loader
Gesiya helium ipo nchini, kusaidia mengi ikiwemo afya ya binadamu

Gesiya helium ipo nchini, kusaidia mengi ikiwemo afya ya binadamu

GESI ya helium ni ya kipekee, baadhi ya matumizi yake hayana mbadala katika maisha ya binadamu.

Baadhi ya matumizi ya gesi hiyo ni pamoja na masuala ya afya ya binadamu hospitalini kwenye maabara, anga, vifaa vya elektroniki kwa uchache. Mwaka 2017 Tanzania ilipata taarifa za awali kuhusu uwepo wa gesi hiyo kwenye Bonde la Ziwa Rukwa huko Songwe.

Kaimu Amidi wa Shule Kuu ya Madini na Jiosayansi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Emmanuel Kazimoto anasema tangu taarifa hizo zitolewe chuo hicho kupitia iliyokuwa Idara ya Jiolojia na Idara ya Jiosayansi kushirikiana na Chuo Kikuu cha Oxford ilijikita kufanya tafiti kuhusu uwepo na asili ya gesi hiyo kwenye Bonde la Rukwa.

Anasema UDSM ilifanikiwa kutengeneza wataalamu wawili waliobobea katika rasilimali hiyo ya gesi ya helium ambao wapo kwenye hatua za mwisho za kumaliza shahada za uzamili.

Katika harakati hizo, imewezesha chuo hicho kupata kifaa maalumu cha kuchunguzia gesi asili ikiwemo helium kinachoitwa ‘Mini Ruedi’ ambacho ni cha kipekee na ni kati ya vifaa adimu kabisa katika eneo la Afrika Mashariki, Kati na Kusini. Uwepo wa kifaa hicho kunaifanya Tanzania kuwa na uzoefu mkubwa Afrika katika utafiti wa rasilimali ya gesi hiyo.

Hivi karibuni UDSM ilitia saini mkataba wa maridhiano na Kampuni ya Rocket Tanzania katika utafiti wa gesi ya helium kwa kuwa nayo imekuwa ikifanya utafiti huo kwa kutumia njia za kijiolojia, kijiokemia na kijiofizikia.

Akielezea ushirikiano wa chuo hicho na kampuni hiyo ya Rocket, Dk Kazimoto anasema kampuni hiyo ilianza kuwasiliana na iliyokuwa Idara ya Jiolojia UDSM mwaka 2019, yaliendelea hadi kufikia wakati huu ikiwa kama Idara ya Jiosayansi ya Shule Kuu.

“Hapa nchini, Kampuni ya Rocket Tanzania Limited inafanya utafiti wa gesi ya helium kwa kutumia njia za kijiolojia, kijiokemia na kijiofizikia. Njia ambazo utaalamu wake pia unapatikana katika Idara ya Jiosayansi ya Shule Kuu,” anasema.

Anasema kwa hali hiyo imekuwa na utaalamu unaoendana, lengo la pamoja na nia ya ushirikiano kati ya kampuni na Shule Kuu katika kuendeleza utafiti na uchunguzi wa gesi ya helium.

“Katika ushirikiano huu kampuni ya Rocket imekubali kuiwezesha Shule Kuu ya Madini na Jiosayansi kutumia vifaa vyake ama kutoa vifaa vya kitaalamu kwa shule katika kipindi chote cha mkataba,” anasema.

Anasema mradi wa kwanza ni muendelezo wa mradi wa utafiti wa gesi ya helium kwenye udongo, katika Bonde la Rukwa, mradi wa pili unahusu kutengeneza ramani ya kijiolojia katika bonde la Rukwa, hususani maeneo yanayodhaniwa kuwa na gesi ya helium.

Na mradi wa tatu ni wa utafiti wa gesi ya helium kwenye udongo katika eneo la bonde la Ziwa Nyasa na wa mwisho ni wa kutengeneza ramani za joto ardhi eneo la bonde la Rukwa.

Anasema katika juhudi za kujenga uwezo wa watumishi wa Shule Kuu, Kampuni ya Rocket imealika wataalamu kutoka Shule Kuu kujifunza katika kazi ya utafiti wa kijiofizikia kwa kutumia mitetemo.

“Hii itatoa uzoefu muhimu si tu katika utafiti wa gesi ya helium bali hata rasilimali nyingine kama mafuta ya asili,” anasema. Naye Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye anasema kuwa chuo hicho kwa upande wa utafiti kinatambua nafasi yake katika maendeleo ya jamii, hasa katika uzalishaji wa maarifa yanayosaidia kutatua changamoto mbalimbali.

Anasema Shule Kuu ya Madini na Jiosayansi ni mpya, ambayo inahudumia sekta muhimu kwa maendeleo ya nchi.

“Kwa kutambua hili, uongozi wa chuo unapenda kuwahakikishia uongozi wa Rocket Tanzania Ltd kwamba UDSM itatoa ushirikiano wa karibu pale wana chuo watakapokuwa wakitoa huduma katika utafiti wa gesi ya helium,” anasema Profesa Anangisye.

Tanzania ni nchi iliyobarikiwa kwa uwepo wa madini mbalimbali ikiwemo dhahabu, almasi, tanzanite, chuma, bati, nickel, copper na mengineyo. Pia kuna gesi aina mbalimbali, kama vile ethane, helium, ambayo hivi karibuni zimepatikana futi za ujazo bilioni 138 kwenye Ziwa Rukwa na zinaweza kuhudumia dunia kwa miaka 20.

Mhadhiri Msaidizi wa Idara ya Jiolojia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Ernest Mulaya aliwahi kusema kuwa kiasi hicho cha helium ni kikubwa na kama itawezekana kuzalisha kiasi hicho chote maana yake Tanzania ina uwezo wa kumsambazia kila mtu wa dunia hii ambao ni watu bilioni 7.8 kiasi cha mtungi wa futi za ujazo 18 ambazo ni zaidi ya lita 500 kila mmoja dunia nzima.

Alisema hazina iliyopo ya helium kwa sasa duniani, imepungua na mahitaji yake duniani kwa sasa ni mengi kuzidi upatikanaji wake hivyo kusababisha bei yake kupanda maradufu siku hadi siku. Kwa maelezo yake nchini Tanzania kwa mara ya kwanza helium ilivumbuliwa kabla ya uhuru katika miaka ya 1950 na Taasisi ya utafiti jiolojia ya Tanganyika hasa maeneo ya ziwa Balangida, Ziwa Manyara na eneo la Majimoto na Mananka mkoani Mara. Baadae miaka ya 1960 katika maeneo ya Rukwa.

Uvumbuzi wa hivi karibuni uliofanyika miaka ya 2013 hadi 2015 uliofanywa na Chuo Kikuu cha Durham na Oxford vya nchini Uingereza ni mwendelezo wa uvumbuzi uliofanyika zamani.

“Ushauri wangu kwa serikali kuwa na mfumo mzuri wa sera na mwongozo mahususi kwa ajili ya gesi hiyo adimu mwanzoni kabisa kabla ya kuingia katika makubaliano yoyote na kampuni ya kigeni.”

Vilevile anasema ni muhimu kuwekeza katika tafiti za helium ili sera na mwongozo viendane na tafiti za kisayansi.

“Kwa mfano, tafiti za mwanzo za gesi hii ninazofanya zinaonesha kwamba kuna uwezekano wa gesi hii kuwa peke yake chini ya miamba ya eneo la Rukwa tofauti na sehemu nyingine duniani kama vile Qatar, Marekani, Algeria na kwingineko ambako gesi hii huzalishwa kama taka ya gesi asilia na mafuta kutoka ardhini,” anasema.

Matumizi mengine ya gesi hiyo ni kutengeneza vitu vya kuzalisha baridi, kutengeneza vifaa vya hospitali vya sumaku ikiwemo mashine ya kupima mwili ya MRI, nyaya za televisheni na intaneti zenye kasi kubwa, chip za kompyuta na simu, hadubini na pia hutumika kwenye ndege.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/69fddcf211becfdc465073a9c3b1e4c9.jpg

HAPA nchini Agosti 23 mwaka ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi