loader
‘Kiswahili fursa ya ajira, Watanzania changamkieni’

‘Kiswahili fursa ya ajira, Watanzania changamkieni’

LEO ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani, wataalamu na wadau wa Kiswahili wamesema Kiswahili ni lugha ya umoja na mshikamano.

Wataalamu na wadau hao walikuwa wakijibu hoja ya HabariLEO kuhusu mchango wa Kiswahili katika maendeleo ya sekta mbalimbali pamoja na mchakato wa Kiswahili kufundishwa katika maeneo mbalimbali duniani.

Mhadhiri Mwandamizi wa Taaluma za Kiswahili wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye pia ni Naibu Rais wa Chama cha Kiswahili Duniani, Dk Musa Hans, anasema si rahisi kwa Watanzania kuwa na maendeleo bila kuwa na umoja na mawasiliano, hivyo Kiswahili ni lugha ya umoja na mshikamano kwa Watanzania.

Anasema Kiswahili kinahitajika katika kujenga umoja na mawasiliano katika nyanja mbalimbali ikiwamo maeneo ya kazi kama vile viwandani, kwenye sekta ya elimu, kwenye masuala ya kawaida ya kijamii kama sherehe na mengine mengi kwa kuwa watu wanahitaji lugha ili kuwasiliana.

“Kwa Tanzania Kiswahili ni kiunganishi kwa watu mbalimbali katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pia ni utambulisho wa Watanzania, mtu akizungumza Kiswahili anajulikana kuwa Mtanzania,” anasema Dk Hans.

Dk Hans anabainisha kuwa Kiswahili ni fursa ya ajira kwa sababu kuna watu wanafundisha Kiswahili kwa wageni na wengine wanafanya kazi ya ukalimani, hivyo wataalamu wa Kiswahili nchini hawana budi kuchangamkia fursa hiyo.

Kuhusu jitihada za kukifanya Kiswahili kifundishwe katika maeneo mbalimbali duniani, anasema jambo la msingi katika hilo ni kuwapo kwanza kwa utashi wa kisiasa ambao kwa sasa unaonekana kwa kiasi kikubwa.

Anataja jambo la pili kuwa baadhi ya watu wanapaswa kuondoa kasumba waliyonayo kwa kudhani kuwa Kiswahili hakiwezi na hakifai kutumika kwa jambo fulani kitu ambacho si sahihi.

Dk Hans anasema kuwa baadhi ya watu wanafikia hatua ya kuona Kiswahili hakifai na kuamua kutumia lugha nyingine kwa kutumia maneno kama ‘lugha ya kitaalamu’ kwa maana kwamba Kiswahili hakiwezi kuwa na utaalamu huku wakisahau kuwa hata Kiingereza kina maneno mengi ya Kilatini, Kifaransa na lugha nyinginezo.

“Pia wataalamu wa Kiswahili wachangamkie fursa, kwa hiyo natoa wito kwa wataalamu wa Kiswahili kuziangalia jamii nyingine kwa kujifunza lugha nyingine kama Kifaransa, Kiarabu ili tuweze kueneza maarifa yetu kwa hao watu,” anasisitiza Dk Hans.

Katibu Mkuu wa Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira (TRAMEPRO), Bonaventura Mwalongo, anasema kila kinapotajwa Kiswahili inatangazwa nchi yaani Tanzania pamoja na mifumo yake ya mawasiliano.

Mwalongo anasema Kiswahili ni miongoni mwa nyenzo kubwa na muhimu kwa Watanzania na kinakwenda nje ya mipaka ya Bara la Afrika na kupanua wigo wa watu kujiamini kwa sababu baadhi ya watu walikuwa wanaona aibu kutumia Kiswahili, lakini kwa sasa kimekuwa moja ya lugha za kipaumbele.

“Hii ni hatua kubwa kwetu, pia tumeona Ubalozi wa Marekani kupitia Balozi Donald Wright, anasema yeye ni mwanafunzi wa Kiswahili, amekubali kujifunza Kiswahili na kafanya tukio maalumu la kuadhimisha Kiswahili, hii ni hatua kubwa kwetu Watanzania tujivunie,” anaeleza Mwalongo.

Anaongeza: “Juhudi ambazo zilianzishwa na waasisi wa taifa letu kwa kukipigania Kiswahili kama Lugha ya Taifa, lugha ya kutuunganisha, sasa inaenda kuwa lugha ya kuwaunganisha binadamu katika dunia hii tunayoishi.”

Ili Kiswahili kifundishwe katika maeneo mbalimbali duniani, Mwalongo anabainisha kuwa kuna haja ya kukiimarisha na kukijengea msingi ili kitoe fursa ya ajira kwa Watanzania kwenda kukifundisha kwenye mataifa mbalimbali duniani na hatimaye kichangie maendeleo ya nchi.

Kaimu Katibu Mtendaji wa Bakita, Consolata Mushi, amewahi kuliambia HabariLEO kuwa kuna fursa nyingi za Kiswahili ndani na nje ya nchi, lakini tatizo ni kwa Watanzania wenye utaalamu wa lugha hiyo kukosa uthubutu wa kuzitafuta na kuzitumia fursa hizo.

Anasema Watanzania ndiyo wenye lugha kwa kuwa ni mali yao, lakini hawajaitendea haki kwa kukosa uthubutu wa kutoka hadharani kutafuta nafasi au fursa kwa kutumia akili na maarifa yao yote.

“Sijui tuliathirika wapi? Mtu anasema mimi nasubiri tuambiwe kwamba nafasi ziko tayari nchi fulani twende. Nakumbuka kuna tuliowafundisha hapa, walipotoka na ule moto wa kutafuta fursa wakatengeneza kundi lao, wakaanza kuhangaika nchi mbalimbali kupitia balozi, ukatokea ubalozi mmoja ukawaambia wako tayari kuwachukua, lakini wakapewa masharti ya kujua Lugha ya Kiarabu,” anasema Mushi.

Anaongeza: “Lile kundi wakatafuta mwalimu wa kuwafundisha Kiarabu lakini wengine wakakata tamaa. Unaweza ukaona namna ambavyo mtu ukitafuta fursa, kwanza wewe mwenyewe uwe mbele, hata hao ambao wako huko, wengi hawakwenda kwa njia za serikali, ila ni wale wanaotafuta usiku kucha.”

Mushi anasema kuwa mafunzo ya Lugha ya Kiswahili wanayoyatoa hayalengi kuwafanya wanafunzi kufikiri kuwa ni lazima waende nje ya nchi kufundisha Kiswahili, bali wanawafundisha ujasiriamali kupitia lugha.

Anasema ujasiriamali huo kupitia lugha uwasaidie wanafunzi kutafuta fursa hizo nje ya nchi au kufanya kazi hiyo wakiwa hapa nchini.

“Kuna wengine wapo hapa nchini wanafundisha Kiswahili kwa kutumia Tehama na wanafaidika sana. Kwa hiyo sisi tulilenga kumuandaa mtu ambaye ama ametoka au hajatoka lakini anaweza akatumia elimu na utaalamu alionao katika kuiuza lugha na yeye akafaidika,” anasema Mushi.

Anabainisha kuwa wanafunzi ambao wameelewa dhana hiyo wameanza kunufaika kwa kuwa wapo waliokwenda nje ya nchi kwa jitihada zao na pia wapo waliofanikiwa kutumia ujasiriamali huo kupitia teknolojia ikiwemo kutengeneza vipindi kupitia youtube.

Kwa mujibu wa Mushi, kwenye kanzidata ya Bakita hadi Septemba mwaka jana kulikuwa na jumla ya wataalamu wa Lugha ya Kiswahili 1,325 waliowapatia mafunzo.

Alisema lengo lao ni kuhakikisha wanawasajili wataalamu wote wa Kiswahili na kuwagawa katika makundi ya ukalimani, wafasiri na walimu wa Kiswahili kwa wageni.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/44f6c808746dc1acdcb28681db712d69.jpg

UTAPIAMLO sugu au udumavu kwenye baadhi ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi