loader
Mahakama Kuu yatupa kesi ya Mdee, wenzake

Mahakama Kuu yatupa kesi ya Mdee, wenzake

MAHAKAMA Kuu Masjala Kuu imetupilia mbali maombi ya Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Halima Mdee na wenzake  19 waliokuwa wakiomba kibali cha kufungua kesi kupinga kuvuliwa uanachama wa chama hicho.

Katika maombi yao Mdee na wenzake walikuwa wakiomba kibali cha kufungua kesi dhidi ya Bodi ya Wadhamini ya Chadema, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG). 

Uamuzi huo umetolewa leo Juni 22, 2022 na Jaji Mfawidhi, John Mgeta. baada ya kutoa umuzi wa hoja za mapingamizi zilizotolewa na Wakili wa Mjibu maombi wa kwanza (Bodi ya Wadhamini ya Chadema) aliyeomba maombi ya Mdee na wenzake yasisikilizwe na yatupiliwe mbali kwa kuwa yalikuwa na dosari.

Akisoma uamuzi huo Jaji Mgeta alikubaliana na hoja mbili ambazo ni hoja ya tatu na ya sita kati ya hoja sita zilizowasilishwa katika mapingamizi ya Kibatala na kutupilia mbali hoja nyingine nne.

Katika hoja ya tatu Kibatala alilalamikia mahakama kuwa Mdee na wenzake walishindwa kuambatanisha taarifa halali na pia katika hoja ya sita wapeleka maombi wamemshtaki mlalamikiwa ambaye hayupo (Bodi ya Wadhamini Chadema), walipaswa kulalamikia wadhamini waliosajiliwa.

"Nakubaliana na Kibatala kuwa waleta maombi walipaswa kuwashtaki wadhamini waliosajiliwa badala ya Bodi ya Wadhamini ya Chadema ambayo haiwezi kusimama kama mshtakiwa kisheria," alisema.

Alisema kuwa pamoja na maelezo mengine yote aliyotoa maombi hayo yanakosa mashiko na akayatupa.

Baada ya kuyatupa maombi ya Mdee na wenzake, Jaji Mgeta alitoa uamuzi wa hali ya ubunge wao na kusema kuwa maombi ya kubaki na ubunge yanakosa pa kusimamia hivyo aliondoa zuio lililowekwa na mahakama hiyo awali la kuwataka wabaki na ubunge wao.

Nje ya mahakama, Katibu Mkui wa Chadema John Mnyika, alisema kwa uamuzi huo haki imeshinda udhalimu, dhulma na usaliti na anaamini kwa kuwa hukumu imeshatolewa Wakili Mkuu wa Serikali atapeleka taarifa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na hatimaye itamfikia  Spika wa Bunge.

"Spika naye katika vikao vya Bunge  vianavyoendelea leo na kesho anapaswa kutekeleza matakwa ya kikatiba ya kuwaondoa wale wasiokuwa na chama na hatua zingine tutazieleza baadaye," alisema.

Sakata la kesi hii lilianza baada ya mkutano wa Baraza Kuu la Chadema uliofanyika Mei 12, 2022 uliyosababisha uamuzi wa wabunge hao kupigiwa kura za kuvuliwa uanacahama na matokeo yakaonesha kura nyingi zilitaka Baraza hilo kuwavua uanachama wabunge hao na ikaafikiwa wavuliwe.

Katika kesi hiyo wabunge hao waliwakilishwa na jopo la mawakili nane wakiongozwa na Wakili Aliko Mwamanenge huku upande wa mjibu maombi kwanza (Bodi ya Wadhamini ya Chadema) ukiwakilishwa na jopo la mawakili wanne wakiongoza na Wakili Peter Kibatala na wajibu maombi namba mbili na tatu (NEC na AG) waliwakilishwa na jopo la mawakili nane wakiongozwa na Wakili wa Serikali, Stanley Kalokola.

foto
Mwandishi: Anna Mwikola

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi