loader
CCM kuendeleza maridhiano kuimarisha umoja nchini

CCM kuendeleza maridhiano kuimarisha umoja nchini

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kitaendelea na majadiliano na maridhiano ili kuimarisha demokrasia na kuunganisha Watanzania.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka alisema jana kuwa, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya chama hicho imepongeza, kuridhia na kuunga mkono Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan kujadiliana na viongozi wa vyama vya siasa kwa lengo la kuimarisha demokrasia na maridhiano.

Shaka aliwaeleza waandishi wa habari kuwa, CCM itaendeleza majadiliano ili kujenga jamii yenye usawa, uhuru wa kujieleza na kushiriki shughuli za kisiasa kwa kuzingatia maadili na sheria za nchi.

"Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM iliyoketi jana (juzi) ilipokea kisha kujadili masuala mbalimbali ya kitaifa ikiwamo hatua zinazochukuliwa na Rais Samia katika kujenga maridhiano ya kisiasa."

"Hivyo, Kamati Kuu imempongeza na kumuunga mkono Rais Samia kwa hatua anazoendelea kuchukua kukutana na kufanya mazungumzo na makundi ya kijamii wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa katika kujenga amani, haki na maridhiano," alisema.

Shaka alisema Kamati Kuu ya CCM imetambua na kuridhia dhamira ya dhati ya Rais Samia kufanya maridhiano kwa kuzingatia uendelezaji urithi, tunu na msingi imara wa ujenzi wa taifa kuviwezesha vizazi vijavyo virithi taifa jema lililo imara.

Alisema CCM inatambua mazingira na mahitaji ya kisiasa yaliyopo ndani ya jamii, hivyo kufanikiwa kwa majadiliano kutawanufaisha wananchi katika kuimarisha misingi ya utawala bora na utoaji huduma za kijamii.

Alitoa rai kwa Watanzania waendelee kumuunga mkono Rais Samia kwa kuwa amekuwa kiongozi anayeongoza kuliunganisha taifa kwa umakini na ujasiri.

Alisema anachokifanya Rais Samia si jambo geni kwa kuwa miaka ya nyuma kulikuwa na maridhiano ya ndani na kwenye nchi nyingine.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/3f7a0fef889aad61346d6ce783551957.jpg

WIZARA ya Afya inaendelea na ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi