loader
Shaka: Katiba inahitaji muda wa kutosha

Shaka: Katiba inahitaji muda wa kutosha

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Shaka Hamdu Shaka amesema chama hicho hakioni udharura wa kuharakisha mchakato wa Katiba Mpya au mabadiliko kwa kuwa suala hilo linahitaji muda wa kutosha na ushirikishwaji wa wananchi.

Shaka aliyasema hayo alipotembelea Makao Makuu ya Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Tazara wilayani Temeke mkoani Dar es Salaam jana, kujionea shughuli mbalimbali za uchapaji akiwa katika ziara yake kwa baadhi ya vyombo vya habari mkoani humo.

Alisema hoja mabadiliko ya Katiba kwa CCM si hoja ngeni, haikuanza leo wala si mara ya kwanza Katiba ya Tanzania kufanyiwa mabadiliko kwani imeshafanyiwa marekebisho mara 14 tangu nchi ilipopata uhuru.

“Hoja hiyo siyo ngeni wala haikuanza leo, tulichosema na tunachosisitiza hatukatai kuwa na Katiba ama ni mabadiliko kama tunaandika upya au tunabadilisha, hatukatai! Lakini tunachosimamia CCM ni kwamba hakuna udharura wa kufikia ama kupatikana kwa hiyo Katiba mpya, ni lazima wananchi ama Watanzania wenyewe ambao ndiyo wadau wakuu wa hiyo Katiba kwanza washirikishwe, pili waelimishwe na pia wajue Katiba wanayoitaka ni Katiba ya aina gani,” alisema Shaka.

Alisema Katiba inayotakiwa kupatikana ni katiba ya wananchi na si wanasiasa kwa sababu wao wamebeba ajenda zao tofauti hivyo suala la Katiba si la kuharakishwa kwa msukumo wa wanasiasa, bali kwa ushirikishwaji kwa maslahi ya nchi na wananchi kama ilivyofanyika katika Bunge la Katiba ambalo liliandaa katiba pendekezwa.

“Kwa sababu Katiba pendekezwa ipo, sasa itategemea na namna ambavyo mazingira yatawekwa katika utekelezaji, lakini kauli yangu ni hakuna jambo la dharura kwenye kupata Katiba, tunahitaji muda wa kutosha ili sasa tukifanya kesho na keshokutwa tusirudie huko,” alisema Shaka.

Maridhiano

Kuhusu hali ya siasa za ndani, Shaka alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha dhamira ya dhati ya kuwaweka Watanzania pamoja na kuvunja siasa za chuki kwani hilo ni jambo la kizalendo linalohitaji ujasiri wa hali ya juu kulitekeleza.

Alisema kitendo cha Rais kuamka na kuwaita viongozi wa vyama vya upinzani ili wafanye majadiliano ya kidemokrasia na kujua tatizo na tofauti ziko wapi, ni kuonesha ukomavu wa kisiasa na nia njema kwa mustakabali wa nchi kwa kuwa kimesaidia kujenga siasa za kirafiki badala ya siasa za chuki na uhasama.

“Tumekuwa tukishiriki pamoja, tumekuwa tukipanga pamoja na hiyo ndiyo dira ya huko mbele tunakokwenda, siasa siyo ugomvi, siasa siyo uhasama wala siasa siyo chuki, bali siasa itumike kama chachu ya kuliunganisha taifa letu na hiyo ndiyo dhamira ya Mheshimiwa Rais,” alieleza Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM.

Alisema pia kuwa Rais ameweka utaratibu wa kukutana na viongozi wa vyama vya siasa na utaratibu huo utawagusa viongozi wa vyama vyote bila kujali kama kikubwa au kidogo kwa sababu katika utekelezaji vyama vyote vya siasa vina wajibu wa kupewa heshima.

Uchaguzi CCM

Alipozungumzia uchaguzi wa chama hicho, Shaka alisema unakwenda vizuri kwa asilimia 95 ingawa zipo changamoto chache ambazo chama kimezifanyia kazi kupitia kanuni zilizowekwa kama msingi wa uendeshwaji wa uchaguzi ndani ya chama.

Alisema chama kimeweka kanuni za maadili ambazo zimekuwa mwongozo unaokiwezesha kupata viongozi bora wenye maadili ikiwa ni pamoja na kuziba mianya ya rushwa katika mchakato wa uchaguzi.

Alisema chama kimeshakamilisha uchaguzi ngazi za chini (Shina, Tawi na Kata) na kinaenda katika uchaguzi wa Mikoa na Taifa na tayari fomu za kuwania nafasi zimeshatolewa na wanatarajia kufunga kazi ya kuchukua fomu Julai 10, mwaka huu.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/36a79655d73b5e538baf87d702bab49c.JPG

Tume Huru ya Uchaguzi na ...

foto
Mwandishi: Anna Mwikola

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi