loader
Ruzuku ya Samia  yashusha bei za  petroli, dizeli

Ruzuku ya Samia yashusha bei za petroli, dizeli

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli ikionesha kupungua kwa bei ya bidhaa hiyo kufuatia ruzuku iliyotolewa na serikali.

Katika taarifa yake petroli imepungua kwa Sh 154 hadi 198 kwa mikoa ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara huku dizeli ikipungua kwa Sh 127 hadi 144 na mafuta ya taa Sh 127 hivyo kufanya lita moja ya mafuta ya petroli kuuzwa Sh 2,994 kwa Mkoa wa Dar es Salaam, 2,985 kwa Mkoa wa Tanga na 2,979 kwa Mkoa wa Mtwara.

Bei ya dizeli pia imeshuka kutoka Sh 3,452 hadi 3,131 kwa Mkoa wa Dar es Salaam, Sh 3,162 kutoka 3,639 kwa Mkoa wa Tanga na Sh 3,165 kutoka 3,650 kwa Mkoa wa Mtwara.

Bei hizi zitaanza kutumika kuanzia leo. Taarifa hiyo imesema kwamba serikali imeweka ruzuku ya Sh 306 kwa lita moja ya petroli na Sh 320 kwa lita ya dizeli kwa Bandari ya Dar es Salaam.

Kwa Bandari ya Tanga ruzuku ni Sh 152 kwa lita ya petroli na Sh 476 kwa lita ya dizeli wakati Bandari ya Mtwara ni Sh 282 kwa lita ya petroli na Sh 486 kwa lita ya dizeli huku mafuta ya taa yakiwa hayajawekewa ruzuku.

Taarifa iliyosainiwa na Mkurugenzi wa EWURA, Modestus Lumato hata hivyo, imebainisha kuwa bei za mafuta katika soko la dunia zimeendelea kuongezeka zaidi kutokana pia na vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine iliyoanza mwishoni mwa mwezi Februari 2022.

Mwezi uliopita Rais Samia Suluhu Hassan alitoa ruzuku ya Sh bilioni 100 ili kukabili ongezeko la bei za mafuta na akasema nafuu hiyo ianze leo Juni Mosi.

Aidha, kutakuwepo na mabadiliko zaidi baada ya kuanza kwa bajeti ya mwaka 2022/23.

Katika taarifa hiyo, Lumato alieleza kuwa kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani mradi tu bei hizo zisivuke bei kikomo au kushuka chini ya bei iliyoruhusiwa.

Ewura inashauri wateja wanunue bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei nafuu zaidi.

Imeandikwa na Anastazia Anyimike, Dodoma na Anna Mwikola

foto
Mwandishi: Waandishi wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi