loader
Rwanda, EAC kunufaika na mkutano wa Madola

Rwanda, EAC kunufaika na mkutano wa Madola

MKUTANO wa Nchi za Jumuiya ya Madola (CHOGM) ulioanza jana na ambao utaendelea hadi kufi kia Juni 26 mwaka huu, unatarajiwa kuinufaisha Rwanda kibiashara, uwekezaji, teknolojia, utalii pamoja na utamaduni.

Mkutano huo unatarajiwa kuleta idadi kubwa ya wageni nchini hapa wakitoka katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola na nchi zisizo wanachama wa jumuiya hiyo kutoka katika maeneo mbalimbali duniani. Kwa mujibu wa Serikali ya Rwanda, mkutano huo unatarajiwa kuwakutanisha wafanyabiashara zaidi ya 300 kutoka maeneo mbalimbali duniani watakaoshiriki kongamano la kibiashara pembezoni mwa mkutano wa CHOGM.

Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Vicent Biruka, alisema mkutano utakuwa na wageni zaidi ya 8,000 kutoka mataifa zaidi ya 54 duniani. Kwa mara ya mwisho mkutano kama huo ulifanyika barani Afrika miaka 15 iliyopita katika Jiji la Entebbe nchini Uganda.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dk Peter Mathuki alisema Rwanda itafaidika kama nchi mwenyeji na kwamba faida kubwa zaidi itakuwa kwa nchi za EAC kwa kuwa wanachama wake wanne ni wajumbe wa mkutano huo. Mbali na Rwanda, Mathuki alisema nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Madola kutoka katika EAC ni Tanzania, Uganda na Kenya hivyo ni sifa kubwa na heshima kwa jumuiya hiyo.

“Ni heshima kubwa kwa Afrika Mashariki kuona kuwa tuna uwezo wa kuhimili mkutano mkubwa kabisa kama huo; nadhani ni kitu tunachopaswa kujivunia kwa kuwa sekretarieti yetu itashiriki kikamilifu katika mkutano huo,” alisema.

foto
Mwandishi: Na Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi