loader
Mambo ya kimila yawapeleka mbio wakazi wa Kiwawa

Mambo ya kimila yawapeleka mbio wakazi wa Kiwawa

WAKAZI wa Kijiji cha Kiwawa, Kata ya Imbasei wilayani Arumeru mkoani Arusha, wamekumbwa na taharuki baada ya watu kadhaa kujeruhiwa kwa kupigwa na mawe ambayo hayajulikani yanapotokea.

Aidha, vioo vya nyumba mbalimbali vimebomolewa na mawe hayo.

Taharuki hiyo iliyoanza juzi imewaibua viongozi wa mila wa kabila la Wameru maarufu kwa jina la Washiri kutafuta suluhu ya mambo hayo yanayodaiwa kuwa ya kimila.

Akizungumza na HabariLEO jana wilayani Arumeru mkoani Arusha, Katibu Tawala Wilaya ya Meru, James Nchembe alisema ni kweli mawe yameendelea kurushwa mara kwa mara bila kujua wapi yanapotokea.

"Serikali haiamini uchawi lakini tumejionea mawe yakirushwa bila kujua yanapotokea, haya mambo yanahitaji wazee wa mila wakae wajue wapi wanaanzia ila haya mawe hatujui yanapotokea," alisema.

Nchembe alisema wanachoomba viongozi wa dini na mila kulitatua tatizo hilo maana ni mambo ya ajabu.

Hata hivyo, jana viongozi wa kimila akiwemo Mshiri Mkuu wa Meru, Hezron Sumary walikuwa katika vikao ili kubaini tatizo hilo chanzo chake ni nini huku akisema atatoa tamko baadaye.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo alisema Jeshi la Polisi limeweka kambi katika eneo hilo ili kubaini tatizo ni nini.

"Hatujui shida ni nini lakini polisi tupo hapa kuangalia chanzo cha haya ni nini," alisema.

Wananchi hao waliiambia HabariLEO kuwa tangu juzi mawe yanayowapiga yanahisiwa kurushwa na mizimu.

HabariLEO ilibaini nyumba tatu zimevunjwa vioo na mawe hayo na nyingine zikiharibiwa mabati.

Wananchi wa eneo hilo walisema mawe hayo yameanza kurushwa wiki mbili zilizopita lakini walipuuza na juzi ndipo kasi ilipoongezeka.

Kutokana na kuzidi kurushwa kwa mawe hayo wananchi wamekuwa wakivaa vitu kichwani vya kujikinga na mawe hayo ikiwemo ndoo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kiwawa, Ernest Pallangyo alisema wameshachukua hatua za awali kubaini ukweli wa mawe hayo ikiwemo kuweka ulinzi usiku na mchana lakini bado hawajafanikiwa kumkamata mtu au kubaini yanapotokea mawe hayo.

Miongoni mwa watu waliojeruhiwa na mawe hayo ni baadhi ya waandishi wa habari wawili waliopigwa mawe kichwani na mwingine mkononi wakati walipokwenda eneo hilo kwa ajili ya mahojiano.

foto
Mwandishi: Veronica Mheta, Arusha

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi