loader
Maombi mawakili Zanzibar  kufanya kazi Bara kutafutiwa ufumbuzi

Maombi mawakili Zanzibar kufanya kazi Bara kutafutiwa ufumbuzi

JAJI Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amesema watafanya mazungumzo na  Baraza la sheria nchini ili kuona namna ya kuwaruhusu mawakili na wahitimu wa Shule ya sheria Zanzibar  kufanya kazi za sheria Tanzania bara.

Kuna sharti la sheria kwa mawakili kutoka nje ya Tanzania bara  kwamba ni lazima awe amefanya kazi miaka mitano kabla ya kuruhusiwa kufanya kazi nchini jambo ambalo,  limetajwa kuwavunja moyo wanafunzi wa sheria.

Profesa Juma ameyasema hayo leo Dar es Salaam baada ya Jaji mstaafu Mbarouk Salim Mbarouk ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Skuli ya Sheria Zanzibar kumuomba  awasaidie katika suala hilo ambalo huulizwa na wanafunzi wa sheria pamoja na wadau mbalimbali wa sheria.

Amesema suala la mawakili wa Zanzibar  kufanya kazi Tanzania bara sio jambo baya kwani ni njia mojawapo ya kuwajengea uwezo pindi watakapokutana na changamoto mbalimbali za kisheria ambazo zitawafanya wawe wazuri.

 "Maombi yenu  nimeyapokea ikiwemo la mawakili na wanasheria wa Zanzibar kuja kufanya kazi Bara sio jambo baya kwani kama mawakili wa nje ya nchi wanaruhusiwa kufanya kazi hapa hakuna tatizo, nitakaa na wenzangu pamoja na baraza la sheria nchini kuliangalia hili," amesema Jaji Profesa Juma.

Hata hivyo, ameutaka uongozi wa shule hiyo ya sheria kuwajenga uwezo wanafunzi hao  kwa kuwapa mafunzo ya ziada nje ya taaluma yao ikiwemo masomo ya biashara ili watakapokosa  kazi wawe na cha kufanya.

Pia amewataka wanafunzi hao wajengewe uwezo katika masuala ya sayansi na teknolojia kwa kuwa hali ya ajira kwa sasa sio nzuri na hata ikiwezekana wafuate ujuzi nje ya nchi.

 

Kwa upande wake, Jaji  Mbarouk

amesema kuwa skuli hiyo imefanikiwa kutayarisha Mtaala na mpango kazi wa miaka mitano kupitia msaada wa fedha kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Amesema shule hiyo imeanzishwa kwa sheria namba 13 ya 2019 na kazi zake zilianza rasmi 2021 baada ya uteuzi wa Mkuu wa skuli hiyo na baraza la skuli.

"Hivi sasa lipo sharti kwamba wakili kutoka nje ya Tanzania Bara lazima awe amefanya kazi miaka mitano kabla ya kuruhusiwa kufanya kazi, sharti hili limekuwa likiwavunja moyo wanafunzi waliopo skuli na wanaotarajia kujiunga katika miaka ya baadaye tunaomba uongozi wa mahakama uone namna ya kusaidia katika hili," amesema Jaji Mbarouk.

Amesisitiza kuwa tayari skuli hiyo imeingizwa katika bajeti ya serikali ya mwaka 2022/23 hivyo, wametayarisha kanuni za taaluma na nidhamu, muundo wa taasisi na muundo wa utumishi.

Ameeleza kuwa wamefanya usaili kwa waombaji 91, waliokubaliwa ni 56 na waliosajiliwa ni 21 ambao wanaendelea na masomo na sehemu kubwa ya wakufunzi wao ni majaji wa Mahakama Kuu Zanzibar na mawakili wazoefu.

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/be729885002bef8de4750705653bb02e.jpg

Tume Huru ya Uchaguzi na ...

foto
Mwandishi:  Francisca Emmanuel

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi