loader
Uvaaji holela miwani mtego hatari kwa macho

Uvaaji holela miwani mtego hatari kwa macho

MIWANI imekuwa bidhaa pendwa inayoakisi usasa, usomi katika jamii na kusababisha matatizo makubwa kiafya.

Wapo watu wanaovaa miwani hata kama hawana tatizo la macho wala kichwa kuuma, wanavaa kama urembo bila kujua ni hatari kwa afya zao.

Hii ni kutokana na kifaa tiba hicho kuuzwa sehemu nyingi bila taarifa za kiafya kuzingatiwa kwanza.

Muuzaji mmoja wa miwani eneo la Soko la Karume, Dar es Salaam, Jumbe Musa, anaiambia HabariLEO kuwa kwa siku anapata wateja watano hadi saba wanaohitaji bidhaa zake.

Anasema wakati wa kuchagua watu wengi wanaangalia ni jinsi gani watapendeza watakavyovaa miwani.

“Wengine wanaokuja wanasema wanataka miwani za urembo na wengine wanasema wanataka miwani za jua nauza zote hapa bei naanzia Sh 5,000 hadi 10,000,” anaeleza Musa.

Alipoulizwa kama anazingatia vyeti vya afya kabla ya kuuza, alisema: “Sijawahi kufanya hivyo, mimi nafanya biashara nataka niuze tu.”

Musa anasema haelewi kuhusu madhara ya kiafya yanayompata mtu anayevaa miwani bila vipimo.

WANAOUMWA MACHO KUNUNUA MTAANI

Consolata Kimathy ni miongoni mwa watu wanaotumia miwani kama kifaa tiba kutokana na tatizo la kutoona mbali. Anasema baba yake pia anatumia miwani kama tiba.

“Kuna siku alisafiri kutoka Iringa hadi Moshi lakini kwa bahati mbaya miwani yake ilivunjika sasa alipokuwa anatembea alikutana na machinga akamweleza shida yake ya miwani, yule muuzaji akampatia kama ile ile lakini hajashauriwa na mtaalamu.

“Sasa hivi mtaani ukitaka miwani unapata anakuuliza tu halafu anakutafutia lenzi na ukiangalia inafanana kabisa na zile tunazopewa hospitali,” anasema Kimathy.

Anashauri uuzaji wa miwani kiholela udhibitiwe pia kwa sababu ni kifaa tiba kinachoweza kuleta madhara.

“Kama hizi za matibabu mtu anaweza kupata tu barabarani, hatapata msukumo wa kwenda kumuona mtaalamu wa afya na pia nawashauri watu wasivae miwani hovyo,” anashauri Kimathy anayevaa miwani kama tiba.

HAYA HAPA MADHARA

Daktari Bingwa wa macho wa Hospitali ya Macho CCBRT, Dar es Salaam, Cyprian Ntomoka anaiambia HabariLEO kuwa watu wanaovaa miwani kiholela wako hatarini zaidi kupata magonjwa ya macho kwa sababu miwani huathiri mishipa ya macho.

Dk Ntomoka anasema kuwa athari kwenye mishipa ya macho husababisha uoni hafifu.

“Kuna watu huwa wanapenda kuvaa miwani bila hata kujua madhara yake, nataka niwaambie kuwa miwani yoyote utakayovaa ina madhara kwa afya ya macho kwa sehemu kubwa.

“Uvaaji holela wa miwani husababisha mishipa ya macho kuharibika na hii mara nyingi inasababisha uoni hafifu hapo ndio matatizo ya macho yanapoanza kwa baadhi ya watu,” anaeleza Dk Ntowoka.

Kwa mujibu wa Dk Ntowoka, asilimia 24 ya matatizo ya macho yanatokana na uoni hafifu baada ya mishipa ya macho kuathirika ambapo moja ya chanzo ni uvaaji holela wa miwani bila kushauriwa na wataalamu wa afya.

“Nawashauri watu kabla hawajavaa miwani wakapime afya ya macho ili daktari ampe miwani inayoendana na tatizo lake, uvaaji holela unaweza kuathiri zaidi macho,” anashauri.

MIWANI YA KUCHUJA MWANGA MUHIMU

Kwa mujibu wa Dk Ntomoka, si miwani tu ni hatari kwa macho ikitumiwa vibaya ametaja matumizi ya vifaa vyenye mwanga mkali pia.

Hii ni kwa sababu uteute unaolainisha macho unakauka, na endapo macho yakiwa makavu yanaweza kuwasha, kutoa machozi, kuumia na wakati mwingine kuwa mekundu.

“Hii tunaita ‘Computer Vision Syndroms’ ni mkusanyiko wa usumbufu ambao mtu anapata kutokana na matumizi ya vifaa vyenye mwanga mkali.

“Ni changamoto kubwa, tunapokea wagonjwa wengi wanaofanya kazi za kutumia kompyuta huwa wanakuja wakilalamika kuumwa macho. Ni muhimu watu wakajua kuwa matumizi ya muda mrefu ya kompyuta, simu na vifaa vingine vyenye mwanga mkali ni hatari kwa macho,” anabainisha Dk Ntomoka.

Anaeleza kuwa katika kliniki yake anawaona wagonjwa watano hadi 10 kwa siku, ambao wamepata madhara ya macho kutokana matumizi ya vitu vyenye mwanga mkali.

“Madhara yanaweza yasionekane kwa sasa ila baada ya miaka kadhaa utaanza kuumwa macho, katika kliniki yangu napata watu wengi wenye tatizo hilo, kila siku naona wagonjwa arobaini, kati yao watano hadi kumi wanakabiliwa na matatizo hayo,” anafafanua.

Dk Ntomoka anawataka watu kufuata ushauri wa matumizi sahihi ya vifaa vyenye mwanga kama kupunguza mwanga na kupumzisha macho kwa dakika 20 kila baada ya saa moja.

“Watu wapate ufahamu juu ya matumizi sahihi ya kompyuta ili wasipate matatizo ya macho, wafuate ushauri wa kutumia simu janja, kompyuta, TV, tableti na zingine kwa madaktari wa macho. Pia ni muhimu kuvaa miwani inayochuja kiasi cha mwanga au kupumzisha macho kwa kila baada ya dakika 20 hadi 30,” anashauri Dk Ntomoka.

Anasema watu wazima mara nyingi huugua macho kutokana na umri kuwa mkubwa au kusumbuliwa na maradhi.

USHAURI WA TMDA

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ndio yenye jukumu la kuhakikisha vifaa tiba vilivyoko nchini vinakuwa salama na kutumika vizuri.

Akizungumza na HabariLEO Kaimu Mkurugenzi wa Udhibiti wa Vifaa Tiba na Vitendanishi, Kissa Mwamwitwa anasema ni muhimu kwa watumiaji kufuata hatua zinazotakiwa.

“Kinachotakiwa kabla mtu hajavaa miwani kama anatatizo la macho amuone mtaalamu wa macho yeye anaweza kumshauri ni aina gani ya miwani aweze kuvaa.

“Lakini pia kama unahitaji kuvaa miwani hata kama huna tatizo ni vyema kumuona mtaalamu ili akupe taarifa sahihi hata unapoamua unajua kuwa hiki kitu kinaweza kunisababishia madhara, kutafuta elimu sahihi ni kitu muhimu,” anasema Mwamwitwa.

Anasema zipo miwani ambazo zinatumika kwa ajili ya mwanga mkali wa jua, kuona mbali, kuona karibu, kusoma, kutoona wakati wa giza na kichwa kuuma.
https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/162db382d8561a748302421702a71d9d.jpg

UTAPIAMLO sugu au udumavu kwenye baadhi ...

foto
Mwandishi: Aveline Kitomary

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi