loader
TPA kutumia bil 750/- kuboresha bandari, yavuna bil 889/- mizigo

TPA kutumia bil 750/- kuboresha bandari, yavuna bil 889/- mizigo

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari (TPA) imetenga Sh bilioni 100.1 fedha za nje kutoka Benki ya Dunia (WB) na Sh bilioni 650 kutoka vyanzo vya mapato vya ndani ya mamlaka kwa ajili ya kutekeleza miradi katika mwaka wa fedha 2022/2023.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alisema hayo jana bungeni Dodoma wakati akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Aliitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na kuongeza kina na kupanua lango la kuingilia meli na eneo la kugeuzia meli, kuboresha gati namba nane hadi 11 na gati namba 12-15 katika Bandari ya Dar es Salaam.

Alisema fedha hizo pia zitasaidia kufunga na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato na mifumo ya Tehama, kuimarisha miundombinu ya reli ndani ya bandari kwa ajili ya kusafirisha mizigo kwa njia ya reli na kuendelea kuboresha Bandari ya Tanga awamu ya pili inayohusisha ujenzi wa gati namba moja na namba mbili yenye jumla ya urefu wa mita 450.

“Pia kukamilisha mradi wa kupanua na kuchimba lango la kuingilia na eneo la kugeuzia meli katika Bandari ya Tanga, kuendelea na ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala na kuendelea na ujenzi wa barabara inayounganisha gati jipya katika Bandari ya Mtwara,” alisema Profesa Mbarawa.

Alisema fedha hizo pia zitatumika katika ununuzi wa mitambo na vifaa kwa bandari zote ili kuboresha uwezo wa kuhudumia mizigo, kuboresha Bandari za Mwanza Kusini, Mwanza Kaskazini, Bukoba na Kemondo kwa ajili ya kuongeza uwezo wake kuhudumia meli kubwa zaidi katika Ziwa Victoria na kuendelea na ukamilishaji wa miradi ya uboreshaji wa bandari katika Ziwa Tanganyika.

Profesa Mbarawa alisema katika kipindi cha Julai, mwaka jana hadi Aprili, mwaka huu, TPA ilihudumia shehena ya tani milioni 11.3 na kukusanya mapato ya Sh bilioni 888.9 ikilinganishwa na shehena ya tani milioni 10.01 iliyohudumiwa na kukusanya Sh bilioni 751.3 katika kipindi kama hicho mwaka 2020/21 sawa na ongezeko la mapato la asilimia 18.32.

Alisema jumla ya magari 162,340 yalipakuliwa katika Bandari ya Dar es Salaam ikilinganishwa na magari 119,854 yaliyopakuliwa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2020/21 sawa na ongezeko la asilimia 35.5.

Profesa Mbarawa alisema kati ya Julai, mwaka jana hadi Aprili, mwaka huu kitengo cha shehena mchanganyiko cha TPA kilihudumia makasha 137,416 ikilinganishwa na 78,573 yaliyohudumiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2020/21 sawa na ongezeko la asilimia 74.9.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/6ab2a8ba51435198ad78cf7b46a2f68c.jpg

MKURUNGENZI wa Kampuni ya Prosperity ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi