loader
Sirro ataka wafanyabiashara washirikiane na Polisi

Sirro ataka wafanyabiashara washirikiane na Polisi

MKUU wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP, Simon Sirro amezindua ofisi mpya ya kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Iringa na ghala la kutunzia silaha katika kituo kikuu cha Polisi cha mjini, mapema leo.

Wakati ofisi ya kikosi cha usalama barabarani imejengwa kwa msaada wa kampuni ya Ivori Iringa,  ghala la kutunzia silaha limejengwa na Asas Group of Companies.

Akizindua majengo hayo, IGP Sirro aliwashukuru wadau hao kwa michango yao mikubwa, akisema inasaidia kuliongezea jeshi hilo ufanisi katika utendaji wake kazi.

Alisema ghala la kutunzia silaha lililojengwa na Asas Group of Companies ni bora kuliko mengine yote ya vituo mbalimbali vya Polisi nchini.

”Nawashukuru Asas na Ivori Iringa kwa misaada yao kwa jeshi la Polisi. Wafanyabiashara wengine acheni ubahiri,  kama hakuna ulinzi,  hamuwezi kulala kwa raha kwani mtakuwa na hofu kubwa ya kuibiwa mali zenu.

“Nawaomba mjitokeze kulichangia jeshi la Polisi, ili lifanye kazi yake sawasawa,” alisema.

Alisema Jeshi la Polisi ni mali ya wananchi na kwa muktadha huo wanatakiwa kulipa ushirikiano ukiwemo wa kusaidia kuboresha mazingira ya utendaji wake kazi.

Alizungumzia pia ulinzi shirikishi alisema Jeshi la Polisi haliwezi kuifanya  kazi ya kulinda wananchi na mali zao pekee yake.

”Halmashauri zitunge sheria za ulinzi shirikishi, ili katika maeneo yote kuwepo na vikundi vya kijamii vinavyofanya ulinzi mitaani kwa gharama za wananchi wenyewe, " alisema na kuwataka hata wale wananchi wenye walinzi wao binafsi au silaha kuchangia ulinzi shirikishi maarufu kama polisi jamii.

Awali Mkurugenzi wa Asas Group of Companies,  Ahamed Salim Asas alisema wataendelea kushirikiana na jeshi la Polisi katika nyanja mbalimbali, ili kurahisisha utendaji kazi wake.

Pamoja na ahadi hiyo Asas aliwataka wananchi kushirikiana na jeshi hilo kukabiliana na makosa ya usalama barabarani, na uhalifu vikiwemo vitendo vya ukatili wa kijinsia na ubakaji wa watoto.

Naye Mkurugenzi wa Ivori Iringa,  Suhail Esmail Thakore alisema waliamua kujenga jengo hilo la usalama barabarani kwa kuwa wanatambua kazi kubwa inayofanywa na kikosi hicho na jeshi la Polisi kwa ujumla wake katika kulinda wananchi na mali zao.

”Tutaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kadri tutakavyopata fursa. Sisi ni wadau na tunaamini tunatakiwa kuwa sehemu ya usalama wa Taifa hili, ” alisema.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/0442ebe5936f643e98ffc597869885cc.jpg

WAFANYABISHARA mbalimbali wa Temeke, ...

foto
Mwandishi: Frank Leonard, Iringa

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi