loader
Tamisemi yatoa maelekezo uteuzi viongozi wa elimu

Tamisemi yatoa maelekezo uteuzi viongozi wa elimu

OFISI ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imeelekeza uteuzi wa viongozi wa elimu katika ngazi za shule, kata, halmashauri na mikoa uzingatie umahiri na uzoefu wa usimamizi.

Waziri wa Tamisemi, Innocent Bashungwa alitoa maelekezo hayo jana wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Umoja wa Maofisa Elimu Maalumu Tanzania Bara (Umemta). Alizitaka halmashauri zote ziwape ushirikiano maofisa ualimu maalumu wanapotekeleza majukumu yao ili kuimarisha huduma kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Pia aliagiza maofisa elimu wote waendelee kuijengea jamii uelewa kuhusu upatikanaji wa elimu kwa watoto wenye mahitaji maalumu. Aidha, aliwaagiza viongozi hao waboreshe miundombinu na mazingira ya kujifunzia na kufundishia katika shule ili ziwe rafiki kwa wanafunzi wote wakiwemo wenye mahitaji maalumu.

Bashungwa alisema serikali imekuwa ikifanya jitihada kubwa kutoa elimu kwa watu wenye ulemavu kwa kuwabaini na kuhakikisha wanaandikishwa kujiunga na elimu ya msingi na kwamba mwaka huu watoto 16,377 walibainika na kuandikishwa kwenye shule stahiki. Alisema serikali pia imeboresha miundombinu kwa kuwajengea mabweni 50 wanafunzi wa shule za msingi yenye gharama ya Sh 4,000,000,000, kununua vifaa na visaidizi maalumu vyenye thamani ya Sh bilioni 4.5 ili kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu wanapata fursa ya kupata elimu kwa faida yao, jamii na nchi.

Bashungwa aliagiza ifikapo mwishoni mwa mwezi ujao uwe umeundwa mkakati wa kuboresha elimu ili kuongeza namna bora ya utekelezaji wa mitaala katika kuzibainisha changamoto na kupata ufumbuzi wa nini kifanyike ili kuimarisha ufundishaji na kujifunza. Alimuagiza Katibu Mkuu wa Tamisemi ndani ya siku saba wakurugenzi ambao hawakuruhusu maofisa elimu maalumu kuhudhuria mkutano huo wawe wamejieleza.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/12237bc8a5846fa5afa0de9f80dee4b1.jpeg

MKURUNGENZI wa Kampuni ya Prosperity ...

foto
Mwandishi: Na Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi