loader
Bandari ya Dar es Salaam ‘inavyopelekwa’ Mwanza

Bandari ya Dar es Salaam ‘inavyopelekwa’ Mwanza

JUNI 14, mwaka jana ikiwa ni miezi michache tangu ashike madaraka ya kuongoza nchi, Rais Samia Suluhu Hassan alisema serikali yake itahakikisha inaipeleka Bandari ya Dar es Salaam ambayo ndio kubwa kuliko zote nchini jijini Mwanza.

Amesema hayo wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha tano cha kutoka Fela wilayani Misungwi, Mkoa wa Mwanza kwenda Isaka, Shinyanga.

 “Ndugu zangu wa Mwanza, tunataka kuileta Bandari ya Dar es Salaam hapa Mwanza maana kukamilika kwa kipande cha tano cha SGR pamoja na vipande vingine vinne ambavyo tunaendelea na mipango ya ujenzi, kutaisogeza karibu Bandari ya Dar es Salaam ndani ya Jiji la Mwanza.”

Hafla hiyo ya uwekaji wa jiwe la msingi iliandaliwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC), ambapo Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) nayo ilishiriki kwa kudhamini tukio hilo.

Siku hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Eric Hamissi alisema kwamba popote duniani, ufanisi katika biashara ya bandari kwa kiasi kikubwa hutegemea uwapo wa mtandao imara wa miundombinu ya usafirishaji hasa reli.

“Ni kwa kutambua hali hii, Mamlaka ya Bandari Tanzania imejielekeza kufanya kazi kwa karibu na taasisi za serikali ili kuboresha miundombinu ya Reli ya Kati na Tazara (Reli ya Tanzania na Zambia) na tayari TPA ina hati za makubaliano (MoU) na taasisi hizo,” anasema Mkurugenzi Mkuu huyo.

Hamissi anaongeza kuwa, TPA inaendelea kuimarisha matumizi ya Bandari Kavu ya Isaka kufuatia punguzo la bei ya usafirishaji lililofanywa na TRC ili kuhimili ushindani wa Bandari Kavu ya Naivasha ya nchini Kenya na pia kujipanga na ujio wa Reli ya Kisasa (SGR).

Ni katika muktadha huo, wakati akiwasilisha bungeni mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2022/23 hivi karibuni, Waziri wa Wizara hiyo, Profesa Makame Mbarawa anaeleza namna serikali inavyoendelea kutekeleza mradi wa reli ya kisasa.

“Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea na kazi za ujenzi wa reli ya SGR kwa awamu mbili, ambapo imeendelea na ujenzi wa awamu ya kwanza iliyogawanyika katika vipande vitano kati ya Dar es Salaam na Mwanza (kilometa 1,219). Utekelezaji wa ujenzi wa vipande hivyo umefikia katika hatua mbalimbali za utekelezaji,” anasema.

Vipande viwili vya awali katika ujenzi wa mradi huo ni Dar es Salaam hadi Morogoro (kilometa 300) na Morogoro hadi Makutupora (kilometa 422).

Mbarwa anasema serikali imeanza utekelezaji wa ujenzi wa reli ya SGR katika awamu ya pili kati ya Tabora na Kigoma ambapo fedha za utekelezaji huo zimeanza kutengwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Kuhusu maendeleo ya reli hiyo, Profesa Mbarawa anasema: “Mheshimiwa Spika, ninapenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa wizara imeendelea kusimamia ujenzi wa vipande hivyo vya reli na hadi kufikia Aprili, 2022 kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro kimefikia asilimia 96.54 na tayari majaribio ya kuingiza umeme wa kuendeshea treni kwenye mfumo (Power system energization) yamekwishaanza.”

Kuhusu kipande cha pili cha reli kutoka Morogoro hadi Makutupora (kilometa 422),  anasema kazi ya ujenzi imekamilika kwa asilimia 85.02 na inatarajiwa kukamilika kwa asilimia 100 Februari, 2023.

Mbarawa anasema serikali imeendelea na ujenzi wa kipande cha reli cha Mwanza - Isaka chenye urefu wa kilometa 341 (kilometa 249 za njia kuu na kilomita 92 njia za kupishania treni) unaofanywa na mkandarasi wa ubia wa kampuni za China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) na China Railway Construction Corporation Limited (CRCC) za nchini China.

Anasema thamani ya mkataba wa ujenzi huo ni Dola za Marekani bilioni 1.326 sawa na Sh trilioni 3.062 ikijumuisha na kodi.

Anasema ujenzi wa kipande hicho hadi Aprili, 2022 ulikuwa umefikia asilimia 6.8 na kwamba kazi kubwa inayoendelea ni ya usanifu na ujenzi wa tuta.

Kwa mujibu wa Mbarawa, kazi nyingine zinazoendelea katika kipande cha Mwanza – Isaka ni pamoja na utwaaji wa ardhi ambapo hadi Aprili, mwaka huu jumla ya kilomita 134 kati ya 249 zilikuwa zimekwishatwaliwa na kukabidhiwa kwa mkandarasi kwa ajili ya ujenzi.

Anasema usanifu wa awali wa njia ya reli umekamilika kwa asilimia 100; usanifu wa kina umefikia asilimia 93; utafiti wa udongo na mifumo ya maji (Geotechnical and hydrological study) umefikia asilimia 65.82 na kwamba ufungaji wa mitambo ya kokoto, zege na kiwanda cha mataruma umekamilika.

Anasema ujenzi wa kambi ya Fela umefikia asilimia 93.4, Bukwimba asilimia 93.33, Seke asilimia 100, Malampaka asilimia 98.94 na Luhumbo asilimia 66.29.

Sambamba na hayo, Profesa Mbarawa anasema ujenzi wa tuta umeshaanza na umefikia asilimia 13.7.

Kuhusu kipande cha Makutupora hadi Tabora chenye urefu wa kilometa 368 (kilometa 294 njia kuu na kilometa 74 njia za kupishania), Profesa Mbarawa anasema mkataba wa ujenzi wa kipande hicho ulisainiwa tarehe 28 Desemba, 2021 kati ya TRC na mkandarasi ambaye ni Kampuni ya Yapi Merkezi kutoka Uturuki na kwamba maandalizi ya ujenzi yanaendelea.

Kwa upande wa ujenzi wa kipande kilichobaki katika awamu ya kwanza cha Tabora – Isaka (kilometa 165), Waziri huyo anasema serikali ipo katika hatua za mwisho za ununuzi wa mkandarasi.

Anasema serikali imeanza maandalizi ya ujenzi wa awamu ya pili ya Reli ya Kisasa,  ambapo ujenzi wa kipande cha Tabora – Kigoma (kilometa 411) upo katika hatua za manunuzi ya mkandarasi.

Aidha, anasema Serikali ya Tanzania na Burundi zimesaini makubaliano ya kuanza ujenzi na kutafuta fedha kwa ajili ya njia ya reli ya Uvinza-Musongati-Gitega (kilometa 282).

Vilevile anasema Serikali ya Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zilishatangaza zabuni ya kufanya upembuzi yakinifu ya reli ya kisasa kutoka Gitega mpaka Kindu (DRC).

Kimsingi, ujenzi wa reli ya kisasa pamoja na maboresho makubwa ambayo yamefanyika katika Bandari ya Dar es Salaam, vinatazamiwa kuongeza uwezo wa sasa wa bandari hiyo kuhudumia shehena kubwa zaidi kutoka wastani wa tani milioni 16 hadi kufikia tani milioni 25.

Faida nyingine ni kupunguza umbali na gharama za kusafirisha shehena.

Imekuwa ikielezwa kwamba, katika hali ya sasakuna  wafanyabiashara kadhaa wa mikoa ya Kanda ya Ziwa na mikoa ya Kaskazini ya Kilimanjaro, Mara na Arusha wanaopitisha shehena katika Bandari ya Mombasa iliyoko nchi jirani ya Kenya.

Ufanisi mdogo wa reli ya kati (meter gauge) umekuwa pia ukichangia shehena kwenda nchi zingine za Maziwa Makuu ikiwemo Uganda kutokuwa kubwa licha ya kukamilika kwa reli katika mji wa Port Bell hadi Kampala nchini Uganda.

Reli hiyo ya Port Bell- Kampala ilikuwa inachangia sana shehena ya nchi hiyo kupitia Tanzania kuwa ndogo na licha ya kuongezeka baada ya kukarabitiwa, kukamilika kwa SGR kunatarajia kuongeza maradufu shehena ya Uganda inayopita Tanzania.

Hakuna shaka kwamba kukamilika kwa ujenzi wa SGR kutaongeza mapato katika Bandari ya Dar es Salaam yanayopotea kwa sasa kutokana na shehena inayopitishwa nchi jirani.

Na kimsingi, kukamilika kwa reli hiyo ya kisasa kwenda Mwanza na tawi lake la Kigoma, si tu kwamba Bandari ya Dar es Salaam itakuwa umesogezwa Mwanza pekee, bali pia Kigoma na nchi za Burundi na DRC.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/255ba5df84a0bb8068602546d27dbf64.jpg

HAPA nchini Agosti 23 mwaka ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi