loader
Mambo yaiva Zoezi la Ushirikiano Imara 2022 Uganda

Mambo yaiva Zoezi la Ushirikiano Imara 2022 Uganda

JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limekabidhi bendera ya Taifa kwa kikundi maalum cha kushiriki  zoezi la kijeshi liitwalo Zoezi la Ushirikiano Imara 2022 nchini Uganda.

Zoezi hilo la kijeshi litakuwa la siku 14 kuanzia Mei 28 mwaka huu na linaandaliwa na nchi  wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, likishirikisha washiriki kutoka majeshi na vitengo mbalimbali vya nchi husika,  kwa nia ya kukabiliana na changamoto za kiusalama kwa pamoja.

Akikabidhi bendera hiyo leo Mei 24 katika kambi ya jeshi ya Kikosi cha Usafirishaji Mwanza, Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la nchi Kavu, Meja Jenerali, Anthony Sibuti, amesema washiriki watapimwa katika maeneo manne, ambayo ni operesheni za ulinzi wa amani, kukabiliana na maafa/majanga, kupambana na uharamia, pamoja na ugaidi.

"Washiriki kutoka Tanzania kwenye zoezi hili wanatoka JWTZ, Polisi, Magereza, Uhamiaji,  Zimamoto na Uokoaji, Wizara ya Mambo ya Nje, Ofisi ya Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu, na Kituo cha Kitaifa cha Kupambana na Ugaidi," amesema.

Amesistiza  kwamba lengo kuu la zoezi hilo ni kuzijengea uwezo nchi wanachama wa Jumuiya katika kukabiliana na changamoto za kiusalama kwa pamoja.

Zoezi hilo pia lina malengo ya kudumisha ushirikiano baina ya vyombo vya ulinzi na usalama na  wadau wengine muhimu katika operesheni za ulinzi wa amani.

"Nitoe rai kwenu mkadumishe ushirikiano miongoni mwenu wenyewe na baina yenu na washiriki wenzenu kutoka nchi zingine.

“Jifunzeni mambo mazuri kutoka kwa wenzenu na pia kutoa fursa ya wao kujifunza kutoka kwenu. Mdumishe nidhamu, uhodari na utendaji mzuri," amesema. 

 

foto
Mwandishi: Abela Msikula, Mwanza

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi