loader
Ufaransa yatoa bil 195/- kuleta neema ya maji Shinyanga

Ufaransa yatoa bil 195/- kuleta neema ya maji Shinyanga

SERIKALI ya Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) wamesaini makubaliano ya mkataba wa mkopo wa Sh bilioni 195 kwa ajili ya mradi wa kusambaza majisafi, kutoa majitaka na usafi wa mazingira katika Mkoa wa Shinyanga.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba na Balozi wa Ufaransa nchini, Nabil Hajlaoui pamoja na Mkurugenzi wa Mkazi wa AFD, Stephanie Mouen walisaini mkataba huo jana Dar es Salaam. Tutuba alisema fedha hizo zitasaidia kutoa huduma endelevu ya upatikanaji wa majisafi na usafi wa mazingira katika Manispaa ya Shinyanga na miji jirani ya Iselamaganzi, Didia na Tinde.

“Hii ni ajenda kubwa inaendana na Mpango wa Tatu wa Taifa wa Miaka Mitano ulioanza mwaka 2021/22 hadi 2026 unaotoa vipaumbele pamoja na mengine ya upatikanaji na usambazaji maji,” alisema Katibu Mkuu Hazina. Alisema mradi huo utawanufaisha wananchi zaidi ya 306,566 kwa kuongeza upatikanaji wa maji kwa siku kutoka mita za ujazo 25,877 hadi 33,944 kwa siku.

Alitoa angalizo kwa mamlaka zinazotekeleza mradi huo ikiwamo Wizara ya Maji na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA), zizingatie thamani ya fedha kwa kuutekeleza kama ulivyopangwa. Balozi Hajlaoui alisema lengo la kuufadhili mradi huo ni kuboresha maisha ya wananchi, mazingira na maendeleo ya kiuchumi. “Tunataka kusaidia kufikia Malengo Endelevu ya Maendeleo (SDGs) ya kuwa na majisafi na kuboresha maisha ya wananchi,” alisema Balozi Hajlaoui.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shuwasa, Yusuph Katopola alisema mradi huo utaanza kutekelezwa mwakani kwa miaka mitatu. Katopola alitaja baadhi ya kazi zitakazofanywa kuwa ni kujenga mtandao wa miundombinu ya kusambaza majisafi yenye umbali wa kilometa 210 katika Manispaa ya Shinyanga na miji mitatu inayonufaika.

Alisema upatikanaji wa maji kwa sasa katika miji hiyo ya Tinde, Didia na Iselamaganzi ni asilimia chini ya 20 na kwamba mradi huo utawezesha ifike asilimia 95. Katopola alisema miundombinu ya maji taka katika Manispaa ya Shinyanga itaboresha huduma hiyo kwa kufikisha asilimia 40 na kwa sasa eneo hilo halina huduma hiyo.

foto
Mwandishi: Na Ikunda Erick

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi