loader
JAMES YUSTAR: Kijana wa mitaani mwenye historia ya kusisimua

JAMES YUSTAR: Kijana wa mitaani mwenye historia ya kusisimua

“NILIOKOTWA katika vinywa vya  mbwa ambao walikuwa wakishambulia  boksi lililotupwa jalalani wakijua kuwa  ni mzoga, wale chakula kumbe nilikuwa hai,” hii ni simulizi ya James Yustar mwenye umri wa miaka 32 sasa.

James ambaye aliishi mtaani hadi pale alipofikisha miaka 23, safari ya maisha yake imejaa misukosuko anayosimulia katika kitabu chake cha Maisha Halisi ya Mtoto wa Mtaani.

SAFARI YAKE ILIANZIA HAPA

Mtawa mmoja jina lake Yustar Justine anamsimulia James kuwa mwaka 1989 alifika katika Visiwa vya Lamu nchini Kenya kutoka nchi moja ya Ulaya akiwa na mtawa mwenzake aitwaye Magdalena, watawa hao hawakutaka kufikia kanisani bali walifikia hotelini.

Kwa desturi yao huamka alfajiri kwenda kanisani kwa ajili ya ibada za asubuhi. Siku hiyo alikwenda Yusta peke yake kwa sababu ya ugeni aliomba mlinzi amwelekeze njia inayoelekea kanisani, mlinzi aliamua kumsindikiza.

Kwa mujibu wa James, wakati Yusta akiwa anaingia katika uzio wa kanisa aliwaona mbwa wanne wakiwa pembezoni mwa jalala wakiburuza boksi lililofungwa na kamba ya katani.

“Kwa sababu alikuwa amesindikizwa na mlinzi wa ile hoteli walikwenda kutazama kwa karibu kile kilichokuwa kikiburuzwa na wale mbwa. Aliniambia kuwa walipofika karibu na kumulika tochi waliona damu kwenye boksi akamuomba mlinzi wa kanisa na yule aliyekuwa naye wawafukuze mbwa na kuwaomba wafungue kamba, hawakutaka kushika damu ile lakini yeye alivaa gloves na kufungua,” anaeleza James kama alivyosimuliwa na Yustar.

Ananisimulia zaidi kuwa kilichomsukuma kutaka kujua kilichopo ndani ni pamba za uzazi alizoziona zikining’inia kwani alihisi kuna mtoto.

“Baada ya kufungua alimkuta mtoto mchanga kaviringishwa katika furushi la nguo akiwa hai baada ya hapo alinibeba hadi kwenye nyumba za masista na kuwaeleza, walinisafisha na kunipa huduma zote, hakupata shida kwa sababu pia ni daktari wa watoto. Kisha  alikwenda kuripoti kituo cha polisi na akapatiwa hati ya kumlea mtoto huyo hadi wazazi wake watakapopatikana,” anasema.

James anasema kuwa mama yake huyo (Yustar) alimsimulia kuwa baada ya siku tatu aliendelea na safari yake kuelekea Nairobi kuanza kazi yake iliyomleta nchini Kenya, hata hivyo mwaka 1990 alihamia Kilimanjaro, Tanzania.

Mwaka 1994 aliomba kuacha kazi za utawa ili aweze kuendelea na huduma nyingine na mwaka 1995 aliacha rasmi kazi ya utawa na kuhamia mkoani Arusha.

Kwa mujibu wa James, mama yake huyo alimsimulia kisa hiki akiwa na umri wa miaka saba wakati akisherehekea sikukuu ya kuzaliwa kwake Mei 25 ambayo ndio siku aliyookotwa.

“Alitoa albamu ya picha na kunionyesha picha za kichanga aliyeokotwa pamoja na picha zake kwani historia ya mama huyu pia naye aliokotwa chooni na mmisionari  wa kizungu aliyefahamika kwa jina la Justine alipofika Afrika kwa ajili ya huduma… nilipoona zile picha na masimulizi aliyonipa sikuweza kujizuia nililia sana kwani niliamini kuwa Yustar ni mama yangu mzazi, nilimuuliza maswali mengi alinijibu huku akilia,” anasema.

YUSTAR APATA AJALI

James anasema wiki mbili baada ya kupewa simulizi hiyo, Yustar alipata ajali mbaya katikati ya barabara ya Arusha na Moshi.

“Alikuwa anatoka kuangalia maduka yake yaliyopo Moshi, ajali ilimuumiza maeneo ya kifuani alipelekwa Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu alikaa wiki tatu akaruhusiwa kutoka… siku chache baada ya kurudi aliniita na kunipa hati za nyumba tatu, kadi ya benki na kadi tatu za magari alinisisitiza nizifiche na nisimpe mtu yeyote na ile albamu ya picha zetu,” anaeleza James.

Anaongeza kuwa mama yake alikuwa anazungumza mambo mengi kuhusu maisha na kumuhusia kuwa Mungu atamsaidia na atakua.

“Aliwaita wafanyakazi wote na msimamizi wa mali zake anko Mayasa Mbusia na kuzungumza maneno mengi huku akiwasisitiza kunitunza na kunilea kwa upendo,” anasema na anaongeza kuwa hazikupita siku nyingi mama yake aliugua ghafla akiwa anatoka kuangalia ujenzi na kukimbizwa hospitali lakini alifariki akiwa njiani. Ilikuwa siku ya maumivu makubwa kwangu kumpoteza mtu muhimu katika maisha yangu, mama alizikwa karibu na nyumba yetu,” anasimulia.

ATEKWA KUTOLEWA KAFARA

“Kifo cha mama yangu kilipelekea historia ya maisha kubadilika, baada ya kumaliza msiba yule mjomba ambaye mama alimpa jukumu la kuniangalia na kunihudumia, alianza kubadilika tabia. Aliwafukuza wafanyakazi, mama alikuwa na maduka ya dawa sita Arusha mjini na moshi, pia alikuwa ameanza ujenzi wa zahanati,” anasema.  

Anasema baada ya kuwafukuza alianza kumnyanyasa (James) na kutaka apewe hati alizoachiwa.

“Alisitisha kunipeleka shule kutumia gari ya nyumbani mwisho aliamua kunitumia watu ili waniteke na kuniua. Nikiwa shule mvua kubwa ikiwa inanyesha nilifuatwa na wanafunzi wenzangu wakaniambia unaitwa na mjomba wako. Moyoni nilishtuka, ni zaidi ya miezi miwili anko alikuwa hanipeleki shule wala hanifuati, nikawa najiuliza ama kwa sababu ya mvua ndio imemfanya anifuate?” anasema.

James anasema aliingia kwenye gari lililokuwa likimsubiri na aliuliza anko yuko wapi kwa sababu alikuwa na wasiwasi na kabla hajajibiwa gari liliondoka kwa kasi huku kiti alichokalia kikilazwa ghafla na watu waliokuwa kiti cha nyuma yake na kumuwekea matambara na kumfunga kamba mikononi.

“Tulitembea umbali mrefu sikujua walikokuwa wananipeleka, walikuwa wakizungumza habari za Mererani na kafara walipiga simu wakitoa maelekezo mazingira yaandaliwe tukafika sehemu nisiyojua wakanishusha,” anaeleza James.

Anasema kuwa mvua kubwa ilikuwa inanyesha, walimbeba na kumuweka katika kifusi cha mchanga wa mgodi na kufunguliwa kitambaa usoni wakamuacha hata hivyo, hakutambua aliko kwa sababu ya giza.

“Niliona mwanga wa tochi ukimulika kama watu wanakuja walipoanza kushuka tu kile kibonde radi ilipiga pakawa kama mchana dakika chache ikafuatiwa na ngurumo mara kikasikika kishindo kama tetemeko ambalo liling'oa mti mkubwa na kuwafukia wale watu…nilisikia sauti zao wakisema tunakufaaaa !!! na lile tetemeko lilisababisha mpaka pale kwenye kifusi  nilichowekwa kitetemeke na kumomonyoka, nami nilianza kubinuka kinyume nyume nikiporomokea kwenye majani,” anasimulia James.

 

SIKU TATU ZA MSOTO PORINI

Anasema baada ya tukio hilo alianza kujiburuza kwa makalio usiku mzima ili kusogea kichakani ajifiche.

 “Usiku uliingia sikupata msaada na nilipishana na wanyama lakini Mungu alivyo mkubwa hawakuweza kunidhuru na mimi sikuwa na hofu nao kwani hofu yangu kubwa ilikuwa ni wale watu waliotaka kuniua,” anaeleza.

James anasimulia kuwa asubuhi siku ya tatu mwili ulikuwa umechunika na nguo za shule alizovaa zilikuwa matambara na  nguvu ya kujiburuza alikuwa hana akapumzika kidogo baada ya muda akaanza kujiburuza tena na alifika mahali kuna mti mkubwa wakati amepumzika akapitiwa na usingizi.

“Sikumbuki nililala kwa muda gani, lakini nilipoamka ilikuwa giza limeanza nilikuwa na nguvu kidogo nikaanza kujiburuza nikiwa katika hali hiyo mara walitokea simba wawili ambao walikuwa wanakimbizana kwa ile hofu nilitetemeka nikaishiwa na nguvu na kupoteza fahamu,” anasema.

Anasema alipozinduka alijikuta amezungukwa na kundi la watu wa jamii ya Kimasai walioanza kumhudumia kwa dawa za asili na alipona lakini hakuweza kuzungumza kwani koo lilikuwa na damu na usaha hata kula alishindwa kwa mwezi mmoja na alikuwa akinywa maziwa yaliyochanganywa na dawa.

James anasema baada ya miezi kadhaa alirudi katika hali ya kawaida japo hakuweza kuzungumza vizuri hadi leo na anabainisha kuwa ilichukua muda kumshawishi aliyekuwa anamhudumia kuondoka kwake na kurudi Arusha kwani alitamani kuendelea na shule.

Baada ya kuruhusiwa kuondoka alipewa zawadi ya ng’ombe wawili na aliwauza katika mnada na kupata fedha na kupanda gari kwa safari ya kuelekea Arusha.

James baada ya kufika alianza kwenda kwenye maduka ya mama yake alichokikuta hakuamini macho yake, zile fremu zilikuwa zinauza bidhaa nyingine.

“Nilipouliza nikaambiwa anko Mayasa amefunga biashara na kuhamia Kenya, nilianza kupata wasiwasi ikabidi nipande gari niende nyumbani huko nikakuta nyumba yetu imepakwa rangi mpya na imepambwa zaidi ya mwanzo. Nilifika getini na kugonga, mlinzi alifungua nikaingia na kuniuliza ninachotaka… nilipoingia mlinzi akaniuliza wewe mtoto wa maasai unaingia humu umeleta nini? Nikamwambia mimi sio maasai, naitwa James Yustar, mtoto wa Dk Yustar, hapa ndio nyumbani kwetu, wewe nani hunijui?

 “Yule mlinzi aliamua kunifukuza kwa kunitoa nje kwa nguvu, nami nikawa nimekasirika tukaanza kuvutana mwisho nilianguka mlinzi aliniburuza na kunitoa nje kisha akafunga geti,” anasema.

Anaongeza kuwa: “Mara gari ikawa imekuja inataka kuingia mle ndani, nikajua atakuwa anko, nikainuka haraka na kukimbilia dirishani nikawa napiga kelele kioo kikafunguliwa mzungu akazungumza kwa kiswahili cha kubabaisha akaniuliza "una shida ganii?"  nikamwambia namtaka anko yuko wapi?

“Alikuwa na dada mswahili akajibu Mayasa hajawaaga huko kwenu, mfuateni anapoishi, hapa ameshapauza,  msitusumbue, alizungumza kwa ukali sana, kisha wakafunga vioo na mlinzi aliwafungulia geti wakaingia nami nikawa nimeingia tena ndani ya geti, mlinzi alianza tena kuniburuza na kunitoa nje nililia sana,” anasimulia.

Anaeleza kuwa baadaye aliamua kwenda kumtafuta rafiki wa anko Mayasa. “Alikuwa na duka stendi kuu, sikumkuta ila nilimkuta mdogo wake, lakini alinielewa na kunielewesha anko ameuza kila kitu na yeye ameondoka hajulikani alipo, wengine wanasema yuko Afrika Kusini na wengine wanasema yuko Kenya.

Kijana huyo alimshauri aende parokiani ili akaonane na masista ili waweze kumsaidia na alipokuwa njiani alikutana na rafiki yake ambaye alikuwa analelewa kwenye kituo cha masista.

 

MAISHA YA MTAANI

James anaeleza kuwa wakati akiwa njiani kuelekea huko alimuona mtoto ambaye walikuwa wakimkuta katika kituo hicho wakati huo alikuwa akiuza sigara.

“Anaitwa Bruno, nilimfuata mbio na kumsimamisha, alifikiri nahitaji sigara. Alishangaa kuniona nikimchangamkia sana, nilipoona yuko na mshangao vile nikamwambia mimi James Yustar, kisha nikamsisitiza akanikumbuka haraka,” anasema.

Rafiki yake alimpa pole kwa aliyopitia na kuanza kumsimulia sababu za kutoka  kituoni na kuingia mtaani kuuza sigara.

James anasema Bruno alikuwa hapendi kukaa katika kituo cha watoto yatima hivyo alitoroka na kwenda kwa baba yake lakini alivyofika huko alikutana na mama wa kambo ambaye hakumpenda.

Anaeleza kuwa Bruno aliamua kutoroka  tena ambapo safari hii baba yake alichukia zaidi akaona ampeleke kituo cha mbali, wakati huo walikuwa wanaishi Same Mashariki, hivyo aliamua ampeleke Arusha kwenye kituo cha masista.

James anasema alianza kupata amani kwani aliamini amekutana na mtu ambaye wanapendana na walianza kupanga safari ya kwenda Namanga mpakani mwa Kenya kuuza pipi, sigara na karanga.

 “Wakati huo Bruno alikuwa na miaka 12 nami nilikuwa na miaka nane, maisha ya kule Namanga sikuyapenda kwa kuwa watu walikuwa wanagombana kila siku wanachomana visu, nikawa naogopa sana.”

James aliogopa baada ya kumsikia rafiki yake Bruno akipanga kutafuta fedha anunue silaha na kwenda kulipiza kisasi kwa baba yake na mama yake wa kambo na kusikia maneno hayo aliogopa na aliamini Bruno ameathiriwa na uvutaji wa bangi na ulaji wa mirungi, hivyo taratibu alimwambia  kuwa aache kutumia dawa hizo.

Anasema miezi mitatu ya kukaa Namanga walipata fedha za kutosha  hivyo walipanga kusafiri kwenda jijini Dar es Salaam kutafuta fedha zaidi.

James anasema hatimaye walifika Dar es Salaam na kukaa mitaani na siku moja rafiki yake alifika maeneo ya Kariakoo na kubaini sehemu nzuri ya kufanya biashara na kukaa.

“Tuliendelea kufanya biashara eneo la Kariakoo ya kuuza mifuko lakini nilikuwa na wazo la kusoma ikabidi nitafute shule, baada ya kuzunguka shule kadhaa nilibahatika kupata shule na kusoma kupitia kwa marafiki niliokutana nao dogodogo center,” anasema. 

Kwa mujibu wa James, alipofika darasa la sita rafiki yake Bruno alipata ajali ya gari kitu ambacho kilisababisha kifo chake.

“Sehemu kubwa ya maisha yangu yaliathirika, niliacha shule na rasmi nikaanza kushinda mitaani, sikuwa na kazi nyingine zaidi ya kuomba omba mitaa ya Kisutu, Posta na Mitaa ya Ohio na marafiki zangu wa kituo cha dogodogo hata hivyo nikaona sio sahihi nikaanza kazi ya kuosha magari,” anasema.

James anasema katika harakati hizo alikutana na marehemu Amina Chifupa, kaka Bonda pamoja na Masoud Kipanya ambao kila Jumamosi walikuwa wanamchukua anakwenda kujiunga na watoto wengine kwenye kipindi cha chuchuchu.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/0a08a1fb6e671dcbbdd8b3df54e17783.jpg

HAPA nchini Agosti 23 mwaka ...

foto
Mwandishi: Aveline Kitomary

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi