loader
‘Benki ya Deutsche  haifadhili Eacop’

‘Benki ya Deutsche haifadhili Eacop’

WIZARA ya Nishati imesema Benki ya Deutsche inayodaiwa kujitoa kufadhili Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (Eacop) haipo kwenye orodha ya benki zinazotoa fedha kwenye mradi huo.

Kumekuwa na taarifa katika mitandao ya kijamii zikidai Benki ya Deutsche imesitisha mpango wa kutoa Dola za Marekani bilioni 3.5 kwa ajili ya mradi huo wa kujenga bomba la mafuta lenye urefu wa kilometa zaidi ya 1,400 kutoka Uganda hadi Tanzania.

Taarifa hiyo ilidai uamuzi wa benki hiyo kujitoa unatokana na wanaharakati wa mazingira kusema mradi huo utaondoa maelfu ya familia na kuleta changamoto kwenye hifadhi za asili jambo ambalo si kweli.

Mratibu wa mradi wa bomba hilo kutoka Wizara ya Nishati Tanzania, Kisamarwa Nyangau alisema benki hiyo inayotajwa haipo kwenye orodha ya benki zinazotoa fedha kwa ajili ya mradi huo.

Alisema tafiti mbalimbali zimefanyika na kuweka mikakati ya kuhakikisha mradi hauathiri mazingira na kwamba yeyote anayeupinga, apinge kwa kufanya tafiti sahihi na zinazojitosheleza.

“Mradi wa Eacop unaandamwa sana kwa sababu kwa sasa uko juu katika kutafuta fedha kwenye soko la dunia, wanaotoa fedha nao walifanya tafiti kujiridhisha kama mradi huu unaweza kukopesheka na wakaridhika,” alisema Nyangau.

Kwa mujibu wa mratibu huyo, kwa sasa duniani kote nishati inayotumika ni mafuta na hata wanaotumia nishati mbadala bado wanatumia mafuta.

Alisema nchi mbalimbali zimegundua rasilimali hiyo kwa miongo ya hivi karibuni na hivyo kufanya uzalishaji wake na hatimaye kujitegemea kwa mafuta.

Kutokana na hilo, Nyangau alisema zipo baadhi ya nchi zitakazokosa soko, hivyo ni lazima kuwapo kampeni mbalimbali kuukosoa kwa makusudi.

“Licha ya ugunduzi wa mafuta kuwa wa hivi karibuni kwa nchi nyingi, suala la nishati jadidifu bado halijaweza kujitosheleza ulimwenguni kote na ni teknolojia mpya kwa Afrika.”

“Tukiitegemea asilimia 100 tutajikuta tunakuwa wategemezi wa teknolojia hiyo na hivyo tutakosa nishati katika viwanda na uchumi kwa ujumla,” alisema.

Alisema ni vema kubaini kuwa suala si mazingira maana viwanda vyao hadi kesho vinazalisha magari na mitambo ya viwanda inayotumia mafuta ya dizeli na petroli.

“Kwa ufupi kuna tafiti mbalimbali zimefanyika na kuweka mikakati mbalimbali kuhakikisha Eacop haitaathiri mazingira ikiwamo kutumia umeme wa Tanesco NzegaTZ/UG, umeme utokanao na mionzi ya jua, kupunguza idadi ya visima kwenye hifadhi na mengineyo,” alisema.

Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki kutoka Kabaale – Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga, Tanzania una urefu wa kilomita 1443.

Kati ya hizo, kilomita 296 zipo Uganda na kilomita 1147 zipo Tanzania zikipita katika mikoa nane ya Tanzania Bara ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga na wilaya 24, kata 134 na vijiji zaidi ya 180.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/70a3cc779a324793964637da739bd45f.jpg

WIZARA ya Afya inaendelea na ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi