loader
Uwanda mpana wa Kiswahili sababu UNESCO kukipaisha

Uwanda mpana wa Kiswahili sababu UNESCO kukipaisha

KATIKA kufikia maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa, lugha ni nyenzo muhimu ya kuwaunganisha watu kufikia azma hiyo kwa kurahisisha mawasiliano kati yao.

Pasipo kuwapo lugha inayofahamika na kutumiwa na watu wengi au wote katika jamii au nchi husika, suala la maendeleo, umoja na mshikamano linaweza lisifikiwe kwa urahisi kwa kuwa hakuna kitu kinachoiunganisha jamii au nchi husika.

Wakati dunia inaadhimisha Siku ya Kiswahili leo, Tanzania na nchi nyingi za Afrika zina kila sababu ya kukienzi kwa namna yake kutokana na mchango wake katika maendeleo yao hasa harakati za uhuru.

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwa kushirikiana na viongozi wenzake wa Chama cha TANU, walifanikiwa kuwaunganisha Watanganyika kupigania uhuru wao kwa amani na baadaye kwa kushirikiana na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Shehe Abeid Amani Karume, wakawaunganisha Watanganyika na Wazanzibari kuwa Taifa moja la Tanzania.

Hayo yote yalifanyika kutokana na kuwapo kwa Kiswahili, lugha iliyofahamika na kufahamika na makabila takribani yote Tanzania ambayo sasa ni zaidi ya 120 hivyo ujumbe wa kupigania uhuru na kuunda Muungano, zikiwa rahisi kwa kuwa wananchi waliwaelewa viongozi wao vizuri.

Sambamba hilo, baada ya Uhuru wa Tanganyika na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Kiswahili kilitangazwa kuwa Lugha ya Taifa na ndivyo kilivyo mpaka sasa kikiendelea kuwaunganisha Watanzania kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Kiswahili pia ilikuwa ni lugha ya ukombozi Kusini mwa Afrika huku kiungo kikuu cha harakati ikiwa ni Tanzania.

Wapigania uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika zikiwamo Angola, Namibia, Msumbiji na nyinginezo, ziliendesha harakati zao za ukombozi kutokea Tanzania ambako wapigania uhuru walilazimika kujifunza Kiswahili na walikifahamu vyema.

Nchi kama Msumbiji, Afrika Kusini, Namibia na Zimbabwe haziwezi kuficha hisia zao kuhusu mchango wa Kiswahili katika ukombozi wao.

Kwa Afrika Mashariki karibu nchi zote hazikwepi ukweli kuwa Kiswahili kimewasaidia katika mengi ikiwamo uhuru wao.

Ili kutoa huduma za jamii zikiwamo elimu, afya, maji safi na salama na huduma nyingine mbalimbali nchini, Kiswahili kilirahisisha kazi hiyo na bado kinaendelea kurahisisha kwa kuwa bajeti za miradi hiyo huandikwa kwa Lugha ya Kiswahili inayoeleweka na Watanzania wote.

Kwa kuonesha umwamba wake, Lugha ya Kiswahili ndiyo lugha ya kufundishia na kujifunzia katika elimu ya awali na msingi zilizo chini ya serikali nchini.

Mahakamani mashauri sasa yanaendeshwa kwa Kiswahili na sheria zinatafsiriwa kwa lugha hii adhimu kumsaidia Mtanzania kuelewa.

Kiimani, Kiswahili kilitumika nyakati za ukoloni katika kueneza dini za madhehebu ya Kikristo na Kiislamu na kinaendelea kutumika mpaka sasa katika ibada za madhehebu mbalimbali ya dini nchini.

Licha ya kuwa na makabila zaidi ya 120, Watanzania wanajisikia ndugu na wamoja kutokana na Kiswahili ambacho kinazungumzwa nchi nzima na kila mahali jambo linalowafanya wajisikie huru kuishi mahali popote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila kuulizana makabila yao tofauti na baadhi ya nchi za Afrika ambazo watu hutambuana kwa makabila yao.

Baada ya kufanya vizuri nchini kwa kuwaunganisha Watanzania kiuchumi, kisiasa na kijamii, Kiswahili kimevuka mipaka hadi katika nchi mbalimbali zikiwamo za Jumuiya ya Maendeleo ya Uchumi Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Umoja wa Afrika (AU).

Katika jumuiya hizo, Kiswahili kinatambulika kuwa miongoni mwa lugha rasmi za mawasiliano katika kutekeleza majukumu ya kuwaunganisha watu kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Hili ni jambo la kujivunia kuona lugha ya Watanzania iliyotumika kabla na baada ya uhuru katika kuwaunganisha katika mambo mbalimbali, sasa inavuka mipaka kwenda katika nchi mbalimbali duniani na kuvutia wengi kujifunza lugha hiyo.

Kupanuka kwa Kiswahili pia kunatoa fursa ya ajira kwa wataalamu wa Kiswahili hapa nchini.

Wataalamu wa Kiswahili wa Tanzania wana fursa ya kufundisha Kiswahili kwa wageni wakiwa nchini au fursa ya kufundisha Kiswahili katika nchi nyingine za Afrika, Ulaya, Amerika na Asia.

Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) linaeleza kuwa mpaka sasa katika kanzidata kuna wataalamu wa Kiswahili walioandikishwa wakiwamo walimu, wakalimani na watafsiri zaidi ya 1,300 tayari kutumika nje ya nchi kuendeleza Kiswahili.

Hili ni jambo kubwa na fursa muhimu ambayo Kiswahili inawapatia Watanzania kama zawadi kwa kukithamini, kukikuza na kukiendeleza kutoka kizazi hadi kizazi.

Haikuwa rahisi kukifanya Kiswahili kufikia hadhi iliyonayo sasa kitaifa na kimataifa kama Watanzania wasingekipa nafasi muhimu ya kuwajenga katika misingi ya umoja na mshikamano.

Unesco yakipa siku

Kazi iliyofanya Kiswahili si ndogo, na hii ndio sababu Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kukipa siku maalumu duniani Julai 7 kila mwaka.

Tangazo hilo lilitolewa Jumanne, Novemba 23, mwaka jana katika makao makuu ya shirika hilo jijini Paris, Ufaransa wakati wa mkutano wa nchi wanachama wa shirika hilo.

Kwa mujibu wa taarifa za Unesco, azimio maalumu la kuitangaza siku hiyo limepitishwa na wanachama wote bila kupingwa.

Hatua hiyo inakifanya Kiswahili kinachozungumzwa na takriban watu milioni 200 duniani (kwa mujibu wa Bakita) kuwa lugha ya kwanza ya Kiafrika kutambuliwa na Umoja wa Mataifa na kuwa na siku maalumu ya kuadhimishwa.

Hivyo, leo dunia inapoadhimisha Siku ya Kiswahili, ni vyema Watanzania na dunia kutambua mchango wa lugha hiyo katika kuwaletea watu maendeleo kiuchumi, kisiasa, kijamii na kuwaunganisha kuwa wamoja na wenye mshikamano.

Matamanio ya Watanzania na wapenda maendeleo ni kuona lugha hii inakuwa kiungo kikubwa kwa Afrika na duniani kote.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/0d67a6e59ea8cbb4fa59ba71f91835bf.jpg

UTAPIAMLO sugu au udumavu kwenye baadhi ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi