loader
TAHARIRI: Tanzania yapaa biashara,  uwekezaji kimataifa

TAHARIRI: Tanzania yapaa biashara, uwekezaji kimataifa

KATIKA dhamira yake ya kutaka kuona wananchi wananufaika moja kwa moja na miradi inayotekelezwa na serikali, Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza ujenzi wa mradi wa bomba la gesi kutoka Tanzania hadi Uganda upitie katika makazi ya watu ili kurahisisha ufi kaji wa nishati hiyo katika maeneo ya vijijini.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba, maelekezo yanalenga kuona wananchi wakinufaika na gesi kama wanavyonufaika wakazi wa Dar es Salaam.

Kwamba bomba halitapita katika mtaro wa bomba la mafuta kutoka Uganda kuja Tanzania ambao sehemu kubwa haupiti kwenye makazi. Mramba anasema serikali ipo katika hatua za mwisho kuanza kusafirisha gesi mikoani, ikianza na Mkoa wa Dodoma ambako itajengwa bohari kubwa ya gesi itakayojazwa kwa kutumia malori.

Tunaunga mkono hatua hii kwani nishati inayotokana na gesi ya asili ni yenye gharama nafuu kwa matumizi ya kupikia nyumbani na kwenye taasisi pamoja na matumizi ya viwandani.

Licha ya kuboresha na kurahisisha maisha, matumizi zaidi ya gesi majumbani yatasaidia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa yanayochangia kuharibu misitu. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Tanzania’s Forest Reference Emission Level (FREL), Tanzania inapoteza takribani hekta 469,000.

Eneo hilo linalopotea linaelezwa kwamba ni karibu sawa na ukubwa wa Jiji la Dar es Salaam. Licha ya kupunguza gharama endapo mtaro wa bomba la mafuta ungetumika, lakini haingii akilini kama bomba hilo la gesi litapitishwa maporini mbali na gesi inakohitajika sana, yaani kwenye makazi ya watu.

Wahusika wanatakiwa kuhakikisha maeneo yote ambayo bomba hilo la gesi litapita hasa vijijini, gesi inasambazwa katika maeneo hayo kwa ajili ya matumizi ya wananchi pamoja na kuhakikisha maeneo ya huduma za jamii kama hospitali, vituo vya polisi, shule na mengineyo yanapata huduma hiyo muhimu.

Aidha, mamlaka hizo pia zinapaswa kuhakikisha miundombinu yote ya kufikisha gesi katika maeneo ya wananchi inajengwa ili kurahisisha usambazaji wake ikiwemo jijini Dar es Salaam ambako bado mkaa unatumika kwa wingi, kwani bila ya hivyo utekelezaji wake utakuwa mgumu.

Rai yetu kwa mamlaka zinazohusika ni kuzitaka kutekeleza kikamilifu agizo hilo la Rais ili wananchi wengi hasa waliopo vijijini waweze kunufaika na gesi hiyo na kuboresha maisha yao pamoja na maeneo waliyopo.

foto
Mwandishi: MHARIRI

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi