loader
MKWASA: RUVU  HAITASHUKA DARAJA

MKWASA: RUVU HAITASHUKA DARAJA

 KOCHA Mkuu wa Ruvu Shooting, Charles Mkwasa amesema pamoja na kikosi chake kupokea kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Mtibwa Sugar, lakini hawawezi kushuka daraja. Akizungumza jana, kocha huyo mkongwe alikiri kuwa matokeo hayo yamezidi kuwaweka katika wakati mgumu, lakini wamejipanga kuzitumia mechi tatu zilizobaki ili kujiweka kwenye mazingira salama ya kutoshuka daraja.

“Tulikuwa na matarajio makubwa ya ushindi lakini haikuwa kama tulivyo tarajia, tunakubali matokeo na tunarudi kujipanga ili kuhakikisha tunashinda mechi zetu tatu zilizobaki na kujiweka katika mazingira salama,” alisema Mkwasa.

Akizungumzia mchezo huo, Mkwasa alisema ulikuwa mchezo bora kwake sababu wachezaji wake walionyesha uwezo mkubwa hasa kipindi cha kwanza lakini kipindi cha pili walipoteza ubora wao na kutoa nafasi kwa wenyeji wao kufunga mabao hayo.

Alisema yeye ni mtu wa mpira anajua vitu kama hivyo vinatokea, wanarudi kujipanga kwa lengo la kufanya vizuri kwenye mechi zote tatu zilizobaki na anaamini nafasi ya kubaki kwenye ligi hiyo msimu ujao ipo tena kubwa.

Mkwasa alisema kwa hali ilivyo hivi sasa siyo mbaya kama watamaliza hata nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi na hiyo ni kutokana na ushindani uliopo kwenye ligi hasa katika nafasi za chini.

Ruvu Shooting ni miongoni mwa timu zenye uzoefu mkubwa na Ligi Kuu, mpaka sasa kwenye msimu huu imekusanya pointi 28 katika michezo 27 imebakiwa na mechi tatu kabla ya msimu kumalizika.

foto
Mwandishi: Na Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi