loader
Takribani tani 60,000 za makaa ya mawe kupelekwa Ulaya kupitia Bandari ya Mtwara

Takribani tani 60,000 za makaa ya mawe kupelekwa Ulaya kupitia Bandari ya Mtwara

MELI ya MV EGT Southern Cross inatarajia kusafirisha kiasi cha tani 59,960 za makaa ya mawe kupitia Bandari ya Mtwara kwenda Amsterdam nchini Uholanzi.

Inaelezwa kuwa shehena hiyo ni kubwa zaidi ya makaa ya mawe kusafirishwa kupitia Bandari ya Mtwara.

Akizungumza mjini hapa leo (Jumatatu) kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano, Nicodemus Mushi amesema usafirishaji wa shehena hiyo kubwa kwenda barani Ulaya ni hatua muhimu ya kulifikia soko kubwa la Bara la Ulaya baada ya bidhaa hiyo baada ya lile ya Asia.

Akifafanua zaidi Mushi alisema mara ya mwisho bandari hiyo kusafirisha shehena kubwa zaidi ilikuwa ni tani 59,815.

"Hii ndio mara ya kwanza kwa shehena kutoka Bandari ya Mtwara kwenda Bara la Ulaya moja kwa moja," alisema Kaimu Mkurugenzi huyo wa Masoko na Uhusiano wa TPA, Mushi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Brigedia Jenerali Marco Gaguti akizungumza alisema, Serikali ya Mkoa wa Mtwara inaridhishwa na utendaji wa TPA na Bandari ya Mtwara hasa katika kutafuta wateja.

Alisema uwekezaji wa Serikali mkoani Mtwara ni mkubwa, ikiwemo Ujenzi wa gati ambao umegharimu Shilingi Bilioni 157.8.

Aidha aliongeza kuwa Serikali imeiwezesha TPA kununua vitendea kazi na kuboresha mazingira ya kufanya kazi hivyo kuna kila sababu ya kuunga mkono jitihada hizi za TPA.

"...Ili kupata wateja zaidi na sasa mwelekeo uwe katika nchi jirani ya Comoro ambayo ina fursa kubwa ya kufanya biashara na Tanzania.

Kwa kushirikiana na Kampuni ya Ruvuma Coal tunaendelea kutafuta masoko zaidi ili kuufanya uwekezaji wa Serikali katika Bandari ya Mtwara kuwa na tija," alisema Brigedia Jenerali Gaguti.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi