loader
Ziara ya Chongolo Shinyanga,,  Simiyu yakata kiu wanachama

Ziara ya Chongolo Shinyanga,, Simiyu yakata kiu wanachama

KUNA usemi usemao mgeni njoo mwenyeji apone. Ndivyo ilivyokuwa kwa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mikoa ya Shinyanga na Simiyu ambapo ziara ya siku tisa ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Daniel Chongolo ilijibu kiu ya wanachama wengi.

Kiu hiyo ni pamoja na kujibu madukuduku yao kuhusu mwongozo na kugombea nafasi mbalimbali za chama kuanzia ngazi ya shina hadi taifa na mambo mengine yaliyoleta sintofahamu na kuwafanya baadhi wabaki njia panda.

Chongolo amefanya ziara hiyo mwishoni mwa Mei hadi wiki ya kwanza ya Juni mwaka huu, ikiwa na malengo matatu, kusalimia na kuwashukuru wananchi na wanachama kwa kuchagua CCM uchaguzi wa 2020 uliopita, kukagua uhai wa chama ngazi ya mashina na kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM katika miradi ya maendeleo nchini.

Katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani Shinyanga, Chongolo alikutana na wanachama na akatumia nafasi hiyo kuwashukuru kwa jinsi wanavyojitoa kitumikia chama na hakusita kuwataka wajitokeze kuwania nafasi za uongozi ndani ya chama.

Katika hilo, Chongolo anaweka msimamo wa chama kwa kupiga marufuku wagombea nafasi za uongozi ndani ya chama hicho nchi nzima ambao ni viongozi kutohusika katika mchakato wa kutoa fomu au kusimamia uchaguzi.

Badala yake akatoa mwongozo kuwa chama kiteue mtu mwingine wa kuusimamia ili kuweka mazingira ya haki na usawa kwenye uchaguzi.

Hatua hiyo ikaibua shangwe kwa wanachama ambao baadhi yao wamesema ni kweli baadhi ya maeneo wapo wagombea walionyimwa fomu na wengine wakiambiwa zimekwisha.

“Mwaka huu ni wa uchaguzi, fomu zitolewe kwa wagombea wote na pale ambapo Katibu wa kata au kiongozi yoyote ndani ya chama anawania nafasi ni marufuku kuhusika kwenye mchakato wa uchaguzi, wabaki kuwa wagombea ili haki itendeke na hii ni kwa nchi nzima,” anabainisha Chongolo.

Marufuku hiyo imetokana na ukweli kuwa iwapo chama kitaruhusu hali hiyo upo uwezekano wa baadhi ya viongozi kushiriki kupanga safu zao na kuwanyima nafasi wagombea wengine wenye uwezo na sifa za kuwania nafasi hizo. Ndio maana Chongolo anasisitiza:

“Chama kina katiba na taratibu na ndivyo vitakavyotumika wakati wa uchaguzi. Kuna mchezo huwa unafanywa na baadhi ya wagombea ambao ni viongozi wa kuwanyima fomu wagombea wengine kwa makusudi tu, wengine wanapanga safu, sasa hatuwezi kufanya hivyo, unataka uchaguzi uwe huru na haki kila mwenye nia awanie na tuchague wenye sifa na uwezo ili tukisaidie chama na wananchi.”

Hatua nyingine aliyofanya Chongolo kuhusu kuwania fursa ndani ya chama hicho ni pale alipotoa mwongozo kwa wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) ambao ni wanachama wa CCM na wanagombea nafasi ya ubalozi wa shina.

Chongolo anasema wagombea wa nafasi hizo ambao wana sifa za kunufaika na Tasaf hawapaswi kuondolewa kwenye unufaika wao kwa sababu nafasi wanazowaniwa si za anasa na kusisitiza kuwa viongozi masikini wenye uwezo wa kuongoza wana haki ya kuwania nafasi ngazi hiyo.

Baada ya kutoa mwongozo huo wanachama hao walipiga vigelegele vya shangwe na baadhi yao wakasema walishatishwa kuondolewa kwenye mfuko huo iwapo watashiriki kuwania nafasi hizo.

Ni wazi kuwa Chongolo anakata kiu ya maswali mengi ya wanachama ngazi ya shina ambao kwa njia moja au nyingine wamekuwa na changamoto zinazokosa majibu pindi wanapotaka kuwania nafasi za uongozi kwa ngazi walizopo.

Masanja Bundala ni Mwenyekiti wa CCM Shina namba 6, wilayani Ushetu alishukuru hatua zinazochukuliwa na chama kutembelea mashina ya chama hicho na kusema huko ndiko kwenye wanachama.

“CCM inajengwa na wanachama kuanzia ngazi ya mashina, ziara hii ni faraja kwetu, inaonesha uhai wa chama na thamani yetu kwake,” anasema Bundala. Pamoja na kuzungumza mengi kuhusu chama na kukemea vitendo viovu vinavyofanywa na baadhi ya viongozi kuwanyima wengine fursa za kuwania, Chongolo alisisitiza kuwa hakuna mwanaCCM mkubwa kuliko CCM yenyewe.

Anawahamasisha wanachama wote kuwa wana haki sawa mbele ya chama kwa sababu hata ada ya uanachama wote wanalipa sawa hivyo kila mmoja amthamini mwenzake.

Pamoja na mwongozo na kukemea wanachama wenye tabia za ovyo dhidi ya wengine, Chongolo ameonya wanachama kuacha kunyemelea nafasi za wengine kwa sasa kwa sababu hakuna zilizo wazi na waache fitna, majungu na uzushi.

“Chama kikishamuweka mtu hakina nafasi tena kwa sasa nafasi zimejaa, ni vyema wanaotaka nafasi hizo wasubiri wakati wa uchaguzi wawanie vinginevyo kama yupo kwa sasa ni mvurugaji na huyu anarudisha nyuma maendeleo. “Acheni diwani, mbunge, wafanye kazi zao msiwavuruge, hatuwezi kwenda mbele kama tunabaki kuwaza nafasi, chama kinafanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano, huo ndio muda wa kuomba, ukishaisha, tulia hadi kipindi kingine,” anasisitiza Chongolo.

Msimamo huo wa Chongolo na chama ukapokelewa kwa shangwe na wanachama ambao hawakusita kusema kiu yao ya maswali kuhusu hayo yaliyosemwa imekata kwani amefafanua na kuweka bayana mambo muhimu yanayokisaidia chama kusonga mbele na kufanikiwa zaidi.

Mwanachama wa CCM Kata ya Mwakitolyo, Paschal Jeremia anasema kwa kauli hiyo ya Chongolo vijana wengi ndani ya chama watajitokeza kuwania nafasi za uongozi katika uchaguzi wa ndani wa chama hicho unaendelea kwa sababu amewahakikishia kila mmoja ana haki na fursa ilimradi ajipime kama anatosha kuwania.

Lakini pia Chongolo anawashauri vijana wa hamasa wa CCM kujitokeza kuwania nafasi za uongozi ndani ya chama na waache kuendelea kuwa chawa wa wagombea wengine.

Ziara hiyo katika mikoa hiyo miwili imekuwa chachu kwa wanachama ambao walijitokeza kwa wingi kumsikiliza kiongozi huyo katika mikutano yake ya ndani na nje kwa wananchi na wanachama.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/293bd1c65d7c38e1790d45fb6afd0261.jpg

HAPA nchini Agosti 23 mwaka ...

foto
Mwandishi: Na Ikunda Erick

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi