loader
Bashungwa aishukuru Asas  ujenzi Zahanati ya Kising'a

Bashungwa aishukuru Asas ujenzi Zahanati ya Kising'a

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI,  Innocent Bashungwa ameishukuru kampuni ya Asas Group kwa kutatua changamoto ya wodi ya wanawake na wanaume katika Zahanati ya Kising'a,  wilayani Iringa.

Kampuni hiyo imetumia zaidi ya Sh Milioni 150 kwa ajili ya ujenzi wa wodi hiyo yenye uwezo wa kulaza wagonjwa 20 kwa mara moja pamoja na ukarabati wa jengo la kutolea huduma ya wagonjwa wa nje (OPD).

Mmoja wa wakurugenzi wa kampuni hiyo,  Ahamed Asas alisema wametoa mchango huo kama wadau wanaotambua na kuthamini mazingira bora ya utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.

”Sisi ni wadau wa maendeleo na katika kata hii ya Kising'a ndiko kwenye mashamba yetu ya ng'ombe. Kwa hiyo sisi ni sehemu ya Kising'a,  na ni sehemu ya maendeleo yake," alisema.

Alisema wataendelea kushirikiana na serikali na wananchi kwa kadri watakavyopata fursa, ili kuhakikisha huduma za afya na nyingine muhimu zinaendelea kuimarika.

Katika ziara yake aliyofanya leo wilayani Iringa,  Bashungwa aliipongeza kampuni hiyo kwa ujenzi wa wodi hiyo uliozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan mwaka 2018, wakati huo akiwa Makamu wa Rais akisema umeifanya zanahati hiyo ipige hatua muhimu kuelekea kituo cha afya.

Ombi la kuifanya zanahati hiyo iwe kituo cha afya lilitolewa na Mbunge wa Jimbo la Isimani ilipo zanahati hiyo,  William Lukuvi.

"Katika mipango yetu ya kata,  tuliamua Zahanati ya Kising'a ndiyo iwe Kituo cha Afya cha kata hii ya Kising'a. Tunajua tumechelewa ombi hili kulileta katika bajeti ya serikali iliyoanza mwezi huu wa Julai, lakini tuna imani bajeti ijayo inaweza kuingizwa,” Lukuvi alisema.

 

Bashungwa aliitaka halmashauri ya wilaya ya Iringa kuanzisha mara moja mipango ya kuongeza jengo la upasuaji,  maabara na maiti katika zahanati hiyo, ambavyo ni vigezo muhimu vya kuifanya iwe kituo cha afya.

 

”Serikali tunalichukua ombi hili na tunataka liwe kipaumbele cha halmashauri. Julai 2023 ambao ni mwaka wa fedha ujao, tuanze kuipanua iwe kituo cha afya," alisema.

 

Katika ziara hiyo Bashungwa ametembelea pia shule ya sekondari Isimani na kuiagiza halmashauri ya wilaya ya Iringa kutumia Sh Milioni 70 za mapato yake ya ndani kujenga jengo la utawala na maabara katika shule hiyo.

Aidha ametembelea kituo cha Afya Kising'a alikoahidi kuongeza Sh Milioni 100, kwa ajili ya ukarabati wake,  shule ya sekondari Nyang'oro inayokabiliwa na changamoto kubwa ya maji, shule ya sekondari Izazi na kituo cha afya Migoli.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/0d18c62c1879971aa12b99ff1b4b8c0a.jpg

Tume Huru ya Uchaguzi na ...

foto
Mwandishi: Frank Leonard, Iringa

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi