loader
Samia haridhishwi na TPA, amng’oa bosi baada ya miezi 15

Samia haridhishwi na TPA, amng’oa bosi baada ya miezi 15

RAIS Samia Suluhu Hassan ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Eric Hamissi baada ya miezi 15 tangu alipomteua Aprili 4, mwaka jana.

Aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu TPA.

Mbossa ni mtaalamu wa Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na katika kazi amekulia katika utendaji wa kazi bandarini na kumpa uzoefu wa masuala ya bandari hali iliyomjenga kama mtumishi mwenye weledi na nidhamu ya kazi.

Awali akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha nne kutoka Tabora hadi Isaka katika hafla iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam jana, Rais Samia alisema haridhishwi na utendaji wa bandari nchini.

Alisema malengo ya serikali ni kuifanya Bandari ya Dar es Salaam kutoa nusu ya bajeti ya nchi kwa kuifanya kuwa kivutio cha wawekezaji, wafanyabiashara na mataifa mbalimbali kuitumia, hali itakayoiletea nchi fedha nyingi zitakazoiwezesha serikali kutekeleza miradi.

Rais Samia aliwataka waliopewa mamlaka ya kuendesha na kuisimamia Bandari ya Tanzania wafanye kazi kwa bidii ili kufikia malengo ambayo nchi imejiwekea.

Alisema Bandari ya Dar es Salaam ndio jicho la Tanzania ndio maana serikali imejizatiti kuweka fedha nyingi kukarabati bandari zote nchini kuhakikisha kuwa kwa pamoja bandari zinazalisha nusu ya fedha za bajeti ya nchi.

Rais Samia alisema tangu alivyochukua hatamu ya kuiongoza Tanzania, alidhamiria kuendeleza bandari pamoja na miradi yote ya kimkakati, lakini hakujua kuwa fedha za miradi hiyo mikubwa katika nchi angezipata wapi na kuongeza kuwa ni kwa kudra za Mwenyezi Mungu kumwezesha kupata fedha hizo.

Aidha, alimuagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali azipitie sheria za ununuzi na taratibu zinazosimamia Ushirikiano wa Sekta Binafsi na Sekta ya Umma (PPP) ili kuondoa urasimu katika utendaji kwa kigezo cha kubanwa na sheria.

“Sheria hizi badala ya kupiga hatua ya kwenda mbele kimaendeleo inaturudisha nyuma, tukiendelea na mambo ya kujali siasa tutawapoteza wawekezaji kwa kuwa mwekezaji akiona anahangaishwa huku akiwa na fedha zake mkononi atakwenda mahali pengine,” alisema Rais Samia.

Aliiagiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ihakikishe wakandarasi wanajenga miradi yenye thamani sawa na fedha inayotolewa ili kuifanya kudumu kwa muda unaotakiwa na kuwafanya Watanzania waitumie kupata ustawi wa maisha yao.

“Wito wangu kwa sekta binafsi ijipange vizuri ili iweze kufaidi fursa zinazotokana na soko kubwa linaloletwa na miradi hususani katika bidhaa za ndani kwani jukumu la serikali ni kuweka mazingira mazuri ili mambo yaende vizuri,” alisema Rais Samia.

Alisema serikali imeagiza vichwa vipya 17 vya treni lakini wakati ikisubiri mchakato ya kutengenezwa kwake, imeagiza vichwa vingine vilivyotumika ili kuhakikisha kuwa mradi unaanza rasmi na Watanzania wanaanza kufaidi miradi yao.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/e50410e378ab1ad9ef9f214cf0011cf7.jpg

Tume Huru ya Uchaguzi na ...

foto
Mwandishi: Selemani Nzaro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi