loader
HabariLEO ilivyokuza Kiswahili EAC

HabariLEO ilivyokuza Kiswahili EAC

MOJA ya nyenzo kuu muhimu ya kukuza Lugha ya Kiswahili nchini na nje ya nchi ni vyombo vya habari kama magazeti, redio, runinga na vya mitandaoni hususani vinavyotoa taarifa kwa lugha fasaha ya Kiswahili.

Vyombo hivi endapo vitatoa taarifa zake kwa kutumia lugha fasaha ya Kiswahili, jamii itajifunza kwa kiwango kikubwa matumizi sahihi ya lugha kupitia habari, makala, picha, video na vipindi mbalimbali.

Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN Ltd) inayochapisha magazeti ya Daily News, Sunday News, HabariLEO, HabariLEO Jumapili na SpotiLEO iliona umuhimu wa kukuza lugha hii na kuamua miaka kadhaa iliyopita kuwa na Toleo Maalumu la Gazeti la HabariLEO Afrika Mashariki.

Lengo likiwa kuiuza bidhaa ya Kiswahili ndani na nje ya nchi, lakini pia kutumia lugha hii kufundishia mataifa mengine kutokana na lugha hii kuandikwa na kuzungumzwa kwa ufasaha zaidi hapa nchini ukilinganisha na mataifa mengine.

Mkurugenzi Mtendaji wa TSN Ltd, inayochapisha magazeti hayo, Tuma Abdallah anasema kuwa uanzishwaji wa gazeti hili ulilenga kuwafikia wazungumzaji wa Lugha ya Kiswahili kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) liwe Gazeti la Kitaifa la Serikali.

Juhudi hizo zimesaidia kuisambaza lugha hiyo hapa nchini na nje ya mipaka ili kukikuza na kukifanya kuwa moja ya lugha maarufu duniani.

“Juhudi hizi zimekwenda na sasa katika kuangalia kama chombo cha Habari, tulianza na Afrika Mashariki ambapo tuliona tuanzishe Toleo Maalumu la Afrika Mashariki ambalo litakuwa na habari zinazohusu Afrika Mashariki na lengo ni kuzifanya nchi za Afrika Mashariki zipende kusoma na kuzungumza Kiswahili kama bidhaa mojawapo, lakini vilevile katika kupata taarifa zao zinazowahusu,” anasema Tuma.

Anaongeza, “Katika kuhakikisha tunakwenda katika soko la Afrika Mashariki, tulianza na Rwanda, ambako tulienda tukafanya vikao kule tukalitambulisha gazeti letu, tukakutana na viongozi mbalimbali tukatafuta namna ambavyo gazeti letu lingeweza kufika kule na kulisambaza na tukapata taasisi moja ya ‘New Times’ ya nchini humo na kuingia nayo makubaliano ya ushirikiano.”

Ili kuhakikisha Lugha ya Kiswahili inapelekwa katika mataifa mbalimbali kupitia gazeti la HabariLEO, limekuwa likiandaa makala maalumu za Kiswahili kwa kushirikiana na Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) zinazotoka katika gazeti hili kila Ijumaa.

Hatua hii imesaidia wengi hasa wageni na wanataaluma mbalimbali kwa kuwa ni ukweli ulio wazi kuwa ni Tanzania pekee inayoandika na kukizungumza vema Kiswahili ukilinganisha na mataifa mengine.

“Kwa Afrika Mashariki ndiyo, lakini pia tunataka kwenda zaidi katika nchi za SADC (Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika) tunataka kwenda na nchi nyingine za Afrika,” anafafanua Tuma.

“Kwa mfano, tumeambiwa Misri kuna chuo ambacho kina Idara ya Kiswahili tunataka twende tukaongee nao tuone namna gani tunaweza tukawa tunasambaza gazeti letu ili walitumie kwa ajili ya kujifunzia lugha,” anaongeza.

“Rwanda tulipokwenda gazeti lilipokelewa vizuri na kule kuna Jumuiya kubwa ya wazungumzaji wa Kiswahili, kuna eneo ambalo kuna waswahili watupu, kwa hiyo lilipokelewa vizuri tatizo ambalo tulipata ni jinsi ya usambazaji wa hili gazeti kule. Mtu ambaye tulikuwa tumemkabidhi alishindwa kudhibiti usambazaji wake, lakini tunaamini tukipata mtu mwaminifu wa kutuuzia gazeti letu kule kuna soko kubwa,” anabainisha Mkurugenzi Mtendaji wa TSN Ltd.

Kutokana na mwitikio mkubwa wa baadhi ya nchi za SADC kutaka kuanzisha programu ya kufundisha Lugha ya Kiswahili katika shule zao mbalimbali, HabariLEO litaendelea kuwa na mchango katika kukuza lugha hii kwa maana litatumika kama nyenzo ya kufundishia Lugha ya Kiswahili katika maeneo hayo.

“Kwa hiyo tutakuwa na maudhui maalumu kwa ajili ya wanafunzi na watu ambao wanajifunza Kiswahili ili wakisoma gazeti iwe ni kama nyenzo ya kujifunzia lugha hii,” anaeleza Tuma.

Katika ujumbe wake wa hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Audrey Azoulay alisema Lugha ya Kiswahili ni moja ya lugha zinazoshamiri na kuvuka mipaka ya kule inakozungumzwa, ambako ina wazungumzaji kati ya milioni 120 hadi 150 (Baraza la Kiswahili Tanzania –BAKITA linaeleza kuwa ni takriban watu milioni 200).

Kaimu Meneja wa Huduma za Habari za Kiswahili katika TSN, Mgaya Kingoba anasema kuwa nia mojawapo ya kuanzishwa kwa gazeti hili ilikuwa ni kuitumia vema fursa ya kuuza bidhaa za Tanzania nje ya nchi, na moja ya bidhaa hizo ni Lugha ya Kiswahili.

“Tuliona hivyo kwa sababu Tanzania ina mchango mkubwa katika lugha hii na eneo hili la Afrika Mashariki kuna mwingiliano mkubwa wa Lugha ya Kiswahili kwa mfano nchi kama Kenya na Rwanda zina maeneo makubwa ya watu wanaozungumza Kiswahili fasaha,” anasema Kingoba.

Anaongeza: “Lakini pia tuliona sisi tuna mchango mkubwa wa kufundisha Lugha ya Kiswahili kwenye hizi nchi, kwa sababu Tanzania ni moja ya nchi ambazo duniani hapa Lugha ya Kiswahili inaongelewa tangu mtoto anapozaliwa. Kwa hiyo ni lugha ambayo sisi tunaiandika na kuizungumza kwa ufasaha zaidi pengine kuliko nchi nyingine zinazotuzunguka,” anasema Kingoba.

Mwaka jana, Bakita kwa kushirikiana na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) walilitunuku gazeti la HabariLEO tuzo ya gazeti bora linaloandika kwa weledi na kwa ufasaha Lugha ya Kiswahili kutokana na mchango wake katika kukuza lugha hii kwa weledi na ufasaha zaidi.

Gazeti la HabariLEO lilianzishwa Desemba 21, 2006.

Lilizinduliwa na Rais wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Kikwete na kuwa gazeti la Kwanza la Serikali la Kiswahili.

Ni matokeo ya maazimio ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, na azimio hilo likawekwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2005-2010 ikiitaka Serikali ya CCM kutekeleza hilo.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/deef97e5f41d3ccfc7438e510961ee5f.JPG

UTAPIAMLO sugu au udumavu kwenye baadhi ...

foto
Mwandishi: Fadhili Akida

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi