loader
Simba kujiuliza Mbeya City

Simba kujiuliza Mbeya City

S IMBA leo inashuka Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Mbeya City, ukiwa ni mchezo wa raundi ya 25 kwa timu hizo mbili katika mwendelezo wa mechi za Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Timu hizo zinakutana zikiwa katika nafasi tofauti kwenye msimamo, waliokuwa mabingwa watetezi wapo nafasi ya pili na pointi zao 51 wakati Mbeya City timu ambayo ilikuwa ya kwanza kuchukua pointi tatu dhidi ya miamba hiyo ya soka nchini wapo nafasi ya 10 na pointi 32.

Pamoja na Simba kupoteza taji la ubingwa, lakini mchezo huo bado unatarajiwa kuwa na upinzani mkali kutokana na kutaka kulipa kisasi cha bao 1-0 walichofungwa kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Simba itakayoongozwa na Kaimu Kocha Mkuu Seleman Matola, baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Pablo Franco kufutwa kazi hivi karibuni, ameahidi kushinda mchezo huo ili kumaliza msimu wakiwa na wastani mzuri wa pointi dhidi ya mabingwa Yanga.

Matola ameeleza kuwa maandalizi yao kuelekea mchezo huo yamekwenda vizuri na wachezaji wote wapo katika hali nzuri kwa ajili ya mchezo huo ambao wameupa uzito mkubwa kwa kuhakikisha wanashinda bila kujali kwamba hawana cha kupata mwishoni mwa msimu.

“Kwa muda ambao tumekuwa kambini wiki moja na nusu wachezaji wote wapo katika hali nzuri na wana ari kubwa ya kupambana ingawa tumeshapoteza taji tunachotaka ni kumaliza kwa heshima na rekodi nzuri kwa klabu yetu,” alisema Matola.

Matola ameeleza kuwa hakuna mchezaji ambaye watamkosa kwenye mchezo huo ukimtoa Hassan Dilunga ambaye ni majeruhi wa muda mrefu na Bernard Morrison ambaye siyo sehemu ya kikosi chao kwa sasa na lengo lao ni kushinda na kulipa kisasi cha kupoteza mchezo wa kwanza.

Matola alisema kwa kiasi fulani kikosi chake kitakuwa na mabadiliko, lakini yatakuwa mabadiliko ya kiufundi ambayo hayatavuruga malengo yao katika mchezo huo.

Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Mbeya City, Mathias Lule ameeleza kuwa wamekuja Dar es Salaam kuendeleza kile ambacho walikifanya kwenye mzunguko wa kwanza na amefurahi kucheza kipindi hiki sababu Simba hawapo sawa kutokana na kupoteza taji dhidi ya watani zao Yanga.

Alisema ni mchezo ambao wamepanga kuyatumia madhaifu ya Simba, ili kuzidi kujiimarisha kwa kukaa nafasi nzuri kwenye msimamo, anaamini hilo linawezekana kutokana na utayari wa wachezaji wake na mazoezi aliyofanya.

“Tunaiheshimu Simba sababu ni timu yenye wachezaji wazoefu lakini tumepanga kutumia madhaifu yao kuhakikisha tunaongeza machungu baada ya yale ya kupoteza ubingwa msimu huu, kifupi tunazitaka pointi nyingine tatu kutoka kwa Simba,” alisema Lule raia wa Uganda.

Kocha huyo alisema mashabiki wao watarajie kuona mabadiliko kwenye kikosi chake kutokana na baadhi ya wachezaji kuwakosa kutokana na majeruhi na wengine kutumikia adhabu ya kadi walizooneshwa kwenye michezo iliyopita.

Mbeya City imedhamiria kumaliza msimu huu kwenye nafasi tano za juu.

foto
Mwandishi: Na Mohamed Akida

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi