loader
Hongera Samia kuwajali wastaafu

Hongera Samia kuwajali wastaafu

MEI Mosi, 2022 katika sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani, Rais Samia Suluhu Hassan kama walivyofanya baadhi ya marais wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), alionesha wazi ‘rangi kuu ya upendo’ kwa wafanyakazi na wastaafu.

Upendo wa Rais Samia ulionekana katika ahadi ya nyongeza ya mishahara na kwa kuzingatia kuwa ahadi ni deni, akatangaza nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa serikali kwa asilimia 23.3.

Tangazo la nyongeza ya mishahara lilikuja baada ya siku 14 tangu Rais alipowasisitiza wafanyakazi akisema, ‘Jambo letu lipo’, akimaanisha kuwa ahadi ya nyongeza ya mishahara aliyoitoa mwaka jana, ataitekeleza na kweli kaitekeleza.

Tunamshukuru na kumpongeza Rais kwani ameonesha upendo na uungwana kwa wafanyakazi nchini kwa kuzingatia ukweli kuwa, ahadi ni deni na kuamua kutimiza.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Profesa Jamal Katundu, alifichua upendo mwingine wa Rais Samia kwa Watanzania hususani wastaafu.

Profesa Jamal alimshukuru Rais kwa kuridhia maombi ya wadau wa sekta ya hifadhi ya jamii wanaojumuisha wawakilishi wa wafanyakazi (Tucta), Chama cha Waajiri (ATE) na serikali ya kupandisha kiwango cha kikokotoo kutoka asilimia 25 iliyolalamikiwa mwaka 2018 hadi asilimia 33.

Sisi tunampongeza Katibu Mkuu huyo kwa kumpongeza na kumshukuru Rais kutokana na uungwana na upendo wake kiasi cha kuridhia ombi hilo.

Tunasema Rais Samia amezidi kuonesha kuwa ni Rais wa watu anayesikiliza na kushughulikia vilio vya watu kwa wakati sahihi.

Aidha, tunaipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Katibu Mkuu Jamal kwa kuanza juhudi za kuuelimisha umma faida za kanuni hii mpya ambazo ni nyingi kwa Watanzania wanaojali kizazi cha sasa na kijacho na wasiotaka kujinufaisha wenyewe.

Hii ni kwa kuwa kanuni mpya inawanufaisha wastaafu kwa maisha bora endelevu yasiyo ya kula leo na kusahau kuwa kuna maisha baada ya kuchukua mkupuo wa pensheni.

Tunashukuru na kumpongeza Rais kwa kuwa kanuni mpya imeongeza kiwango cha mkupuo wa pensheni katika mifuko yote.

Kadhalika, pensheni za wastaafu watakaotumia kanuni hizi zitakuwa zikihuishwa mara kwa mara kwa kuzingatia mfumuko wa bei, hali ya maisha na uwezo wa mifuko ya pensheni.

Ndio maana tunaungana na wananchi na taasisi zote zinazompongeza Rais kwa kuwa tunajua dhahiri kuwa, huu ni upendo mkubwa kwa wastaafu kwani kanuni mpya inaongeza kiwango cha malipo ya mkupuo kutoka asilimia 25 iliyokataliwa mwaka 2018 hadi asilimia 33 kwa asilimia 81 ya wanachama wa mifuko.

Kwetu sisi, hii ni neema kubwa, japo ‘wenye lao’ wanaweza kujaribu kupinga kwa kuwa kwenye msafara wa mamba, kenge hawakosekani.

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi