loader
Serikali awamu ya sita ilivyoiongezea mwendo sekta binafsi

Serikali awamu ya sita ilivyoiongezea mwendo sekta binafsi

SEKTA binafsi pana, nyeti na muhimu kwa maendeleo na ustawi wa taifa lolote duniani.

Ni injini ya maendeleo hasa kwa mataifa ambayo kisheria hayafanyi biashara kwa asilimia 100 lakini inapaswa kujenga mazingira wezeshi kwa watu wake na wawekezaji kufanya biashara kwa ubia kama ilivyo Tanzania.

Hata hivyo, mfumo wa sekta binafsi hauwezi kufanikiwa endapo hakutakuwa na sera nzuri, sheria na mfumo rasmi unaowatambua.

Chini ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan, sekta binafsi imeonesha kuridhishwa kwake na ushirikiano inaoupata. Katika Mkutano wa 13 wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC) uliofanyika Juni 7, mwaka huu (2022), Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Paul Makanza, alizungumzia kuridhishwa kwake na umakini wa serikali katika kutekeleza maazimio ya TBNC.

Makanza alisema serikali imeungana na sekta binafsi katika kujenga uchumi wa taifa. Alisema anavutiwa na mrejesho wa serikali katika uamuzi uliofanywa na Mkutano Mkuu wa 12 wa Baraza uliofanyika Juni 26, mwaka 2021, ikiwa ni wa kwanza kufanyika chini ya Uenyekiti wa Rais Samia.

“Hii inatupa imani kwamba serikali imedhamiria kweli kuondoa vikwazo vyote vinavyoelezwa. Ipo dhamira ya dhati ya kujenga uchumi wa taifa letu,” anasema.

Si kila Mtanzania anaelewa uzito wa kauli hii, lakini ukweli ni kwamba katika ufunguzi wa mkutano wa 12, Mwenyekiti wa TPSF, Angelina Ngalula, aliipongeza serikali kwa kazi nzuri zilizotekelezwa kukuza uchumi na kuinua maendeleo ya taifa, hasa juhudi binafsi za Rais Samia.

Angelina pia ni mjumbe wa TNBC na Mwenyekiti wa Kongani ya Usafirishaji na siku hiyo alisema: “Tunaipongeza serikali kwa kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji na ushirikishwaji wa sekta binafsi ambayo imekutana na kufanya majadiliano na rais, waziri mkuu, mawaziri, wabunge na watendaji wa serikali.

“Pamoja na mikakati ya kuendeleza sekta binafsi, majadiliano yetu yalielekezwa katika kukemea na kudhibiti rushwa katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasa eneo la kukadiria kodi na kufunguliwa akaunti za benki za wafanyabiashara zilizofungiwa na TRA jambo lililorudisha imani,” alisema Angelina.

Taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya mkutano wa 12 inatoa ushahidi wa kutosha kwa nini sekta binafsi ina imani na kauli, ahadi na vitendo vya serikali.

Mathalani, iliazimiwa kwamba mfumo wa majadiliano wa TNBC uwe sawa na wa majadiliano wa masuala ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar ili maazimio ya sekta binafsi na ya umma yatokane na maridhiano ya pande zote mbili.

Ambapo uboreshaji wa mfumo umefanywa na kugusa ngazi ya taifa, wizara, mikoa na wilaya. Sasa TNBC inaridhika kuhusu mfumo wa majadiliano (ulioibuka), ufanisi wa utekelezaji wa maazimio na mrejesho kati ya sekta ya umma na binafsi utaimarika.

Hata hivyo, pia iliazimiwa kuwa mfumo wa TNBC uwe jumuishi kwa kuongeza wadau zaidi; suala ambalo limetekelezwa kwa kuongeza idadi ya washiriki, hasa wafanyabiashara na wawekezaji. Vilevile iliazimiwa kwamba Ofisi ya Rais, Tamisemi, isimamie mikutano ya mikoa na wilaya ambapo Tamisemi kwa kushirikiana na Kamati ya Utendaji ya TNBC imetekeleza.

Mikutano imefanyika Tabora, Songwe, Simiyu, Shinyanga, Ruvuma, Pwani,Njombe, Mwanza, Mtwara, Morogoro, Mbeya, Mara, Manyara, Kigoma, Geita na Dar es Salaam.

“Mikoa ya Singida, Simiyu, Ruvuma, Rukwa, Njombe, Manyara na Iringa imepatiwa mafunzo kuhusu namna bora ya uendeshaji wa majadiliano yenye tija na ufanisi pamoja na kutoa mrejesho kuhusu utekelezaji wa maazimio,” inasomeka taarifa ya mrejesho.

Mengine yaliyoazimiwa na kutekelezwa ni kuwapo kwa mapitio ya sera, sheria, kanuni na taratibu ili kuainisha upungufu; ambapo Ofisi ya Waziri Mkuu imeelekeza wizara zote za kisekta kufanya mapitio, kuonesha upungufu na kupendekeza uboreshaji wa sera na sheria mbalimbali.

Mambo yaliyofanyiwa mapitio na uboreshaji ni Sheria ya Fedha ya 2021/22, Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya 1996, Sera ya Biashara ya 2003, Sera ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo ya 2003, Sheria ya Uvuvi ya 2003 na Mpango Mkakati wa miaka 15 wa kuendeleza uvuvi kuanzia mwaka 2021/2022.

Taasisi zote za umma zitekeleze majukumu na kutoa huduma bora kwa wafanyabiashara na wawekezaji kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi.

Ofisi ya Waziri Mkuu imezielekeza taasisi zote kufanya hivyo. Ofisi hiyo pia inafanya mikutano na taasisi zote za urekebu kuzielekeza namna bora ya kufanya kazi kwa weledi bila kuathiri biashara na uwekezaji wa sekta binafsi, ikihimizwa matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika taratibu na malipo.

Iliazimiwa yakamilishwe majadiliano kuhusu mikataba ya kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati na unganishi ya Mchuchuma, Liganga na Bandari ya Bagamoyo. Timu ya kitaifa ya majadiliano ya serikali tayari imeundwa na inajadiliana na wawekezaji.

Wizara ya Fedha na Mipango idhibiti ongezeko la kodi au tozo mpya. Wizara imetoa maelekezo kwa wizara nyingine na taasisi zote za umma, ikizitaka kutofanya marekebisho ya tozo bila kushauriana na wizara husika.

Kadhalika kuboreshwa mazingira ya biashara baina ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa kuondoa vikwazo au sheria, kanuni na taratibu zisizokuwa na tija katika kudumisha biashara na Muungano.

Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeboresha mazingira hayo ya biashara. Kwa upande wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Mifugo na sekta binafsi wajadiliane na kutoa mapendekezo kuhusu sheria, kanuni na taratibu ili kuondoa changamoto za mwingiliano kati ya maeneo tengefu ya utalii na ufugaji.

Wataalamu kutoka wizara hizo mbili walikutana Desemba 21, 2021 kwa ajili ya kupata uelewa na kutoa mapendekezo ya kutatua changamoto za kisheria, kanuni na taratibu zilizopo kuhusu maeneo yaliyohifadhiwa au tengefu kwa ajili ya utalii na ufugaji.

Hata hivyo, ilishauriwa ijengwe na kuimarisha miundombinu wezeshi inayounganisha Tanzania na majirani. Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi inaratibu tafiti kuhusu ujenzi wa miundombinu wezeshi ya kuunganisha Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kuchochea biashara kati ya nchi hizo mbili.

Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara na TNBC wamefanya tathmini ya mifumo ya ukaguzi wa mizigo, hususani magari, kabla na baada ya kusafirishwa. Tathmini hiyo ilithibitishwa na mkutano wa wadau Novemba 19, 2021.

Sekta binafsi pia imeshauriwa iunde mfumo wa kujitathmini na kufanya biashara na uwekezaji kwa weledi, uaminifu na nidhamu kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni na taratibu za nchi sawa na serikali inavyowajibika.

Taarifa ya mrejesho inaonesha kuwa sekta binafsi haijatekeleza azimio hilo. Mkutano huo pia ulitoa maazimio mengine ya kuyasukuma mbele maendeleo ya taifa.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/d72349e57ced08e8450d1a250dc999eb.jpg

UTAPIAMLO sugu au udumavu kwenye baadhi ...

foto
Mwandishi: Dunstan Mhilu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi