loader
Majaliwa aagiza Tamisemi  kasi ukusanyaji mapato

Majaliwa aagiza Tamisemi kasi ukusanyaji mapato

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Nchi-Tamisemi, Innocent Bashungwa na viongozi wengine wa wizara hiyo wahakikishe suala la ukusanyaji mapato kwenye mikoa, halmashauri na mamlaka za serikali za mitaa linapewa kipaumbele ili kuongeza mapato ya serikali.

Majaliwa alitoa agizo hilo jana alipokutana na Waziri wa Tamisemi, Naibu mawaziri, Katibu Mkuu, Naibu makatibu wakuu, wakurugenzi na wakuu wa taasisi za wizara hiyo kwenye kikao alichokiitisha jijini Dodoma.

“Ajenda ya ukusanyaji mapato iwe ya kudumu ili yaongezeke hadi kufikia shilingi trilioni 2 kutoka makadirio ya sasa mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo halmashauri zimekadiria kukusanya mapato ya ndani ya shilingi trilioni 1.01 ikilinganishwa na shilingi bilioni 863.85 zilizoidhinishwa kwa mwaka 2021/2022,” alisema na kuongeza: “Nimekuja kwenye ziara ya kawaida ya kiutendaji ili kuzungumza na viongozi wakuu wa wizara na wakuu wa idara.

"Ni lazima ujitambue wewe ni nani hapa kwenye wizara, unatakiwa kufanya nini, mpango kazi wako ukoje na je, ni wako peke yako ama unahitaji watu wengine ili uweze kuutekeleza.

”Majaliwa alisema Rais Samia Suluhu Hassan anataka kuona Watanzania wanafikiwa na huduma hivyo wajiulize kama huduma hizo zinafika kwa wananchi kwa wakati.

"Waziri Mkuu Majaliwa pia aliwapongeza viongozi na watendaji wa wizara kwa kuongeza hati safi kwenye taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) katika kipindi cha mwaka 2019/2020 na 2020/2021.

“Taarifa ya CAG kuhusu Hesabu za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa mwaka wa fedha 2020/2021 imebainisha halmashauri 178 sawa na asilimia 96 zimepata hati safi, halmashauri sita sawa na asilimia tatu zimepata hati zenye shaka na halmashauri moja sawa na asilimia moja imepata hati mbaya,” alisema Majaliwa.

Alisema matokeo ya ukaguzi wa hesabu za mwaka wa fedha 2020/2021 yanaonesha mwenendo mzuri wa aina ya hati za ukaguzi zilizotolewa ikilinganishwa na ukaguzi wa hesabu za mwaka wa fedha wa 2019/2020.

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi