loader
Sensa ni kwa maendeleo yetu, tusiache kuhesabiwa

Sensa ni kwa maendeleo yetu, tusiache kuhesabiwa

HAPA nchini Agosti 23 mwaka huu, kutafanyika tukio kubwa, la kihistoria na lililobeba mustakabali wa maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kiutamaduni kwa taifa.

Baada ya miaka 10, serikali itafanya Sensa ya Watu na Makazi ikiwa ni kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu Sura 351 kifungu kidogo cha 6(2)(a).

Sensa ya mwaka huu itakuwa ya sita kufanyika nchini baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa mwaka 1964. Sensa nyingine zilifanyika 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012.

Sensa ya mwaka huu inafanyika katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Umoja wa Mataifa wa kufanya Sensa kwa miaka ya 2020 unaoanzia 2015 hadi 2024 ambapo Tanzania ni mwanachama.

Katika kupata ushirikiano na wenye ufanisi kutoka kwa wadau wote Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali (OCGS) Zanzibar zimeandaa mkakati wa uelimishaji na uhamasishaji Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ili kuwashirikisha kikamilifu wananchi katika zoezi hilo la kitaifa.

Lengo kuu ni kuhakikisha wananchi wote wanaelewa umuhimu wa sensa ili watoe ushirikiano na kushiriki kikamilifu katika sensa. Kwa upande mwingine ni kuhakikisha viongozi wa kisiasa, kijamii na kiimani wanashiriki katika kuelimisha na kuhamasisha umma kushiriki katika sensa.

Maana ya Sensa ya Watu na Makazi

Sensa ya Watu na Makazi ni utaratibu mzima wa kukusanya, kuchakata, kuchambua na kusambaza taarifa za kidemografia, kiuchumi, mazingira na jamii za watu wote na makazi yao katika nchi katika kipindi maalumu.

Kwa maana nyingine sensa ni zoezi la kupata idadi ya watu wote nchini, kwa umri na jinsi mahali wanapoishi, viwango vyao vya elimu, hali ya ajira, hali ya vizazi na vifo, hali ya makazi na taarifa nyingine nyingi muhimu.

Kuwa na takwimu sahihi kuhusiana na watu ambazo zimechambuliwa na kuainishwa kwa makundi, ukubwa na mtawanyiko wa watu na makazi ni muhimu katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Takwimu hizi ndizo zinazoweza kuainisha mahitaji halisi ya wananchi yakiwemo ya makundi yenye uhitaji maalumu kwa mfano watu wenye ulemavu, watoto, wanawake, vijana na wazee, kwa kipindi cha sasa na kijacho hivyo hurahisisha uandaaji wa sera na mipango ya maendeleo kulingana na mahitaji na mazingira yaliyopo.

Sensa za Watu na Makazi ambazo hufanyika katika nchi zote ulimwenguni hutekelezwa kwa kufuata kanuni na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, utaratibu unaofuatwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, Tanzania ikiwa mojawapo ni kufanya sensa kila baada ya miaka 10.

Zoezi la sensa hufanyika kwa kutumia karani wa sensa kwenye eneo la kijiografia ili kuhesabu kaya na watu wote waliolala kwenye kaya husika usiku wa kuamkia siku ya sensa pamoja na kuchukua taarifa zao kulingana na maswali yaliyomo kwenye dodoso la sensa.

Sensa na Maendeleo

Mipango ya maendeleo ya nchi tangu uhuru imekuwa ikijikita katika kumkomboa Mtanzania kutokana na maadui wakuu watatu kama alivyobainisha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere ambayo ni ujinga, umasikini na maradhi.

Kwa msingi huo dhumuni kuu la sensa ya mwaka 2022, ni kukusanya takwimu sahihi ziweze kutumika kupima kiwango cha maendeleo kilichofikiwa katika kupambana na maadui hao watatu pamoja na kuandaa miongozo itakayotumika katika kutayarisha mipango ya maendeleo endelevu ya muda mfupi, wa kati na mrefu.

Takwimu zitakazokusanywa zitatumika katika kutunga sera za kiuchumi, kijamii na mazingira na zitatumika pia kutathmini ubora wa hali ya maisha ya watu kwa ujumla kwani serikali inatambua kuwa ni vigumu kupata maendeleo endelevu bila kuwa na takwimu sahihi na za kuaminika kuhusu watu na makazi.

Umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi 2022

Lengo la Sensa ni kupata takwimu za msingi za watu na hali za makazi ambazo zitasaidia kutunga sera, kupanga na kufuatilia mipango ya maendeleo ya kimkakati inayolenga kukuza ustawi wa nchi na watu wake.

Matokeo ya sensa yatasaidia serikali kutathmini utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa 2016/2017 hadi 2020/22, Mpango wa Pili wa Kukuza Uchumi Zanzibar (MKUZA 2) kupata takwimu za msingi kwa ajili ya kupima utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo 2021/22 hadi 2025/26.

Pia kutathmini Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025, Dira ya Maendeleo Zanzibar ya mwaka 2050 pamoja na kupata takwimu za msingi za kufanya maandalizi ya dira nyingine ya taifa ambayo mchakato wake unaendelea ndani ya serikali.

Kwa muktadha huo hapo juu ni wajibu wa kila Mtanzania kushiriki na kutimiza wajibu wake kufanikisha zoezi hilo la kitaifa ili kupata taarifa na takwimu sahihi kwa maendeleo ya nchi na watu wake kwa msingi wa ugawaji wa rasilimali ya taifa kwa kila eneo la utawala hapa nchini.

Rais Samia Suluhu Hassan wakati akizindua rasmi Nembo ya Sensa ya Watu na Makazi Aprili 08, mwaka huu mjini Zanzibar na kutangaza sensa itafanyika siku ya Jumanne Agosti 23, mwaka huu, aliwahimiza Watanzania kujitokeza siku hiyo kushiriki tukio hilo adhimu kwa nchi ili kuwezesha taifa kupata taarifa na takwimu sahihi zitakazosaidia serikali kupanga mipango ya maendeleo kiuchumi na kijamii.

Kutokana na umuhimu wa sensa kwa taifa, Rais Samia anazihimiza taasisi za serikali na binafsi kutumia nembo ya sensa katika shughuli zote za kiserikali na za sekta binafsi ili kuitangaza hadi itakapokamilika.

Ili kukamilisha sensa, ni muhimu watu wote watakaolala katika kaya binafsi usiku wa kuamkia siku ya sensa na wote watakaokuwa katika kaya za jumuiya zikiwemo hoteli, nyumba za kulala wageni, hospitalini, magereza, mabweni ya wanafunzi, kambi za kijeshi, vituo vya kulelea watu wenye mahitaji maalumu wakiwemo yatima na wazee, kambi za wavuvi na watu wasio na makazi maalumu, kuhesabiwa.

Vituo vya usafiri wa umma vikiwemo vituo vya mabasi, garimoshi, viwanja vya ndege na bandari navyo ni eneo jingine ambalo litahusisha sensa. Katika maeneo hayo, watu watahesabiwa kwa utaratibu maalumu utakaoandaliwa na Kamati za Sensa katika ngazi za mitaa, kitongoji na Shehia.

 

Kamisaa wa Sensa nchini na Spika mstaafu, Anne Makinda, anasema sensa ni muhimu kwa nchi, suala la rushwa halina nafasi katika kukamilisha zoezi hilo, hivyo ni kosa kisheria kuwaomba fedha makarani ambao watafanya kazi hiyo.

"Ni marufuku kutoa pesa, kisa kazi ya ukarani, acheni tabia hiyo na nyie waombaji msishawishike kutoa pesa kwa mtu yeyote kwa kuwa maombi hayo yanakwenda kitehama na hakuna gharama yoyote," anasema Makinda.

Makinda anawahimiza watumishi wa umma wazungumzie kufanikisha sensa ya mwaka huu na maofisa habari ndiyo wataalamu wa habari, watumie nafasi yao kusaidia kuhamasisha wananchi kupitia mitandao ya kijamii kutoa elimu hiyo kwa kuwa wanaosoma zaidi mitandao ni vijana.

Ewe Mtanzania, jiandae, kuhesabiwa, jitokeze ili taifa litapate takwimu sahihi kwa maendeleo. Mimi nipo tayari kuhesabiwa Agosti 23, 2022, wewe je?

 

 

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/369fd248ebfd3b5586f10563094d6ebe.jpg

UTAPIAMLO sugu au udumavu kwenye baadhi ...

foto
Mwandishi: Rahel Pallangyo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi