loader
Changamoto ya maji yadaiwa kupunguza warembo Katavi

Changamoto ya maji yadaiwa kupunguza warembo Katavi

BAADHI ya wanaume katika Kijiji cha Ikondamoyo Kata ya Uruila, Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, mkoani Katavi, wameomba mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa mradi wa maji Ikondamoyo kuharakisha mradi huo, ili kupunguza idadi ya wanawake wenye vipara kwa madai ya kukosa muda wa kusuka.

Wakizungumza na Daily News Digital kwa nyakati tofauti, Wanakijiji hao wamedai kuwa, kwa sasa wanapata changamoto ya kukosa warembo, kwani wanawake wengi kijijini hapo wananyoa vipara kwa kukosa muda wa kujiremba na badala yake muda mwingi huutumia kutafuta maji.

"Mradi huu ukikamilika utaondoa kelele zote kwa sababu maji yatakuwa karibu, lakini pia tutapata sasa wanawake warembo wasiokuwa na vipara eneo letu kwa sababu ya kufuata maji mbali, wanakosa hata muda wa kusuka," amedai Victori Mlela mkazi wa Kijiji cha Ikondamoyo.

Amedai kwa sasa wanatumia maji ya kisimani, ambayo si safi na salama na mara kadhaa yamewasababishia magonjwa ya kuhara.

"Kijijini kwetu tuna shida sana ya maji, tunaugua sana taifodi kwa ajili ya kunywa maji machafu, tunakunywa maji ya kisimani, na tunatumia kamba ya chandarua, ambazo huwa zinakatikia kwenye maji," amedai John Maganga.

Naye mwenyekiti wa Kijiji cha Ikondamoyo, Philipo Mswanya amesema amepokea kwa furaha mradi huo wa maji katika Kijiji chake, ambapo amesema kwa sasa wananchi hufuata maji umbali mrefu na hupokea kesi nyingi zinazohusu migogoro ya wanandoa kuchelewa kurudi nyumbani kwa ajili ya kufuata maji.

"Ilikuwa ni kama ndoto kulala kuamka tunaambiwa tumeingiziwa Sh milioni 450 kwa ajili ya mradi huo, wananchi pia wamefurahi ujio wa mradi huu, kukamilika huu mradi utakuwa umeondoa changamoto ya wananchi kuendelea kuchota maji visimani, maji ambayo si safi na salama," amesema. 

Kwa upande wake Mhandisi Mkuu Ruwasa Wilaya ya Mpanda, Elinathan Karagwe amesema walipokea kiasi cha Sh Milioni 450 fedha zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa ajili ya mapambano ya UVIKO-19 kwa ajili ujenzi wa mradi wa Kijiji cha Ikondamoyo Kata ya Uruila ulioanza Februari mwaka huu na unatarajia kukamilika ifikapo mwishoni mwa Juni mwaka huu.

"Mradi huu ukikamilika tunatarajia kuwahudumia zaidi ya wananchi 2500 na tutajenga vituo 6 vya maji, ambapo tutaweka katika shule ya msingi Ikondamoyo, katika Kituo cha Afya na maeneo mengine," amesema.

 

foto
Mwandishi: Swaum Katambo, katavi

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi