loader
MBEYA CITY YAITISHA SIMBA

MBEYA CITY YAITISHA SIMBA

KOCHA Mkuu wa Mbeya City, Mathias Lule amesema wamepo Dar es Salaam kwa lengo moja tu, kuhakikisha wanapata ushindi dhidi ya Simba katika mchezo utakaopigwa kesho katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha huyo alisema waliwasili Dar es Salaam takriban siku tatu kabla ya mechi ili kuhakikisha wanazoea hali ya hewa kwa ajili ya mchezo huo.

“Tumejiandaa vizuri na vya kutosha ndiyo maana leo (jana) tuna siku ya pili tunafanya mazoezi hapa Dar es Salaam ili kuzoea mazingira ili tupate ushindi, mechi mbili zilizopita tulipoteza na hatuko hapa kwa ajili ya kuendelea kupoteza, hii ni mechi nyingine na tunahitaji matokeo mengine,” alisema Lule.

City itaingia katika mechi hiyo ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba kwenye mechi ya mzunguko wa awali.

Naye Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola alisema wanatambua ugumu wa mechi hiyo na nyingine zilizobakia, ambapo wanahitaji kushinda mechi zote tano ili kuweka heshima na kuwapa furaha mashabiki wao.

“Hatuna nafasi kubwa ya kutetea ubingwa, lakini tunataka kuweka heshima kwa kushinda mechi tano zilizobaki ikiwamo dhidi ya Mbeya City, ingawa tunajua ni mechi ngumu ila lengo letu ni kuwapa furaha mashabiki wetu hivyo maandalizi yetu ni mazuri na nina imani tutaibuka na ushindi dhidi yao,” alisema.

foto
Mwandishi: Na Hans Mloli

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi