loader
Yanga kutangaza ubingwa leo?

Yanga kutangaza ubingwa leo?

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga leo wanashuka uwanjani kuikabili Coastal Union ya Tanga kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Mchezo huo unaweza kuwa kama fainali kwa Yanga ambao wanahitaji pointi tatu tu kutangazwa mabingwa msimu huu, lakini pia Coastal Union wanahitaji kushinda kupanda nafasi za juu na kupata nafasi ya uwakilishi wa kimataifa msimu ujao.

Yanga licha ya ubora walionao wakiwa hawajapoteza mchezo wowote ya ligi hiyo, katika michezo mitano iliyopita walionekana kuyumba kidogo baada ya kupata sare tatu na kushinda michezo miwili.

Kwa upande wa Coastal Union ambao walikuwa nafasi za chini, wanaonekana kuimarika na kurejea kwenye kasi baada ya michezo mitano iliyopita kupata matokeo mazuri yaliyowapandisha kwenye msimamo.

Coastal imeshinda michezo minne iliyopita kati ya mitano na kupata sare moja ikionesha wazi ‘gari limewaka.’ Timu hizo zilikutana mara ya mwisho katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo, ambapo Yanga ikiwa ugenini kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga ilishinda mabao 2-0.

Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi alisema jana kuwa, mchezo huo hautakuwa rahisi kwani wanatarajia kukutana mara tatu kwani baada ya leo watacheza tena mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (FA).

“Wachezaji wangu wanajua umuhimu wa mchezo huu, nimeongea nao namna tunavyotakiwa kuwaheshimu wapinzani, lakini pia kupambana na kushinda, nimefurahi kuona namna walivyo na morali,” alisema.

Nabi alisema mchezo huo utawakosa nyota watatu wa timu hiyo, Bakari Mwamnyeto (majeruhi), Kibwana Shomari anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano na kipa Djigui Diarra ambaye amechelewa kurudi kutoka katika majukumu ya timu yake ya taifa ya Mali.

Kocha Msaidizi wa Coastal Union, Joseph Lazaro alisema: “Mechi yetu tunataka kuanzia pale tulipoishia, kuweka historia kuifunga timu ambayo haijafungwa.” “Tunawaheshimu tunaocheza nao kutokana na ubora, lakini tumekuja kupambana na Yanga ili kuwa sehemu salama kwasababu tulipo sio salama,” alisema.

foto
Mwandishi: Na Grace Mkojera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi