loader
Hakuna  pingamizi  Yanga

Hakuna pingamizi Yanga

MWENYEKITI wa Kamati ya Uchaguzi wa Yanga, Malangwe Mchungahela, amewataka wanachama wa timu hiyo kuhakikisha wanakamilisha taratibu zote za kikatiba ili waweze kupata fursa ya kupiga kura kuchagua viongozi wapya wa klabu yao.

Uchaguzi Mkuu wa Yanga unatarajia kufanyika Julai 10, ambapo wanachama waliokidhi vigezo watashiriki kupiga kura kuchagua viongozi wapya watakaoiongoza timu hiyo kwa kipindi cha miaka minne.

Hadi jana siku ya mwisho ya kuwasilisha pingamizi, Mchungahela alisema hakukuwa na pingamizi lolote lililowasilishwa katika kamati hiyo ya uchaguzi.

Akizungumza na HabariLEO, Mchungahela ameeleza mpaka sasa taratibu zote zinaohusiana na uchaguzi huo zinakwenda vizuri na hawajapokea pingamizi lolote kuhusu mgombea wa nafasi yoyote kwa sasa.

“Kwetu hii inaonesha kazi ya upembuzi kwa wagombea imefanyika kwa weledi mkubwa na hivyo ndivyo tulivyotaka sababu lengo ni kuhakikisha uchaguzi huu unafanyika kwa amani, uwazi ili kila mtu akapate haki yake,” alisema Mchungahela.

Kiongozi huyo alisema kuwa kwa sasa hawawezi kujua idadi kamili ya wanachama watakaoshiriki kupiga kura sababu bado chaguzi za matawi hazijamalizika, lakini anaamini jambo hilo linakwenda vizuri na muda siyo mrefu utakamilika na Kamati yake itapata idadi kamili ya idadi ya wapiga kura.

Alisema yeye na wenzake wapo imara kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri na washindi wanapatikana kihalali hivyo amewataka wanachama wao kuhakikisha wanakamilisha mapema taratibu zote kabla siku iliyopangwa ya kufanyika kwa uchaguzi huo.

Nafasi zinazogombewa kwenye uchaguzi huo ni Rais, ambayo ina mgombea mmoja pekee Injinia Hersi Said wakati katika nafasi ya Makamu wa Rais inawaniwa na watu wawili, Arafat Haji na Suma Mwaitenda, huku nafasi ya wagombea ujumbe zikiwa na idadi kubwa ya wagombea jambo ambalo linaonesha namna ushindani utakavyokuwa mkali.

foto
Mwandishi: Na Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi