooza (polio) na imetaka wanaofanya hivyo wachukuliwe hatua za kisheria.

Waziri wa wizara hiyo, Ummy Mwalimu alisema hayo jana wakati akizindua kampeni ya kitaifa ya chanjo hiyo kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Chanjo hiyo ilianza kutolewa jana na kazi hiyo itahitimishwa Mei 21 mwaka huu.

Watoto 10,500,000 wanatarajia kuchanjwa wakiwemo 10,295,316 Tanzania Bara na 281,489 visiwani Zanzibar.

Ummy alisema kumekuwa na taarifa kwenye mitandao ya kijamii za upotoshaji kuhusu chanjo hiyo na kwamba kuna watu wamerekodi clip inayopotosha kwamba inaua.

"Nilimuomba Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye kuangalia kuna watu wamerekodi na jambo hilo sio zuri kwenye jamii, upotoshaji sio mzuri," alisema na kuongeza:

"Wanatangaza taarifa za kupotosha kuwa chanjo hii ina madhara, upotoshaji kama huu haufai wanaofanya hivi wachukuliwe hatua na vyombo vya sheria." 

Ummy alisema ugonjwa wa polio umekuwa ukiathiri watoto chini ya miaka mitano na huduma za chanjo zitafanyika katika zahanati, vituo vya afya na hospitali pia kwa njia ya mkoba na tembezi na watoto watafuatwa walipo.

Alisema Tanzania ilianza kutoa chanjo ya polio mwaka 1975 na kwamba mtoto anatakiwa kupata chanjo nne ikiwemo anapozaliwa, mtoto anapofikisha wiki nne, anapofikisha wiki 10 na mtoto anapofikisha wiki 14.

Alisema kuanzia mwaka 1995 hadi 1996 Tanzania haikuwahi kupata mgonjwa.

"Mwaka 1996 alipatikana mgonjwa mmoja ambaye kwa sasa ana miaka 28 ambaye aligunduliwa na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Masasi wakati huo, Dk William Mengeye," alisema.

Waziri huyo aliwataka wazazi na walezi wenye watoto chini ya umri wa miaka mitano wahakikishe watoto wao wanapata chanjo hiyo muhimu.

Alisema mwaka 2015 Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza Tanzania kuwa ni nchi isiyokuwa na ugonjwa wa polio.

Alisema Februari mwaka huu walipokea taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa nchi ya Malawi imepata mgonjwa wa polio na Malawi ni jirani na Tanzania.

Alisema kuwa maagizo ya WHO taifa lilitakiwa kuchukua hatua, kuchanja watoto wote kwenye mikoa inayopakana na Malawi ikiwemo Njombe, Ruvuma, Mbeya na Songwe na walifanikiwa kuchanja watoto 1,138,639 wakati lengo lilikuwa kuchanja watoto 975,839. Pia alisema WHO imethibitisha ugonjwa huo kuingia nchini Msumbiji.

Alisema kuwa utoaji wa chanjo nyingine kwa ajili ya watoto itaendelea kama kawaida.

"Pelekeni watoto wakapate chanjo, mtoto asipopata chanjo anaweza kuwaambukiza wengine kwa kutokuwa na kinga," alisema.

Kwa upande wake, Issa Ibrahim (28) akitoa ushuhuda wake alisema alipata ugonjwa wa polio akiwa na miaka mitatu wakati huo ilikuwa mwaka 1996.

"Niliambiwa nilidondoka ghafla nje ya nyumba, baadae nilikutwa na polio ugonjwa ambao hauna tiba, wazazi na walezi wenye watoto chini ya miaka mitano wawapatie watoto wao chanjo hiyo ni muhimu," alisema.

Alisema kuwa mguu wake wa kushoto umepooza hawezi kufanya kazi ngumu wala kutembea umbali mrefu. "Wazazi wasidharau chanjo hiyo," alisema.

Mkurugenzi wa Afya kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dk Ntuli Kapologwe alisema watashirikiana kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, Stanslaus Nyongo alisema kinga ni bora kuliko tiba hivyo Bunge litashirikiana na serikali ili zoezi hilo lifanikiwe na kuwaepusha watoto na walemavu.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Antony Mtaka alisema mkoa huo umepokea dozi 551,029 za chanjo ya matone ya kupooza (polio) na wanatarajia kuwafikia watoto 479,156 kutoka katika halmashauri zote nane.

Alisema Mkoa wa Dodoma umepanga kuwa na timu za uchanjaji 1,151 ambazo zitapita nyumba kwa nyumba kuanzia Mei 18 hadi 21, mwaka huu.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/c487ed0ff4992d1f8d002373ba026859.jpg

MKURUNGENZI wa Kampuni ya Prosperity ...

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi, Dodoma

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi