loader
Walioitwa mafunzo JKT wapewa siku tatu

Walioitwa mafunzo JKT wapewa siku tatu

JESHI la Kujenga Taifa (JKT), limetoa siku tatu kwa vijana walioitwa kuhudhuria mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria kwa mwaka 2022, ambao hawajaripoti mpaka sasa kuripoti makambi ya JKT mara moja.

Pia JKT imetoa nyongeza ya majina ya vijana waliohitimu elimu ya kidato cha sita mwaka 2022 kujiunga na mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria kwa mwaka 2022.

Haya yameelezwa jijini hapa na Mkuu wa Tawi la Utawala JKT, Brigedia Jenerali, Hassan Mabena alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu wito wa kujiunga na mafunzo ya JKT kwa Mujibu wa Sheria mwaka 2022 Awamu ya Pili.

Alisema Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele anawataka kuripoti makambini vijana wote walioitwa kuhudhuria Mafunzo ya JKT Kwa Mujibu wa Sheria kwa mwaka 2022, ambao hawajaripoti mpaka sasa waripoti makambi ya JKT mara moja.

Alisema vijana hao wanaotakiwa kuripoti makambi ya JKT yaliyo karibu na maeneo wanayoishi.

" Vijana hao wote waripoti makambi ya JKT yaliyo karibu na maeneo wanayoishi, isipokuwa Kambi ya Makutupora JKT iliyopo mkoani Dodoma, Chuo Cha Ungozi Cha Jeshi la Kutenga Taifa(CUJKT) iliyopo Kimbiji mkaoni Dar es Salaam na Ruvu JKT iliyopo Mlandizi mkoani Pwani, ambayo inapokea wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana kwa macho yenye miundombinu ya kuwahudumia watu wa jamii hiyo," alisema.

Alisema vijana hao wote wanatakiwa kuripoti makambi ya JKT kuanzia jana hadi Juni 25 mwaka huu.

" Orodha kamili ya majina ya vijana walioitwa awamu ya pili, vifaa vinavyotakiwa kwenda navyo vipatikana katika tovuti ya JKT ambayo ni www.jkt.go.tz.

" Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele anawakaribisha vijana wote walioitwa ili waweze kujiunga na vijana wenzao katika kujifunza uzalendo, umoja wa kitaifa, stadi za kazi, stadi za maisha na utayari wa kulijenga na kulitumikia Taifa,” alisema.

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi