loader
Mwanafunzi auawa, atupwa pembeni ya mto

Mwanafunzi auawa, atupwa pembeni ya mto

JESHI la Polisi mkoani Geita linachunguza kifo cha mwanafunzi wa darasa la saba, Shule ya Msingi Buhalahala mjini Geita, Johnson Thomas (14), ambaye amekutwa amefariki dunia na mwili wake ukiwa umetupwa pembezoni mwa mto.

Taarifa hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Kamishina Msaidizi (ACP), Henry Mwaibambe, wakati akizungumuza na waandishi wa habari mjini Geita, ambapo hadi sasa hakuna mtu anayeshikiliwa.

Kamanda Mwaibambe amebainisha, mwili wa mwanafunzi (kijana) huyo umepatikana siku ya Juni 18 mwaka huu majira ya saa 11 jioni tangu alipoondoka nyumbani kwao siku ya Juni 12 mwaka huu na kupotea kusikojulikana.

“Uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtoto huyo alitoka nyumbani kwao kwa kutumia usafiri wa bajaji iliyokuwa inaendeshwa na Benson Theophili siku ya Juni 12, majira ya saa 11 jioni kuelekea Buhalahala Senta kupeleka sare za shule kwa ajili ya kushonewa.

“Mara ya mwisho mtoto huyo alionekana na mwanafunzi mwenzie ambaye jina lake limehifadhiwa akielekea barabara inayoelekea ofisi za GPH Buhalahala, ambapo ni tofauti na kule alipokuwa anaishi na hakuonekana tena mpaka alipokutwa amefariki.

“Mwili wa marehemu una majeraha mguu wa kushoto, huku kama ulipondwa na kitu kizito, ambacho hakijafahamika. Awali mwili wake ilisadikika kijana huyo unyayo wake umekatwa na jicho limenyofolewa, lakini uchunguzi ulipofanyika viungo hivo vimekutwa vimepondeka,” amesema.

Awali akizungumuza na waandishi wa habari katika ibada ya mazishi ya kijana huyo, msemaji wa familia, Theophili Mkwata, amesema baada ya kuupata mwili wa kijana huyo walikuta ukiwa umechapwa na mijeredi mingi na kuharibiwa sehemu ya mguu mmoja na jicho moja limeharibiwa.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Buhalahala, Sylivester Mathias, amekiri kupokea taarifa za kupotea kwa Johnson, ambapo walifanya juhudi kumtafuta mwanafunzi huyo kwa kushirikisha wanafunzi wengine, lakini hawakufanikiwa kumpata.

foto
Mwandishi: Yohana Shida, Geita

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi