loader
Maandalizi Sabasaba asilimia 95, nchi 20 zathibitisha kushiriki

Maandalizi Sabasaba asilimia 95, nchi 20 zathibitisha kushiriki

MAANDALIZI ya Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, Sabasaba yamekamilika kwa asilimia 95. Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), David Langa alisema hayo Dar es Salaam wakati akizungumza na HabariLEO.

“Kwa kiasi kikubwa mabanda yote na maeneo ya wazi yameshapata washiriki, ambapo wapangaji wa kudumu wote watashiriki na wapangaji wa msimu nao wamekwisha oneshwa maeneo yao, kilichobaki nikulipia,” alisema Langa.

Alisema maonesho hayo yatafunguliwa Juni 28, mwaka huu na hadi Juni 17, mwaka huu nchi 20 zilikuwa zimethibitisha kushiriki ikiwamo Marekani ambayo haijawahi kushiriki tangu yalipoanzishwa miaka 46 iliyopita. Alitaja baadhi ya nchi ambazo zimethibitisha kushiriki ni Botswana, China, India, Ujerumani, Syria, Iran, Kenya, Poland, Morocco, Rwanda, Nigeria, Ghana, Misri, Uganda, Burundi, Angola na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

“Kutokana na nchi nyingi kuruhusu raia wake kutoka nje ya nchi zao kumesababisha washiriki wa kimataifa kuwa wengi ikilinganishwa na mwaka jana,” alisema Langa. Alisema kwa mara ya kwanza mwaka huu kutakuwa na programu ijulikanayo kama Urithi Wetu itakayokusanya wanafunzi wa sekondari waliofaulu vizuri kutoka mikoa ya pembezoni mwa nchi wakiwa na walimu na wazazi wao.

“Lengo la programu hii nikutoa elimu na uelewa kwa kizazi cha sasa ili wawe mabalozi wazuri kwa wenzao warudipo mikoani nakuwaeleza umuhimu wakujali vya kwetu, ambapo wazazi, wanafunzi na walimu hao watagharamiwa huduma za usafiri kutoka mikoa husika, malazi na chakula nakupelekwa katika vivutio mbalimbali vilivyopo Jiji la Dar es Salaam na viunga vyake,” alisema.

Langa alisema mikoa itakayonufaika kwa kuanzia ni ya pembezoni ikiwamo Manyara, Lindi, Dodoma na Unguja Kusini, ambapo kila mkoa utatoa shule sita za wanafunzi waliofanya vizuri kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne. Alisema katika maonesho hayo kiingilio kwa wakubwa ni Sh 3,000 na watoto na wanafunzi Sh 1,000.

“Tiketi za kiingilio zitapatikana katika vituo vya mabasi ya mwendokasi na getini uwanjani,” alisema. Maonesho hayo yatamalizika Julai 13, mwaka huu.

foto
Mwandishi: Na Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi