loader
Afya Kamilifu na mapambano  kufikia 95-95-95 Mara

Afya Kamilifu na mapambano kufikia 95-95-95 Mara

HADI sasa takribani asilimia 90 ya wanaume mkoani Mara wamefi kiwa na huduma za tohara kupitia mradi wa Afya Kamilifu.

Ni mradi wa miaka mitano kuanzia 2018, wenye lengo la kuzuia maambukizo mapya ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na hivyo kufikia lengo la 95-95- 95 (Tisini na tano tatu) kwa wakati.

Unatekelezwa na Shirika la kimataifa Amref–Tanzania kwa udhamini wa Serikali ya Marekani kupitia Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC).

Wanufaika wengine wa mradi huo ni Tanga, Simiyu na Zanzibar (Unguja na Pemba), ambako umekua ukitekelezwa kwa miaka mitatu ya mwanzo na miwili ya mwisho unatekelezwa Mara, kuanzia Oktoba mwaka jana. Kwa ujumla wake (Tanga, Simiyu, Mara na Zanzibar), mradi unatarajia kunufaisha watu 166,767, ifikapo Septemba 2023.

Umezinduliwa rasmi Mei 23 mwaka huu wilayani Musoma, huku Mkurugenzi Mkaazi wa CDC, Dk Eva Matiko akisisitiza kwamba lengo kuu ni kudhibiti maambukizo mapya ya VVU na hatimaye kufikia lengo la 95 tatu ifikapo 2025.

Anafafanua kwamba 95 tatu maana yake ni asilimia 95 ya wanaoishi na VVU (WAVIU) wawe wamepima na kujua hali ya afya zao, asilimia 95 wawe wameanza kutumia dawa za kufubaza virusi (ARVs) na asilimia 95 ya wanaotumia dawa wawe wameshafubaza virusi mwaka 2025.

Tohara kwa wanaume inapewa kipaumbele katika mradi huo hasa baada ya tafiti kuonesha kwamba inazuia maambukizi ya VVU kwa zaidi ya asilimia 60 kwa mujibu wa watafiti.

“Vilevile CDC imekubaliana na maombi ya mkoa ya kuongeza wigo wa huduma ya tohara kwa wanaume katika halmashauri za Rorya, Tarime TC na Serengeti DC ambazo hazikuwa sehemu ya mradi ili kufikia mkoa mzima,” anasema Dk Matiko.

Sambamba na hilo, CDC kupitia mradi huo inashirikiana na uongozi wa mkoa na halmashauri kutoa chanjo ya Covid-19 kwa Watu Wanaoishi na Virus vya Ukimwi (WAVIU), watoa huduma za afya na jamii kwa ujumla.

Kufikia sasa, asilimia 92 ya WAVIU, asilimia 86 ya watoa huduma za afya na asilimia 14.3 ya wananchi wenye umri zaidi ya miaka 18 na wenye vigezo wamekamilisha chanjo mkoani Mara. Anasema CDC inathamini mafanikio ya huduma za matibabu ya VVU zinazonufaisha WAVIU 54,719 mpaka sasa mkoani Mara, ambalo ni ongezeko la asilimia 4.9 tangu Oktoba 2021.

Anasisitiza kwamba mradi mkoani Mara umeonesha mafanikio mazuri na unatarajia kuimarisha rasilimali watu, ambapo tayari watoa huduma za afya wapatao 568 wamewezeshwa na mradi na wanafanya kazi kwa karibu zaidi na watumishi wa serikali ili kutoa huduma za viwango kwa WAVIU kuanzia ngazi ya vituo vya afya hadi jamii.

Hata hivyo, bado kuna uhitaji mkubwa wa watumishi katika vituo vipya vya huduma na matunzo vilivyoanzishwa ndani ya mkoa, anasema na kuongeza kwamba kunahitajika pia kipaumbele kwa Kamati za Afya za Halmashauri (CHMT) kusimamia huduma.

Mkurugenzi wa Mradi, Dk Edwin Kilimba anasema huduma za tohara kwa wilaya za Rorya, Tarime na Serengeti zinaanza mwezi huu (Juni) ili kuhakikisha mkoa wote umefikiwa.

Anasema kutokana na kwamba tayari asilimia kubwa ya wanaume imehudumiwa tangu kuanzishwa kwa Afya Kamilifu mkoani humo, lengo la kila mwaka la mradi litafikiwa kabla ya mwaka wa kwanza kuisha (Oktoba mwaka huu).

Kupitia mradi huo, wanaume wanapata huduma katika vituo vya afya na katika magari yanayozunguka maeneo mbalimbali ya mkoa ili kurahisisha tohara, lakini pia kupunguza mlundikano wa wahitaji katika hospitali.

“Tunajivunia mwamko wa wanaume. Tohara ni mojawapo ya silaha muhimu katika kuzuia maambukizo mapya ya VVU,” anasema Dk Kilimba.

Dk Kilimba anasema mbali na tohara, upimaji afya, utoaji wa ARV na kufuatilia WAVIU ili kutambua kama virusi vinafubaa au la ni huduma pia zinazotolewa katika mradi huo. Anasema vipimo vya mtu kujipima mwenyewe pia vinapatikana katika vituo vyote vya afya, ambapo kila mhitaji anapatiwa akajipime kwa wakati wake.

Anachosisitiza Mkurugenzi ni wapimaji kurudisha majibu kwa watoa huduma ili wanaojikuta na maambukizo wafanyiwe uhakiki zaidi wa vipimo na anayethibitika kuambukizwa aanze dawa za kufubaza virusi mara moja. “Tunawapatia elimu kwanza ya matumizi ya vipimo hivyo.

Upimaji ni hatua muhimu katika kuzuia maambukizo mapya ya VVU, hivyo kurahisisha kutimia kwa lengo la 95 tatu,” anasema.

Mkuu wa Wilaya Rorya (DC), Juma Chikoka, anasema tohara kwa wanaume ni mojawapo ya maeneo yanayopewa kipaumbele kupitia Afya Kamilifu kwani maambukizo yako juu katika wilaya hiyo kwa asilimia sita ikilinganishwa na wilaya zingine za Mkoa wa Mara.

“Tumeshaanza elimu kwa umma kueleza umuhimu wa tohara kwa wanaume. Tunashukuru mwitikio ni mkubwa,” anasema. Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk Halfany Haule, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa Mara, anawashauri wanaume wa Rorya kuifanya tohara kuwa sehemu ya tamaduni zao kama ilivyo Musoma ambako wanaume hutafuta huduma hiyo wenyewe.

“Mwamko huo wa wanaume wa Musoma umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza maambukizo (wilayani) hadi kufikia asilimia tatu za sasa,” anasema Dk Haule.

Akizungumzia Afya Kamilifu, anasema sambamba na tohara kwa wanaume, upatikanaji wa ARV unatiliwa mkazo zaidi, akawashauri wananchi mkoani humo kujitokeza kupima afya zao ili wanaobainika kuwa na maambukizi waanze dawa mapema.

“Mara bila Ukimwi inawezekana kwani kwa sasa hali ya maambukizi kimkoa ni asilimia 3.6. Tunaamini kupitia mradi huu ambao umekuja kuunga mkono jitihada za muda mrefu za serikali, maambukizi yanaweza kuwa sifuri,” anasema.

Kuhusu tohara, Dk Haule anashauri wanaume wasifanye zoezi hilo kienyeji bali watumie wataalamu wa afya kwa uhakika wa huduma bora. Utafiti wa Athari za VVU Tanzania (THIS) 2016-2017, unasema asilimia 49.7 ya wanaume wa umri wa kuanzia miaka 15 nchini ndio waliopatiwa huduma za kitabibu na asilimia 27.9 wamepatiwa huduma kienyeji.

THIS inaonesha pia kwamba asilimia ya wanaume wasiotahiriwa ni 34.4 kwa wale wenye umri kati ya miaka 75 hadi 79 na asilimia 15.1 kwa vijana wenye umri wa miaka kati ya 20 hadi 24.

Miongoni mwa waliopima VVU wakati wa utafiti, asilimia 42.5 walionekana kufanyiwa tohara ya kitabibu na asilimia 38.0 kutofanyiwa tohara kabisa.

“Kwa wale waliokutwa bila maambukizo ya VVU, asilimia 20.2 walionekana kutofanyiwa tohara aina yoyote na asilimia 49.3 kufanyiwa tohara ya kitabibu,” inasema tafiti hiyo.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/554c21ad1f0a0c75f3e59bcb53e10fda.jpg

HAPA nchini Agosti 23 mwaka ...

foto
Mwandishi: ABELA MSIKULA

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi