loader
Heshima Stendi ya Magufuli ulinzi wa hadhi, mapato

Heshima Stendi ya Magufuli ulinzi wa hadhi, mapato

OPERESHENI ya kuondoa wazururaji na mawakala feki katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli kilichopo Mbezi Luis, Ubungo, Dar es Salaam inapaswa kuwa endelevu ili kukipa kituo hicho heshima na kuzuia upotevu wa mapato.

Kituo hicho kilizinduliwa na Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli, Februari 24, mwaka 2021 nakutoa maagizo kadhaa ambayo hayakusimamiwa vyema na sasa uongozi wa stendi hiyo umechukua maamuzi magumu yakuhakikisha wazururaji na matapeli hawatekelezi yao katika eneo hilo.

Stendi hiyo inahudumia mabasi zaidi ya 3,000 kila siku na kutoa fursa ya wafanyabiashara kuendesha shughuli zao kwa mujibu wa sheria na taratibu.

Akizindua stendi hiyo, Magufuli aliwataka wafanyabiashara wadogo maarufu wamachinga kuruhusiwa kufanya biashara katika kituo hicho.

Magufuli alisema wakati stendi hiyo ikitarajia kupokea mabasi 3,000 abiria watahitaji huduma na si wote wataingia katika kituo hicho, hivyo wamachinga watakaouza vyakula wanaruhusiwa wakiwemo mama lishe kwani serikali inajali wananchi.

“Vitu vilivyomo hapa havitamsaidia mmachinga hataingia mle, sasa nitoe wito kwako waziri na mkurugenzi mmenipa jina nalikubali kwa ajili ya kuwatetea hawa watu, nataka niwe balozi wao, nataka itakavyoanza hawa wamachinga wasifukuzwe kwa sababu ni kwao, mkiandika jina Magufuli stendi halafu wamachinga wakawa wananyanyaswa hapa sihitaji hilo.”

“Nikueleze Waziri (Selemani Jafo-Tamisemi wakati huo) inawezekana umejichongea kwa kuiita hii stendi jina la Magufuli, nataka yafanyike haya ambayo Magufuli ninataka yafanyike. Wananchi waruhusiwe mpanue maeneo,” alisema Magufuli.

Baada ya nukuu hiyo wapo watu ambao wanayatafsiri vibaya maneno yake kwamba machinga wanapaswa kuingia ndani bila utaratibu lakini ukweli ni kwamba, Magufuli aliwataka wapanue maeneo nje ya kituo na kuwapa wamachinga wakiwamo mama lishe kuendesha shughuli zao.

Wapo baadhi ya watu waliokuwa wakiendesha biashara zao kupitia stendi hiyo tangu ikiwa Mnazi Mmoja, Kisutu, Ubungo na sasa Mbezi wamekuwa wakikiuka utaratibu kwa kisingizio cha kauli ya Magufuli.

Mara kwa mara abiria walikuwa wakilalamikia mawakala kwa kuwatapeli na hata kuwapandisha kwenye magari ambayo si chaguo la abiria ama hata kuwasababishia usumbufu garini ambapo siti moja inakuwa imelipiwa na abiria wawili lakini hata muda wa kuondoka usiwe sahihi pasipokujali umuhimu wa safari ya mteja.

Kwa kuliona hilo uongozi wa stendi umeamua kutangaza kiama cha mawakala feki pamoja na wazururaji wanaoshinda kituoni hapo bila kazi maalumu.

Operesheni hiyo imeibua mambo huku baadhi ya mawakala wakilalamika kunyanyaswa na uongozi wa stendi kama walivyolieleza HabariLEO hivi karibuni.

“Sisi tupo hapa kihalali lakini Mkuu wa Kituo na Meneja wake hawatutaki wakati tunalipa ushuru kila siku kabla yakuingia stendi na tunalipa gharama nyingine ikiwemo usafi wa choo,” alisema kijana kwa niaba ya wenzake ambao hawakutaka majina yao yaandikwe gazetini.

Huku wenzake wakimuunga mkono, alisema kuwa wakionekana kituoni hapo huswekwa rumande na kutoka kwa faini ya kuanzia Sh 20,000 hadi Sh 30,000 hivyo wanaiomba serikali kuingilia kati suala hilo.

Mkuu wa Kituo cha Polisi katika stendi hiyo, Cosmas Msigwa akijibu lawama hizo anasema mabasi yote yanayoanzia safari zake kituoni hapo yana mawakala watano watano kwa kila basi hivyo walalamikaji hao ni mawakala feki ama wasumbufu na wazururaji.

“Mwandishi hao si mawakala bali ni wazururaji kwa kuwa wamiliki wa mabasi wote wameajiri mawakala watano watano na wanapatikana ofisini kwao na si barabarani.

“Lakini hawa feki ndiyo wanaotoa sifa mbaya kwa abiria wa nchini na wale wa kimataifa na kituo hiki kuonekana kuwalea matapeli wakati heshima ya kituo hiki ni kubwa Afrika na kwa mujibu wa viwango vya ubora ni cha saba Afrika,” alisema Msigwa.

Kwa upande wake Ofisa Biashara wa kituo hicho, Geofrey Mbwama, anasema ili kuimarisha usalama wa abiria na mizigo kituoni hapo wameanzisha operesheni hiyo kuwasaka wapigadebe, matapeli na wazururaji katika kituo hicho na maeneo yaliyo karibu na kituo.

“Operesheni hiyo ni endelevu na tunaifanya usiku na mchana na kwa kiasi kikubwa imeanza kuzaa matunda na malalamiko ya watu kuibiwa yanapungua, kikubwa ni kutoa elimu ya kutosha kwa abiria wetu kwamba sehemu ya uhakika ni kufika ofisi husika au ofisi za mawakala wa mabasi katika maeneo na vituo kadhaa vinavyotambulika kuliko kuburuzwaburuzwa,” anasema Mbwama.

Mbwama alieleza lengo la operesheni hiyo ni kukipa kituo hicho heshima inayolingana nayo kuliko kuwa genge la wahuni, vibaka na wazururaji na kwamba wameanzisha vituo vinne vya kukamata ambapo askari wanafanya doria ya kutosha usiku na mchana.

Hadi makala haya yanaandikwa watu 25 wamekamatwa na wamechukuliwa hatua za kinidhamu, ikiwamo kupigwa faini na wengine kufunguliwa mashitaka kwenye Mahakama ya Jiji,” alisema Mbwama.

Mkurugenzi wa Habari Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustafa Mwalongo aliliambia HabariLEO kuwa operesheni hiyo imekuja wakati muafaka kutokana na matapeli wengi kuhujumu kampuni za usafirishaji kituoni hapo.

Taarifa ya Ofisa Habari wa Manispaa ya Ubungo, Joina Nzali inaeleza kuwa, tangu kuanzishwa kwa stendi hiyo kwa takribani miezi 11 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 imekusanya Sh bilioni 3.4, fedha zinazotumika kuimarisha miundombinu ya huduma kwenye stendi hiyo.

Nzali alisema manispaa hiyo imetumia Sh bilioni 1.1 kwa ajili ya kutoa mikopo ya wanawake, vijana na wenye ulemavu, mikopo isiyo na riba yenye lengo la kuinua maisha ya wananchi. Pia imetumia Sh bilioni moja kwa ajili ya usafi wa maeneo mbalimbali ya manispaa hiyo.

Aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya mwezi mmoja kwa wananchi kuhusiana na ulipaji ushuru, ada, tozo na kodi zinazotozwa na halmashauri hiyo, kampeni iliyoanza Mei hadi Juni mwaka huu.

Nzali alibainisha lengo la Halmashauri ya Ubungo la mwaka wa fedha wa 2021/22 unaoishia mwezi ujao ni kukusanya Sh bilioni 23 na tayari imekusanya Sh bilioni 18 huku akisisitiza kuwa maofisa kodi wa Ubungo wameongeza ubunifu katika kusimamia kodi na tozo nyingine ili kuhakikisha makusanyo yanapatikana kwa ufanisi, hususani kwenye kituo cha mabasi.

Alisema msisitizo wa kukusanya mapato katika Stendi ya Magufuli umefanikisha kupatikana kwa kiasi hicho cha fedha kinachotumiwa kuhudumia abiria na wananchi wanaopata huduma katika stendi hiyo na kuimarisha miundombinu kadhaa mfano ujenzi wa daraja linalounganisha stendi hiyo na Kituo cha Daladala cha Mbezi Mwisho.

“Kwa mwaka wa fedha wa 2022/23 kwa maana ya mwaka ujao wa fedha, Manispaa imejipanga kukusanya Sh bilioni 27 na ndiyo maana tumeanzisha kampeni hii ili kuwaelewesha wananchi umuhimu wa kulipa ada, kodi na tozo mbalimbali ambapo tunawafuata walipo na kisha kuwaelewesha faida za kulipa kodi na namna zinavyosaidia maendeleo yao,” alisema Nzali.

Akizungumzia kuhusiana na maendeleo yaliyotokana na kodi hiyo, Joina alibainisha kuwa Manispaa imejenga madarasa 100, vituo vya afya viwili na zahanati tatu kupitia mapato ya ndani na kuwataka wananchi kulipa kodi na tozo kwa kuwa ni fedha zinazosaidia maendeleo yao.

“Hakuna haja ya kuogopa kufika kwenye maeneo ya Manispaa ya kulipia kodi kama pale kituo cha mabasi cha Simu 2000, Stendi ya Magufuli na katika kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma ya kulipa kodi kwa urahisi manispaa itajenga ofisi katika eneo la Manzese na Goba ili kuwaepusha wananchi dhidi ya vishoka ambao wamekuwa wakiwalaghai wananchi kuwa malipo ya kodi ni bei kubwa,” anasema Nzali.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/b9b06c7c0e83ce37605d013364ae252f.jpeg

HAPA nchini Agosti 23 mwaka ...

foto
Mwandishi: Dunstan Mhilu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi