loader
Ufaransa yakaribishwa kulima alizeti, kujenga viwanda

Ufaransa yakaribishwa kulima alizeti, kujenga viwanda

SERIKALI imekaribisha wafanyabiashara kutoka Ufaransa waje kulima alizeti na kujenga viwanda vya mafuta ya kupikia.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amewaeleza kuwa nchi inakabiliwa na uhaba wa mafuta ya kula kutokana na uzalishaji mdogo wa alizeti na mawese.

Aliwaeleza Dar es Salaam kuwa uhaba huo pia umetokana na athari za vita baina ya Urusi na Ukraine iliyosababisha bei ya mafuta kupaa hivyo serikali iko tayari kuwapa ardhi kwa ajili ya kilimo hicho.  

"Kwa kuzingatia hali iliyotokea duniani baada ya Covid-19 na haya ambayo yanaendelea ya mzozo wa nchi mbili, Urusi na Ukraine, ambao ni wazalishaji wakubwa wa mafuta ya kula; nitoe wito kwa wawekezaji kuwa Tanzania inaweza kulisha dunia kwa suala la mafuta ya kula mkiwekeza kwenye eneo hilo," alisema Dk Mwigulu.

Alisema hayo alipokutana na kuzungumza na ujumbe wa Shirikisho la Wafanyabiashara wa Sekta Binafsi kutoka Ufaransa (MEDEF) unaohusisha kampuni 41 na Taasisi ya Biashara ya Ufaransa.

Ujumbe wa shirikisho hilo upo nchini kwa mwaliko wa Rais Samia Suluhu Hassan alioutoa wakati wa ziara nchini Ufaransa hivi karibuni.

Dk Mwigulu alisema kuna mikoa zaidi ya minane inayofaa kwa uzalishaji wa mbegu za mafuta ya alizeti na mikoa mingine zaidi ya minne inayofaa kwa kilimo cha chikichi inayozalisha mafuta ya mawese na akawaalika kuchangamkia fursa hiyo ili kutosheleza soko la ndani na kuilisha dunia.

Alisema wawekezaji kutoka Ufaransa na kwingineko wanakaribishwa kuwekeza nchini kwa sababu kuna fursa nyingi katika kilimo, ujenzi wa miundombinu, maliasili, bandari, uvuvi na usafirishaji.

"Sisi Wizara ya Fedha na Mipango tumeifanyia kazi changamoto ya utozaji kodi mara mbili na suala hilo liko hatua za mwisho za maamuzi na tutatekeleza nyenzo ya blue print ili kutengeneza mazingira bora ya uwekezaji na kufanyia biashara; tunawahakikishia kwamba tutashirikiana na sekta binafsi kwa sababu sekta hiyo ndio injini ya kukua kwa uchumi," alisema Dk Mwigulu.

Dk Mwigulu aliwaeleza kuwa kuna soko la uhakika nchini, Afrika Mashariki na nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa aliyeambatana na ujumbe huo, Samuel Shelukindo alisema wawekezaji hao wameona fursa ya kuwekeza na wako tayari kuwashawishi wawekezaji wengine waje kutafuta fursa hizo.

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi