loader
TPA inavyosikiliza wateja wake

TPA inavyosikiliza wateja wake

“KAWAIDA tunazungumza, tunakutana lakini leo tumemtembelea ofi sini kwake, kwanza kumshukuru kwa kazi tunayofanya naye katika bandari za Tanzania ikiwemo Bandari ya Dar es Salaam na Bandari ya Tanga, ambako mizigo kutoka na kuingia Rwanda inapitia.

“Kwa hivyo ni muhimu sisi kama ubalozi tuwe karibu sana na Mkurugenzi Mkuu wa ports (bandari) za Tanzania. So (kwa hiyo) kila mara tunajaribu kuona changamoto gani zipo pale.

Maboresho ya miundombinu yamefanyika, so (kwa hiyo) kila siku kunakuwepo na ongezeko la mizigo kwani economy (uchumi) inapanuka hivyo ni muhimu sana sisi kama balozi tuwe karibu sana na ports za Tanzania ili kuhakikisha kwamba watu wetu huduma wanazopata ni za hali ya juu.

“Tunamshukuru mheshimiwa Eric Hamissi kwa usaidizi wake, yuko karibu nasi kila siku tukimtaka tunampata na leo tulikuwa na mambo mengi sana tumezungumza, changamoto tulizokutana nazo na tunatumaini atazifanyia kazi.” Anasema Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Meja Jenerali Charles Karamba wakati alipotembelea bandari hiyo hivi karibuni.

Ujio wa Balozi wa Rwanda makao makuu ya TPA ni matokeo ya uwazi uliopo ndani ya mamlaka hiyo katika kuhudumia wateja. Wateja wamewekewa mlango wazi kwa mazungumzo ili kutanua zaidi ufanisi na tija katika huduma za bandari. Pia ujio wa namna hiyo sehemu ya mikakati endelevu ya kimasoko inayofanywa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa nchi jirani kwa lengo la kudhibiti soko la bidhaa.

Kwa Rwanda sasa hivi soko limekuwa na kufikia karibu asilimia 90 kwa mwaka. Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Eric Hamissi anasema kwamba kukua kwa soko hilo, kumetokana na mikakati ya kimasoko inayofanywa na Mamlaka hiyo nchini humo. Kazi hiyo pia inafanyika katika nchi za Zambia, Burundi, Jamhuri ya Watu wa Congo na Uganda.

“Pamoja na mikakati yetu ya kimasoko pia tunaishukuru jamii ya wafanyabiashara nchini Rwanda kwa kuzitangaza na kutumia bandari zetu za Dar es Salaam na Tanga kupitisha bidhaa zao,” anasema Hamissi.

Hamissi ameongeza kwamba TPA imeweka nguvu kubwa katika kurudisha uhusiano mzuri zaidi na jamii ya wafanyabiashara wa Rwanda na mataifa mengine yanayotumia bandari zake ili kuendelea kuhudumia masoko hayo kwa ufanisi zaidi. Na kila anayeingia katika mazungumzo huwa na kitu cha kuondoka nacho na mara zote TPA imekuwa na maneno yenye uthabiti mkubwa wa huduma yenye ufanisi na tija na ndicho kinachofanyika.

Katika mazungumzo kati ya Balozi wa Rwanda na Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mkurugenzi huyo alimuahidi Balozi na jamii ya wafanyabiashara nchini Rwanda kwamba TPA itaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza ili kurahisisha na kuboresha zaidi huduma zinazotolewa na bandari kwa wafanyabiashara hao.

“Mhe Balozi tunakuahidi kuwa tutaweka mazingira mazuri zaidi katika kutoa huduma kwa bandari zetu ili kuongeza ufanisi na kurahisisha zoezi la utoaji wa mizigo katika bandari zetu,” anasema Hamissi. Naye Balozi Karamba, amesema kwamba wao kama ubalozi hawana budi kuwa karibu na uongozi wa TPA kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu ili iwe rahisi kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza.

Mizigo inayopita katika Bandari za Dar es Salaam na Tanga imekuwa ikiongezeka kutokana na huduma nzuri wanazopata bandarini pamoja na maboresho ya miundombinu yanayoendelea. Balozi ameongeza kwamba uchumi wa nchi zao umekuwa ukikua na hivyo kuchochea ukuaji wa shehena ya mizigo inayopita bandari za Dar es Salaam na Tanga na kwenda au kutoa nchini Rwanda.

Shehena ya Rwanda inayopita katika Bandari ya Dar es Salaam na Tanga imekua kutoka tani 922,135 mwaka 2017/2018 hadi kufikia tani 1,293,531 kwa mwaka 2020/2021. Bidhaa zinazosafirishwa zaidi ni pamoja na bidhaa za vyakula, vifaa vya umeme, ujenzi, pembejeo za kilimo na magari. Mizigo ya Rwanda husafirishwa hadi nchini humo kupitia barabara huku asilimia ndogo tu ikisafirishwa kwa njia ya reli.

Kwa kutumia Bandari ya Dar es Salaam, watumiaji wanakuwa wamepunguza umbali kwa zaidi ya kilomita 300 kama wangelitumia nchi jirani. Hata hivyo, ukarabati na ujenzi unaoendelea wa SGR unaotarajia kuwa na tawi kutoka Isaka, Kahama nchini Tanzania hadi Kigali, Rwanda unatarajiwa kuongeza matumizi ya Bandari ya Dar es Salaam; na kwa matumizi ya reli kutakuwa na nafuu zaidi kigharama na muda.

Usafirishaji wa shehena ya Rwanda kwa njia ya barabara mwaka wa 2020/21 ilikuwa tani 729,852 ikiwa ni ongezeko la 13.17% ikilinganishwa na mwaka uliopita ambao ulirekodi tani 644,902. Hata hivyo, katika mwaka wa 2020/21, Rwanda haikusafirisha mizigo yake kupitia reli kama ilivyokuwa mwaka 2019/20 ambapo ilisafirisha tani 646 kwa reli.

Ongezeko la mizigo kutoka Rwanda inatokana na Bandari ya Dar es Salaam kuwa shindani ikiwamo ushuru kwani bandari ya Dar inatoza 40% na 29% chini katika kushughulikia uagizaji wa makontena ya futi 20 na 40 mtawalia, ikilinganishwa na bandari jirani. Aidha, kuna muda mfupi wa usafiri wa siku 3 kutoka Dar hadi Kigali ikilinganishwa siku 5 -10, kulingana na msongamano wa kuvuka mpaka, kutoka Mombasa hadi Kigali.

Pia nchi kama Burundi na DRC nazo hutumia njia ambayo Rwanda hutumia na wao pia kwa kutumia Bandari ya Dar es Salaam wanapunguza sana gharama. Kwa Zambia kuna bomba la mafuta la Tanzam lakini pia kuna reli ya Tazara ambayo ni kiunganishi kizuri cha kuihudumia nchi hiyo kutoka Bandari ya Dar es Salaam, kimsingi nchi jirani na Tanzania kwa kutumia bandari za Tanzania wanajiweka katika nafasi kubwa ya kukuza uchumi kupitia sekta ya usafirishaji.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/d8c7eda3b6849530495b32c47d79e2f2.jpeg

HAPA nchini Agosti 23 mwaka ...

foto
Mwandishi: Na Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi