loader
Nape aonya wakandarasi mkongo wa taifa

Nape aonya wakandarasi mkongo wa taifa

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ameonya wakandarasi waliopewa kazi katika Mkongo wa Taifa kuwa atakayefanya vibaya atakuwa amejiondoa katika kupewa kazi na wizara na serikali.

Alitoa onyo hilo jana jijini Dodoma kwenye kikao kazi cha kutoa vyeti kwa wakandarasi wajenzi wa kilomita 4,442 za mkongo huo.

"Kama kuna kazi unaweza kucheza nayo basi cheza na kazi za wizara nyingine, lakini ukicheza na za wizara hii utakosa za wizara hii na za serikali nzima, inabidi maneno mengine magumu tuyaseme na kwenye hili itabidi niwe mkali kidogo," alisema na kuongeza:

"Kazi hii tunayoikamilisha Desemba, 2022 itatuambia nani twende naye ili tusipasuane vichwa mbele ya safari. Mimi siamini katika kumpiga mtu buti kabla ya kumwambia, tumeweka fedha ya umma kwenye hii miradi lazima ifanyike kwa ubora na kwa wakati."

Nape alisema fursa zipo kwa wakandarasi ila zitapimwa kwa kazi wanazopewa hivyo wakifanya kazi vizuri watafurahia kufanya kazi na serikali na wakifanya vibaya watajuta kufanya kazi na wizara hiyo.

 

Alisema kwa mwaka wa fedha 2022/2023 serikali inatarajia kujenga zaidi ya kilomita 1,600 na vituo vipya 15 vya Mkongo wa Taifa, lengo likiwa ni kufikia wilaya 81 na urefu wa kilomita 14,361 sawa na asilimia 95 ya lengo la kufikia kilomita 15,000 ifikapo mwaka 2025.

Alisema tangu kuanza kujengwa kwa mkongo huo mwaka 2009, ujenzi umefikia kilomita 8,319 na zaidi ya Sh bilioni 670 zimetumika na una vituo kwenye mikoa 25 Tanzania Bara na wilaya 43 kati ya 139 sawa na asilimia 30.9.

Nape alisema mwaka 2021/2022 zilitengwa Sh bilioni 170 kwa ajili ya kujenga kilomita 4,442 na kuongeza uwezo kutoka 200G kwenda 800G, huku jumla ya mikataba 22 ilisainiwa na ilihusisha kampuni nane, ambapo kati ya hizo sita ni za Watanzania huku kazi ikipangwa kukamilika Desemba, mwaka huu.

Alisema kwa sasa serikali ipo kwenye mchakato wa kuhamishia shughuli zote za mkongo huo kwenye Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Jim Yonazi alisema lengo la mkongo huo ni kufikia kilomita 15,000 ifikapo mwaka 2025 na uongoze Afrika Mashariki na Kati.

Mkurugenzi wa Tehama wa wizara hiyo, Mlembwa Mnako alisema mkongo huo umesaidia kupunguza gharama za kusafirisha mawasiliano kwa njia ndefu, ambapo awali walikuwa wakitumia satelaiti.

Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Peter Ulanga alisema shirika hilo litahakikisha linaifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kidijiti.

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/d809a1a160325471998b8ba37eb92516.jpg

WIZARA ya Afya inaendelea na ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi