loader
Bodi Mikopo Serikali za Mitaa hatarini kufutwa

Bodi Mikopo Serikali za Mitaa hatarini kufutwa

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa amezitaka Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa, Taasisi ya Soko la Kariakoo na Shirika la Elimu Kibaha zijitafakari kiutendaji.

Alisema hayo jijini Dodoma wakati akifungua semina ya maofisa habari wa mikoa, halmashari na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo.

Alisema taasisi hizo tatu zinapaswa kujitahimini kiutendaji ili kuwa na tija na kwenda na wakati.

"Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa kwanza sijui wanafanya kazi gani. Nimeshamuagiza Katibu Mkuu (Profesa Riziki Shemdoe) ninataka ‘justification’ kwanini taasisi hii iendelee kuwapo,  kwa nini  tusiifute," alisema.

Bashungwa alimuagiza Katibu Mkuu kuhakikisha hadi mwisho wa mwezi huu anakuja na uchambuzi wa kina kama taasisi hiyo iendelee au la.

"Bodi ya Mikopo Serikali za Mitaa mnatoa mikopo kwa nani na kwa tija ipi. Kwenye hili Katibu Mkuu nakupa deadline (siku ya mwisho) hadi mwezi huu mwishoni nipate uchambuzi wa kwa nini  iendelee ku-exist (kuwapo)."

"Kama imeshindwa kutimiza wajibu wake tuangalie jukumu hili linaweza kufanywa na nani ili huduma muhimu kwa Watanzania ziendelee kutolewa lakini si kwa utaratibu ambao upo," alisema.

Kuhusu Shirika la Soko  Kariakoo, Bashungwa aliutaka uongozi wa shirika hilo kujipanga kuhakikisha linakwenda na uhalisia wa sasa.

"Lakini pia Shirika la Soko Kariakoo mjipange kuhakikisha malengo ya kuanzishwa kwake  katika  kuhudumua ndugu zetu wa Dar es Salaam, lakini mnaweza kwenda mbali zaidi mkaangalia uhalisia wa sasa. Maana sio lazima kuwa ambacho mlielekezwa kufanya kiendelee kuwa hicho chicho," alisema.

Kwa upande wa Shirika la Elimu Kibaha, alilitaka kuwa wabunifu na kwenda na wakati badala ya kung'ang'ana na madhumuni ya kuanzishwa kwake mwaka 1960.

 "Nilienda pale nilitoa maelekezo kwamba Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere alianzisha Shirika la Elimu Kibaha ili kusaidia nchi kupambana na maadui watatu ambao ni umasikini, maradhi na ujinga.”

"Wakati ule hakukuwa na shule za kata ambazo sasa kila kata kuna shule, lakini ukienda kwenye shirika wako kwenye mambo ya mwaka 1960 ya kujenga shule katika eneo moja,” alisema Bashungwa na kuongeza:

"Shirika wanapaswa kuwa wabunifu, mfano wana ekari 2,000 kwa nini wasiwashirikishe vijana wahitimu kushiriki kwenye green house (kilimo cha kitalu nyumba) au horticulture (kilimo cha bustani ya ndani), kwa kufanya hivyo tutatoa ajira na tutakuwa tumepambana na umasikini, Katibu Mkuu hili lisimamieni taasisi hizi zibadilike."

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/b3c7017d8cd184d9e0c50918e496c549.jpg

Tume Huru ya Uchaguzi na ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi